Monday, February 27, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yahamia Dodoma Rasmi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ofisini kwake Mjini Dodoma. Waziri Mahiga leo ameutangazia Umma wa Watanzania kuwa Wizara imehamia Dodoma rasmi.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU WIZARA KUHAMIA DODOMA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuufahamisha Umma kuwa tayari imeshahamia Dodoma kuanzia tarehe 17 Februari, 2017.  Hatua hiyo imehusisha Awamu Mbili, awamu ya kwanza imetekelezwa tarehe 28 Januari, 2017 na awamu ya pili imetekelezwa tarehe 17 Februari, 2017.

Miongoni mwa Watumishi waliohamia Dodoma katika awamu hii ya kwanza ni pamoja na Viongozi Wakuu na Watumishi wa Wizara wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Augustine P. Mahiga na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan A. Kolimba pamoja na Watumishi Kumi (10) waliofuatana nao.

Awamu ya pili iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima na Naibu Katibu Mkuu Balozi Ramadhan M. Mwinyi ambao waliongozana na Watumishi 33 wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika Uhamisho huu, jumla ya Watumishi 43 wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameungana na Viongozi wao Wakuu kwenye ofisi za Makao Makuu ya Wizara na Serikali Dodoma.

Mawasiliano ya Wizara yatakayotumika kuanzia sasa ni kama ifuatavyo:

Katibu Mkuu,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Barabara ya Makole,
S.L.P 2933,
Jengo la LAPF, Ghorofaya6,
DODOMA.

Namba za Simu: +255 (0) 262323201-7,
Nukushi           :  +255-26-2323208,
Barua pepe      :   nje@nje.go.tz
 Tovuti             : www.foreign.go.tz


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 27 Februari, 2017.

Mhe. Waziri Mahiga na Naibu Katibu Mkuu Balozi Ramadhani Mwinyi wakijadili jambo kabla ya kuanza kwa mkutano Ofisini Mjini Dodoma.

Waandishi wa habari wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri Mahiga kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje kuhamia Dodoma.

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akiwa katika picha na baadhi ya watendaji wa Wizara mjini Dodoma. 
Walioketi ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (wa pili kulia), Naibu Katibu Mkuu,  Balozi Ramadhani Mwinyi (wa kwanza kulia) Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bw. Nigel Msangi (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bw.Hamid Mbegu wakiwa katika picha ya pamoja na  watumishi wa Wizara Mjini Dodoma. 

Sunday, February 26, 2017

Rais Museveni amaliza ziara yake nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akiagana na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili hapa nchini.
Rais Museveni akiagana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga. Kushoto ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.). Kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi.
Rais Museveni akiagana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Bw. Elibariki Maleko akiagana na Rais Museveni
Rais Museveni akipunga mkono wa kwa heri kwa Rais Magufuli na Viongozi wengine walioshiriki kumuaga mara baada ya kumaliza ziara yake nchini.
Kutoka kulia ni Balozi wa Uganda nchini Mhe. Dorothy Hyuha, Balozi Shiyo, Mkuu wa Itifaki, Balozi Grace Martin, Mnikulu, Bw. Ngusa Samike na Balozi Zuhura Bundala, Mshauri wa Rais Masuala ya Diplomasia wakimuaga Rais Museveni (hayupo pichani) mara baada ya kumaliza ziara yake nchini.

Rais Magufuli awaapisha mabalozi wanne

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Pindi Hazara Chana. Hafla za uapisho zimeanyika leo jijini Dar es Salaam
Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Chana
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Khartoum, Sudan Mhe. Silima Kombo Haji. Hafla za uapisho zimeanyika leo jijini Dar es Salaam
Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Silima
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Mascut, Oman Mhe. Abdallha Abas Kilima. Hafla za uapisho zimeanyika leo jijini Dar es Salaam

Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Kilima
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Balozi wa Tanzania nchini Seoul, Korea Kusini, Mhe. Matilda Swila Masuka. Hafla za uapisho zimeanyika leo jijini Dar es Salaam
Mhe. Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Balozi Masuka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa nne kutoka kushoto), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassani Suluhu (wa tatu kutoka kushoto), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa (wa nne kutoka kulia), Katibu Mkuu Kiongozi Mhe Eng. John   Herbert Kijazi (wa pili kutoka kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Azizi Mlima (wa tatu kutoka kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wateule mara baada ya kuapishwa, Ikulu jijini Dar es Salaam.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Mabalozi wapya wanne waapishwa na kupangiwa vituo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo na kuwaapisha Mabalozi wapya wanne ambao uteuzi wao ulifanyika    tarehe 03 Desemba 2016. 

Mabalozi hao ambao waliapishwa leo na Mhe. Rais Ikulu jijini Dar Es Salaam ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana ambaye anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. John Haule. Mhe. Haule ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa  iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alistaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 2016.

Mhe. Chana kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Unaibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika Serikali ya awamu ya nne.

Balozi mwingine aliyeapishwa ni Mhe. Silima Kombo Haji anayekwenda kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Jamhuri ya Sudan baada ya Mhe. Rais kuamua kuufungua upya Ubalozi huo ambao ulifungwa miaka ya nyuma kutokana na sababu za kiuchumi. Kabla ya uteuzi huo Balozi Silima alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Walioapishwa pia ni Mhe. Abdallah Kilima ambaye anakwenda nchini Oman kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Ali Saleh aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Balozi Kilima kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea, Mhe. Matilda Masuka naye aliapishwa na Mhe. Rais leo. Balozi Masuka kabla ya kukabidhiwa majukumu hayo mapya alikuwa Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini China.   Jamhuri ya Korea ni moja kati ya nchi sita ambazo Mhe. Rais Magufuli amefungua Balozi mpya. Nchi nyingine ni Algeria, Jamhuri ya Sudan, Uturuki, Israel na Qatar.

  Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 26 Februari, 2017.




Saturday, February 25, 2017

Tanzania yaahidi kuimarisha Diplomasia ya Uchumi na Uganda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Uganda hapa nchini, Mhe. Yoweri Museveni (anayeonekana ameketi kulia). Katika hotuba yake Rais Magufuli aliahidi kuimarisha urafiki na undugu uliodumu kwa miaka mingi baina ya mataifa hayo mawili.
Mhe. Rais Museveni nae akihutubia katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini.
 Pamoja na kuzungumzia masuala ya ushirikiano wa kidiplomasia, Rais Museveni aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuikomboa  Uganda dhidi ya adui Nduli Idd Amin Dada na ukombozi wa kiuchumi kwa kujenga reli ya kati " standard gauge" ambayo itaenda sambamba na ujenzi wa bandari kavu "Dry Port" Jijini Mwanza ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo ya Uganda kutoka Bandari ya Dar es Salaam. 
Sehemu ya Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Serikali ya Tanzania waliohudhuria mkutano huo ambao ulitanguliwa na hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano katika masuala ya Siasa na Diplomasia. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Kimataifa wa Uganda, Mhe. Okello Oryem wakisaini Mkataba wa Ushirikiano katika masuala ya Siasa na Diplomasia.
Wakibadilishana mkataba mara baada ya kuusaini.
Marais wakipongezana mara baada ya kutoa hotuba.

Rais Museveni awasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili


Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli akimkaribisha nchini Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha Julius Nyerere tayari kwa kuanza ziara ya siku mbili hapa. Katika ziara hiyo Mhe. Museveni anatarajiwa kufanya mzungumzona mwenyeji wake Magufuli pamoja na kutembelea Kiwanda cha Azam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akiwa  na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Kassim Majaliwa (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) wakati wa mapokezi ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni
Rais Museveni pamoja na mwenyeji wake Rais Dkt. Magufuli wakisikiliza nyimbo za mataifa yao
Makamu wa Rais akiwa uwanja wa ndege na Viongozi mbalimbali wa ngazi za juu Serikalini wakati wa mapokezi ya Rais Museveni.
Rais Museveni pamoja na Rais Magufuli wakitizama moja ya kikundi cha ngoma kilichokuwa kikitoa burudani uwanjani hapo.
Rais Yoweri Kaguta Museveni pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakizungumza jambo.
===================================================
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 


Tanzania na Uganda sio nchi rafiki tu bali ni ndugu wa kweli lakini Kiwango cha biashara kati ya nchi hizo hakitafsri ipasavyo ukubwa wa udugu na urafiki uliopo kati ya yao. 

Hayo yalibainishwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam akiwa na Mgeni wake Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni. 

Rais Museveni yupo nchini Tanzania kwa ziara ya Kiserikali ya Siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26 Februari 2017.

“Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 126.744 mwaka 2016 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 99.882 zilizouzwa mwaka 2015”. “Hiki ni kiwango kidogo sana ukilinganisha na udugu mkubwa tulionao kati ya nchi zetu mbili”alisema Dkt. Magufuli.

Rais Magufuli alieleza kuwa ili kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, Serikali yake imeanza mkakati wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam-Mwanza-Isaka hadi Burundi na Rwanda. Rais Magufuli alisema pia kuwa Serikali itajenga Bandari Kavu jijini Mwanza ili kuwarahisishia wafanyabiashara wa Uganda kuchukulia bidhaa zao Mwanza badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam. 

Sanjari na hayo Serikali itaboresha bandari ya Bell na itapunguza vizuizi vya barabarani na kubaki vitatu ili kupunguza muda mwingi unaopotezwa na malori ya mizigo kwenye vizuizi hivyo.

Kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga, Rais Magufuli alisema Serikali yake ilishafanyia kazi vikwazo vyote saba vilivyowasilishwa ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kutoa mwito kwa mwekezaji kuanza ujenzi wa bomba hilo haraka kwani hakuna kisingizio kingine. Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa kupanga tarehe ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba hilo  na kwamba yupo tayari kusafiri kwenda nchini Uganda kama itakubalika jiwe hilo kuwekwa nchini humo. 

Aidha, Rais Magufuli alizungumzia jitihada za Serikali yake kufufua Shirika la Ndege la ATCL kwa kununua ndege sita kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga nchini na nchi jirani. Alimuomba Rais Museveni muda utakapofika ndege hizo ziweze kwenda Uganda jambo ambalo liliafikiwa.

Akizungumzia Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Umoja wa Ulaya (EPA), Rais Magufuli aliuona mkataba huo kama kikwazo katika juhudi za Serikali za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. Hivyo alimuomba Rais Museveni kumuunga mkono kuepuka mkataba huo kwa manufaa ya wananchi wa EAC.

“Rais Museveni alibebwa na Tanzania wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo namuomba Rais Museveni naye anibebe katika suala hili la EPA kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu na Jumuiya yetu” alisisitiza Rais Magufuli. 

Kwa upande wake, Rais Museveni alibainisha kuwa, hadi leo tatizo kubwa kwa Bara la Afrika lililopelekea hadi kutawaliwa na wakoloni huko nyuma ni ukosefu wa umoja na msimamo wa pamoja.  Alisema amekuja Tanzania kujadiliana na Rais Magufuli ili kupata msimamo wa pamoja kuhusu Mkataba wa EPA wenye manufaa kwa wananchi kwani undugu na umoja  uliopo kati ya nchi hizi mbili ni zaidi ya mkataba huo.

Kuhusu mpango wa Tanzania kujenga reli ya kiwango cha kimataifa, Rais Museveni aliupongeza mpango huu na kuutaja kama mchango wa pili wa Tanzania katika ukombozi wa Uganda. Alisema reli hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa uchumi wa Uganda kwa kuwa utakuwa ni usafiri wa haraka na gharama nafuu.

Rais Museveni kabla ya kuondoka nchini kesho tarehe 26 Februari 2017 atatembelea kiwanda cha AZAM kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam. AZAM pia imefanya uwekezaji nchini Uganda.  


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam, 25 Februari, 2017