Wednesday, February 15, 2017

Taarifa ya Serikali kuhusu Watanzania waliopata matatizo nchini Msumbiji

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba (Mb.), amezungumza na waandishi wa habari, kufafanua suala la Watanzania waliopata matatizo ya kufukuzwa nchini Msumbiji. Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wote wanaosafiri kwenye nchi nyingine kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu ikiwemo kupata vibali halali vya kukaa kwenye nchi husika. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Innocent Shiyo na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga.
Sehemu ya waandishi wa habari wakimsikiliza Dkt. Kolimba (hayupo pichani), alipokuwa akizngumza nao.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
==================================================



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu Watanzania waliopata matatizo nchini Msumbiji

Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez ulio Cabo Delgado, Jamhuri ya Msumbiji.
Serikali ya Msumbiji imekiri kuwepo kwa operesheni maalum ya kuwakamata na kuwarudisha raia wa nchi za kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata Sheria za Uhamiaji za nchi hiyo. Aidha, Serikali hiyo imetaarifu kwamba, zoezi hilo limeanzia mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.

Kufuatia hali hiyo, Ubalozi wetu nchini Msumbiji upo eneo la tukio ili kufuatilia suala hili na mamlaka husika. Aidha, unaendelea kufanya mawasiliano ya Kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao, unapewa kipaumbele. Inakadiriwa kuwa Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.

Kuanzia zoezi hilo lilipoanza, Raia wa Tanzania wapatao 132 wamesharudishwa nchini. Tarehe 11/02/2017 walirejeshwa raia 58. Tarehe 14/02/2017 wamerejeshwa raia 24 na leo tarehe 15/02/2017 wamesharejeshwa raia 50.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na jirani yetu Msumbiji ni mzuri, na hivyo itafanya kila jitihada kuhakikisha hali ya usalama wa Watanzania na biashara zao, inarudi kuwa shwari na kwa wakati. Mwezi Desemba 2016, Tanzania na Msumbiji zilifanya mkutano wa ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano. Mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pemba, Cabo Delgado uliainisha maeneo ya ushirikiano yakiwemo masuala ya biashara na uhamiaji.

Serikali inaendelea kuwakumbusha Watanzania waishio ughaibuni, kufuata Sheria na taratibu za nchi hizo, ikiwemo kuwa na vibali halali vya makazi na biashara.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

15 Februari, 2017

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.