Monday, February 6, 2017

Tanzania na Malawi zasaini kushrikiana katika mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia na usafiri wa anga

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba ya kufunga kikao cha JPCC kati ya Tanzania na Malawi kilichofanyika Liolongwe. kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Ramadhan Mwinyi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Francis Kasaila akiwasilisha hotuba katika kikao cha JPCC kati ya Tanzania na Malawi

Wajumbe wa kikao cha JPCC wakifuatilia kwa makina hotuba za Mawaziri wa Mambo ya Nje zilipokuwa zinawasilishwa

Sehemu nyingine ya ujumbe ikifuatilia hotuba za Mawaziri

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Malawi na Tanzania wakiweka saini mikataba ya kushirikiana katika Mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia na usafiri wa anga. Nyuma ya Waheshimiwa Mawaziri, kulia ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Bw. Mustafa Usi na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi.

Waheshimiwa Mawaziri wakibadilishana mikataba baada ya kuisaini

Waziri Mahiga akisalimiana na wajumbe mbalimbali. Anayeshikana naye mkono ni Bi. Elizabeth Rweitunga, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje.

Picha ya pamoja kati ya Waheshimiwa Mawaziri na wajumbe walioshiriki kikao cha JPCC.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Malawi zasaini kushrikiana katika mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia na usafiri wa anga

 Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi kimeweka mazingira mazuri ya kushughulikia mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa ambapo juhudi za kutafuta suluhu zilisimama kutokana na mabadiliko ya uongozi nchini Malawi.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt, Augustine Mahiga (Mb) wakati alipokuwa anasoma hotuba ya kufunga kikao hicho jijini Lilongwe siku ya Jumapili tarehe 05 Februari 2017.

Mhe. Waziri alieleza kuwa kikao hicho kimefanyika kufuatia maelekezo ya Waheshimiwa Marais wa Tanzania na Malawi ambao walifanya mazungumzo walipokuwa Ethiopia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika na kutoa wito kwa jopo la viongozi wa zamani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuongeza kasi ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Jopo la viongozi wa zamani wa SADC lililopewa dhamana ya kushughulikia suala hilo linaundwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais wa zamani wa Msumbiji; Mhe. Thabo Mbeki, Rais wa zamani wa Afrika Kusini  na Mhe. Festus Mogae, Rais wa zamani wa Botswana.

Waziri Mahiga alieleza kuwa japo Tanzania na Malawi zinatofautiana katika mpaka wa Ziwa Nyasa lakini tofauti hizo sio kikwazo kwa nchi hizo kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya faida ya wananchi wa pande zote mbili.
 Alisema kikao hicho cha JPCC kinatoa fursa kwa pande mbili kujadili na kukubaliana maeneo mbalimbali ya ushirikiano na kuweka utaratibu wa utekelezaji.

Aidha, katika kikao cha JPCC, wajumbe wanakitumia kubuni mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyoafikiwa.

 “Nafurahi kusikia mmejadili na kukubaliana maeneo mengi ya ushirikiano ikiwemo biashara, kilimo, utalii, tehama, utangazaji, utunzaji wa mazingira na usafiri wa anga”. “Ni jambo la kupongezwa katika majadiliano yenu pia mmependekeza iundwe Kamati ya Makatibu Wakuu ambayo itakuwa inakutana kila baada ya miezi sita ili kutathmini utekelezaji wa maeneo yaliyoafikiwa kwa mujibu wa muda uliokadiriwa”.  

Mhe. Mahiga alitoa maelezo namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyoboresha miuondombinu ya Bandari ya Dar Es Salaam, barabara na mipango ya kuboresha Reli ya TAZARA kwa kushirikiana na China ili Malawi iweze kusafirisha bidhaa zake kwa urahisi.

“Ni jukumu letu na pia ni wajibu wa kimataifa kuzihudumia nchi zisizokuwa na bandari. Hivyo, Tanzania ambayo imezungukwa na nchi nane zisizokuwa na bandari itaboresha miundombinu ili nchi hizo ziweze kusafirisha bidhaa zao bila usumbufu wowote.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mhe. Francis Kasaila alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya bandari, barabra na reli ili Serikali ya Malawi na wafanyabiashara waweze kusafirisha bidhaa kwa urahisi. Alisema ili vituo vya mizigo vya Malawi vilivyopo Dar es Salaam na Mbeya vifanye kazi kwa ufanisi hakuna budi kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, Reli ya TAZARA, barabara ya Dar es Salaam hadi Mbeya na kujenga Kituo cha Pamoja cha kutoa Huduma mpakani.

Kikao hicho kilimalizika kwa kushuhudiwa uwekaji saini wa mikataba ya makubaliano katika Mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia na usafiri wa anga.

Mhe. Waziri kabla ya kurejea Dar es Salaam siku ya Jumatatu amepangiwa miadi ya kuonana na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Prof. Peter Mutharika ambapo amepanga pamoja na mambo mengine kujadili suala la Watanzania wanane wanaoshikiliwa katika gereza kuu la Mzuzu kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.



Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 06 Februari 2017

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.