Sunday, February 12, 2017

Taarifa kwa vyombo vya Habari


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MABALOZI WATATU WAPANGIWA VITUO VYA KAZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu ambao aliwateua tarehe 3 Disemba 2016.

Mabalozi hao waliopangiwa vituo ni Mhe. Joseph Sokoine anayekuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Omar Yussuf Mzee anayekuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Algeria na Mhe. Grace Mgovano anayekwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Dkt. Ladislausi Komba nchini Uganda ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Balozi Sokoine ambaye anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nafasi ya mwisho alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza ya Mhe.  Rais Dkt. Ali Mohammed Shein.

Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Ubalozi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.

Mabalozi wote waliopangiwa vituo vipya vya kazi wataapishwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho siku ya Jumapili tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu jijini Dar Es Salaam saa tano asubuhi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki,
Tarehe 11 Februari 2017

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.