TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mabalozi
wapya wanne waapishwa na kupangiwa vituo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo na kuwaapisha
Mabalozi wapya wanne ambao uteuzi wao ulifanyika tarehe 03 Desemba 2016.
Mabalozi hao ambao waliapishwa leo
na Mhe. Rais Ikulu jijini Dar Es Salaam ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya,
Mhe. Dkt. Pindi Chana ambaye anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. John Haule.
Mhe. Haule ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa
iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alistaafu
kwa mujibu wa sheria mwaka 2016.
Mhe. Chana kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi
aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Unaibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto katika
Serikali ya awamu ya nne.
Balozi mwingine aliyeapishwa ni Mhe.
Silima Kombo Haji anayekwenda kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Jamhuri
ya Sudan baada ya Mhe. Rais kuamua kuufungua upya Ubalozi huo ambao ulifungwa
miaka ya nyuma kutokana na sababu za kiuchumi. Kabla ya uteuzi huo Balozi
Silima alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar katika Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Walioapishwa pia ni Mhe. Abdallah
Kilima ambaye anakwenda nchini Oman kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Ali
Saleh aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Balozi Kilima kabla ya kuteuliwa
kushika wadhifa huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini
Jamhuri ya Korea, Mhe. Matilda Masuka naye aliapishwa na Mhe. Rais leo. Balozi
Masuka kabla ya kukabidhiwa majukumu hayo mapya alikuwa Mkuu wa Utawala katika
Ubalozi wa Tanzania nchini China.
Jamhuri ya Korea ni moja kati ya nchi sita ambazo Mhe. Rais Magufuli amefungua
Balozi mpya. Nchi nyingine ni Algeria, Jamhuri ya Sudan, Uturuki, Israel na
Qatar.
Imetolewa
na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 26 Februari,
2017.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.