Tuesday, October 25, 2016

Wamisri watangaziwa fursa za Uwekezaji za hapa nchini


Mhe. Mohammed Haji  Hamza, Balozi wa Tanzania nchini Misri akiwakaribisha wageni waliohudhuria katika ufunguzi wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na misri lililofanyika  katika miji ya Cairo na Alexandria kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba 2016.
Kongamano hili lililowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili lilifunguliwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Mhe Balozi Amina Salim Ali. Kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali zinahusika na uwekezaji, biashara, ujenzi, usafirishaji, elimu, afya, viwanda, uhandisi ,kilimo na utalii. Kongano hilo liligharmiwa na kuratibiwa  kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Jumuiya za Wafanyabiashara wa Misri na makampuni binafsi ya biashara ya Misri.
Katika kongamano hilo washiriki wa Tanzania pamoja na kutoa mada zilizohusu fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na hasa katika sekta ya viwanda na utalii pia walipata fursa ya kushiriki katika mazungumzo  ya ana kwa ana ya kibiashara.
Siku ya pili ya kongamano hili washiriki kutoka Tanzania walipata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali za uzalishaji na huduma zikiwemo: kijiji cha teknolojia cha Cairo, viwanda vya utengezaji madawa, vifaa tiba na rangi za ujenzi mjini Cairo pamoja na viwanda vya nguo, vifaa vya ujezi na samani za chuma katika miji wa Tenth Ramadhani .  Siku ya tatu ya kongamano hilo baadhi ya washiriki kutoka Tanzania walitembelea vyuo vikuu vya Alexandria na chuo kikuu cha kiarabu cha sayansi, teknolojia na usafiri wa bahari mjini Alexandria na kuwa na mazungumzo ya ushirikiano na viongozi wa vyuo vikuu hivyo. Ujumbe wa Tanzania pia ulipata nafasi ya kutembelea kiwanda cha kutengenezea manukato kilichopo nje kidogo ya jiji la Akexandria.

Akiwa jijini Cairo, Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo alipata nafasi ya kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Misri, Rais na Mtendaji Mkuu wa  Afri exim bank na Katibu Mkuu wa Wakala wa Ushirikiano na Maendeleo wa Misri.. 

Vingozi mbalimbali walioshiriki kwenye ufunguzi wa konganano la kibiashara mjini Cairo siku ya  tarehe 17 Oktoba 2016 wakisimama wakati wa Nyimbo za Taifa za Tanzania na Misri zilipopigwa. Wa kwanza kutokea kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda wa Misri. Wa pili ni Katibu Mkuu wa Wakala wa Ushirikiano na Maendeleo wa Misri, watatu ni Mhe Balozi Amina Salim Ali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Mohamed Haji Hamza , watano ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar na wa sita ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Biashara ya Misri. Waliosimama mbele ya meza kuu ni Mabalozi kutoka nchi za  SADC waliopo mjini Cairo.

Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Zanzibar akifuatilia neno la ukaribisho kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Mhe. Mohammed Haji Hamza
Balozi Hamza akisalimiana na kubadilishana mawazo na washiriki mbalimbali wa kongamano la biashara jijini Cairo mara baada ya ufunguzi kukamilika.

Monday, October 24, 2016

Waziri Mahiga ahimiza umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa

WAZIRI MAHIGA AHIMIZA UMUHIMU WA SOMO LA UMOJA WA MATAIFA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine mahiga amependekeza ni vema somo la Umoja wa Mataifa likaingizwa katika mitaala ya masomo, ameeleza hayo alipokuwa akihutubia  katika kilele cha Maadhimisho ya 71 ya Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo Waziri Mahiga alisema “Maadhimisho haya ni muhimu  kwa historia ya nchi yetu kwakua yanawezesha vizazi vyetu kuelewa historia ya nchi yetu na Shirika la Umoja wa Mataifa tangu kupatikana kwa Uhuru hivyo ni vyema Walimu na Wadau wote katika Sekta ya Elimu wakatilia mkazo umuhimu wa somo la Umoja wa Mataifa katika shule zetu za Msingi na Sekondari.”

Vilevile ameeleza umuhimu na mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa Tanzania na  kwa nchi wanachama wengine wa Umoja huo ni pamoja na kutengeneza agenda ya kimataifa ya maendeleo; kuleta amani hususan baada ya vita ya kwanza na  ya pili ya Dunia; vilevile Shirika hilo limekuwa likiendelea kuhakikisha amani na Ulinzi inapatikana katika mataifa yenye migogoro ambapo Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikishiriki katika masuala ya ulinzi wa amani katika baadhi ya mataifa kama Lebanon, Sudan Kusini (Dafur) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Pamoja na hayo ameeleza kuwa kupitia shirika la umoja wa Mataifa Tanzania imefanikiwa kuwa na  wawakilishi wa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa ambao pamoja na shughuli nyingine za mashirika hayo yamekuwa yakifadhili na kushiriki katika shughuli za maendeleo ambapo wastani wa bilioni za fedha za miradi ya maendeleo zimekuwa zikitolewa kwaajili ya miradi ya maendeleo. Vilevile Mahakama ya Umoja wa mataifa ya mauaji ya kimbari iliamuriwa kujengwa nchini Tanzania ambapo makao makuu yake yapo Jijini Arusha licha ya kumalizika kwa kesi majengo pamoja na nyaraka zote zilizokuwa zikitumika zimeendelea kubaki nchini kama kumbukumbu za marejeo.

Naye Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Alvaro Rodriguez alieleza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs), umuhimu wa kutunza amani na kuheshimu haki za binadamu sambamba na usawa wa jinsia.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa yanayowakilisha nchi zao hapa nchini. Wengine ni wadau wa maendeleo kutoka Sekta binafsi na taasisi za Serikali. 


Mfalme wa Morocco aendelea na ziara nchini

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 



Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
             11466 DAR  ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MFALME WA MOROCCO AENDELEA NA ZIARA NCHINI

Mfalme wa Morocco, Mtukufu Mohammed VI aliyewasili jana kwa ziara ya kitaifa, ameendelea na ziara yake nchini ambapo leo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano ya Tanzania na Morocco katika maeneo mbalimbali ya Kidiplomasia, Siasa, Uchumi, Ulinzi na Ustawi wa Jamii.

Akielezea mahusiano ya Tanzania na Morocco, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alisema kuwa ziara hii ni matokeo ya  Mhe. Rais kuridhia ujio huo wa Mfalme wa Morocco na ujio wake umekuwa ni maalum sana kwa kuwa unakumbushia historia iliyowekwa na mgeni wa kwanza kutoka Morocco, Bw. Iban Batutu aliyetembelea Tanzania eneo la Kilwa Mwaka 1631.

Baada ya mazungumzo,  Mhe. Rais Magufuli na Mgeni wake, Mtukufu Mfalme wa Morocco walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 22 ambayo inalenga kuendeleza sekta mbalimbali kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Morocco.

Baadhi ya Mikataba hiyo ni Makubaliano baina ya Benki ya Kilimo ya Tanzania na Benki ya Kilimo ya Morocco  ili kuwawezesha wakulima wetu kusindika mazao yao na kuyasafarisha nje yakiwa yamekamilika, Makubaliano baina ya Kampuni ya Mbolea ya Morocco na ya Tanzania ambapo kwa pamoja zitabadilishana uzoefu na utaalamu kwa lengo la kuiwezesha kampuni ya Tanzania kuzalisha mbolea ya kutosha kulingana na mahitaji, Makubaliano katika Sekta ya Anga ambapo katika siku za usoni Shirika la Ndege la Morocco litaanzisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Rabat hadi Dar es Salaam.

 Makubaliano mengine ni pamoja na kusaidia wakulima wadogo wadogo, kuendeleza Sekta ya Utalii ya Tanzania hususan katika fukwe za Zanzibar na hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro, makubaliano  baina ya Shirika la reli la Tanzania na lile la Morocco ambapo watashirikiana  kuboresha usafiri  wa reli kwa madhumuni ya kupunguza gharama za uzalishaji pamoja na kuendeleza reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga.

Viongozi hao pia walishuhudia uwekaji saini ya Mkataba baina ya Kampuni ya chai ya Tanzania na ile ya Morocco kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kutengeneza chai yenye ubora wa hali ya juu ili iweze kupata soko nchini Morocco na nchi nyingine.

Aidha, akiongea katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Bw. Salahddine Mezouar amesema wakati sasa umefika nchi hizi kupeleka mbele mahusiano yao na hii ndio sababu kubwa iliyopelekea nchi hizi mbili kukubaliana kusaini jumla ya mikataba 22, amesema nchi ya Morocco imefurahishwa na utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuri.

Mtukufu Mfalme atahitimisha ratiba yake kwa siku ya leo kwa kushiriki dhifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli  Ikulu, Dar es Salaam.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 24 Septemba 2016

Rais Magufuli ampokea Mfalme Mohammed VI wa Morocco Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Mfalme Mohammed VI wa Morocco wakipungia mikono wananchi waliojitokeza kwenye mapokezi ya Mfalme huyo Ikulu Jijini Dar es Salaam
Mfalme Mohammed VI wa Morocco akisalimia wananchi waliojitokeza kumpokea Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mfalme Mohammed VI wa Morocco mara baada ya Mfalme huyo kuwasilia Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mfalme Mohammed VI wa Morocco wakiwa katika Mazungumzo, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza katika hafla ya kutoa taarifa ya mazungumzo maalum, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika hafla ya kutoa taarifa ya mazungumzo maalum, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Tanzania yaungana na Nchi zingine Duniani kuadhimisha kilele cha Siku ya Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na watendaji wa mashirika mbalimbali ya Kimataifa yaliyopo Nchini kwenye maadhimisho ya kilele cha Siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika katika viwanja vya Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa amesimama sehemu maalumu wakati wimbo wa taifa ukipigwa
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akikagua gwaride maalum katika maadhimisho  ya kilele ya Siku ya Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria maadhimisho ya Kilele ya Umoja wa Mataifa
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akihutubia kwenye maadhimisho ya kilele ya Siku ya Umoja wa Mataifa 
Baadhi ya wanafunzi wenyemahitaji maalum wakiwa wameshikilia mabango ya malengo 17 ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa

Sunday, October 23, 2016

Rais Magufuli ampokea Mfalme Mohamed VI wa Morocco

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Mfalme H.M Mohammed VI wa Morocco wakati wimbo wa Taifa ukipigwa mara baada ya Mfalme huyo kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. 
Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mfalme Mohamme VI wa Morocco
Mfalme Mohamed VI akipungia wananchi waliojitokeza kumpokea uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

Friday, October 21, 2016

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza awasilisha Hati za Utambulisho kwa Malkia Elizabeth II

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akisalimiana na Malkia Elizabeth II wa Uingereza mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya nchi hiyo ya Buckingham kwa ajili ya kuwasilisha Hati za Utambulisho. Kulia ni mwenza wa Dkt. Migiro, Prof. Cleophas Migiro.
Mhe. Balozi Dkt. Migiro akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Malkia Elizabeth II wa Uingereza huku mwenza wake Prof. Migiro akishuhudia
Malkia Elizabeth II akisalimiana na Prof. Cleophas Migiro
Malkia Elizabeth II akizungumza na Mhe. Balozi Migiro 

Waziri Mahiga akutana na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza muda wake

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza  Muda wake Mhe.Mehdi Aghajafari. Balozi Mhe. Mehdi Aghajafari wiki ijayo anatarajia kuondoka Nchini kurejea Iran. 
Kutoka Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Abdalah Kilima, maafisa kutoka Wizarani Bi. Zainab Angovi, Bw. Gerald Mbwafu na Kisa Doris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Balozi wa Iran Nchini aliyemaliza muda wake Mhe.Mehdi Aghajafari wakionesha zawadi ya picha iliyokabidhiwa Mhe. Balozi


Wakati huo huo Waziri Mahiga amekutana na kuongea na Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem  

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Agustine Mahiga akimsikiliza Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem wakati wakifanya mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam


Waziri Mhe. Mahiga akielezea jambo wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait Nchini Mhe. Jasem Al-Najem. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati Balozi Abdallah Kilima akifuatilia mazungumzo.

Tanzania na Uswisi zasaini Mkataba wa Makubaliano kuhusu ushirikiano wa kisheria kwenye masuala ya Jinai

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) kwa pamoja na Mhe. Florence Tinguely Mattli, Balozi wa Uswisi hapa nchini wakisaini Mkataba wa Makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uswisi kuhusu Ushirikiano wa Kisheria kwenye masuala ya Jinai. Mkataba huu utasaidia kuzijengea uwezo mamlaka zinazohusika na masuala ya Jinai na pia kubadilishana taarifa kuhusu masuala hayo.
Mhe. Mahiga na Mhe. Mattli wakiendelea na zoezi la kusaini huku Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozini wakishuhudia. Kulia aliyesimama ni Bw. John Pangipita, Afisa Mambo ya Nje na Bi. Sheila Ally.
Tukio hilo pia lilishuhudiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Balozi Joseph Sokoine (wa pili kutoka kushoto), Katibu wa Waziri, Bw. Gerald Mbwafu na Bw. Pangipita (wa pili kutoka kulia)
Dkt. Mahiga pamoja na Balozi Mattli wakibadilishana Mkataba mara baada ya kumaliza kuweka saini.

Thursday, October 20, 2016

Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco kufanya ziara ya siku tatu nchini

Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea na Wahandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara rasmi ya siku tatu ya Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco nchini. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara Jijini Dar es Salaam.  Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco anatarajiwa kuanza ziara hiyo tarehe 23 hadi 25 Oktoba, 2016.
Baadhi ya wanahabari wakimsikiliza Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje atembelea Ofisi za Mambo ya Nje Zanzibar

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akizungumza na Watumishi wa Wizara waliopo Ofisi ya Wizara ya Zanzibar. Wengine ni baadhi ya Watumishi wakimsikiliza akiwemo Mkurugenzi wa Idara hiyo, Balozi Silima Haji (wa kwanza kulia)
Naibu Waziri Mhe. Dkt Susan Kolimba akitoa maelekezo kwa watumishi hao
Baadhi ya Watumishi wakimsikiliza Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan Kolimba (hayupo pichani)

Wednesday, October 19, 2016

Waziri Mahiga azungumzia maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Mhe. Balozi Dkt. Mahiga, amezungumzia umuhimu wa maadhimisho wa Siku ya Umoja wa Mataifa na faida za Jukwaa la umoja huo kwa maendeleo ya Taifa. Maadhimisho hayo yatafikia kilele tarehe 24 Oktoba, 2016
Mhe. Waziri akiendelea kuzungumza na waandishi wa habari
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) akifuatilia mkutano. Kulia ni Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bi.Chansa Kapaya
Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
 Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bi.Chansa Kapaya akizungumza na waandishi wa habari.

                                                   

                          

TAARIFA YA PAMOJA YA UMOJA WA MATAIFA NA SERIKALI

             YA TANZANIA KWA VYOMBO VYA HABARI


Imezuiwa hadi Oktoba 19, 2016, Mchana kwa saa za Afrika Mashariki.


MAADHIMISHO YA MIAKA 71 YA UMOJA WA MATAIFA YASISITIZA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU

’Wito watolewa kwa kila mwananchi kuwajibika kwa malengo ya Dunia’

Oktoba 19, 2016 Dar es Salaam – OKTOBA 24 kila mwaka Umoja wa Mataifa hufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.

Mwaka huu mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na serikali, wadau wa maendeleo na vijana wataadhimisha miaka 71 ya uwapo wa Umoja wa Mataifa kwa staili ya aina yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mkutano wa waandishi wa habari na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikishirikiana na Umoja wa Mataifa , maadhimisho hayo mwaka huu yamelenga kuelezea kwa undani shughuli zinazofanywa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ili kuwezesha maendeleo endelevu.
Katika mkutano huo wa pamoja, waandishi wa habari walielezwa kwa ufupi Mpango Mpya wa Maendeleo Chini ya Ufadhili wa Umoja wa Mataifa ( UNDAP ll -2016 hadi 2021) kwa serikali ya Tanzania; na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa Tanzania ambamo malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) kama yalivyosanifiwa na kukubalika na jumuiya ya kimataifa, yameshirikishwa.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari pia kulikuwepo na majadiliano  ya mafanikio ya shughuli za Umoja wa Mataifa hadi sasa duniani na pia nchini Tanzania .

Pia mazungumzo hayo yalijikita katika malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na umuhimu wa malengo hayo kumilikishwa kwa wananchi na wajibu wao katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na utekelezaji wenye mafanikio.

Pia ilielezwa katika mkutano huo kwamba maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa, Siku ya Umoja wa Mataifa, yatafanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam Oktoba 24.

Maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yamebeba ujumbe wa :“Uwezeshaji wa vijana Tanzania kufikia malengo ya dunia” yanafanyika huku kukiwa na malengo mapya ya dunia ya maendeleo endelevu.Malengo hayo ya SDGs yamelenga kuondoa umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.

Aidha ujumbe huo unaenda sanjari na mpango wa maendeleo wa awamu ya pili wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania (UNDAP II) ambao unaendeleza ule wa awali wa kuanzia 2011-16 ukiwa umejikita katika masuala ambayo ni muhimu kwenye kukabili umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya mwaka huu yalitanguliwa na  kongamano la vijana wapatao 200, ambao walijadili masuala yanayogusa fursa za uchumi na maendeleo ya jamii na mchango ambao unaoweza kutolewa na vijana kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo.

Maadhimisho hayo yatafikia kilele chake nchini kwa tukio litakalofanyika Visiwani Unguja  Oktoba 26 mwaka huu.

Imeelezwa kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaonesha uwapo wa ushirikiano mkubwa na wenye tija kati ya Tanzania, wananchi wake na Umoja wa Mataifa.

Aidha maadhimisho hayo yanaonesha ni kwa namna gani pande zote zipo tayari kutekeleza mipango ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania yenye lengo la kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Akizungumza umuhimu wa ushirikiano huo katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano, ukiwa ni mpango wa wananchi wenyewe, Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Augustine Mahiga, alielezea Tanzania kuunga mkono Umoja wa Mataifa ukifanyakazi kama taasisi moja  na kuwataka watengeneza sera kuhakikisha kwamba wananchi wote wananufaika na ushirikiano huu wa Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Waziri Mahiga alisisitiza wakati Tanzania inajikita katika kutekeleza mpango wake mpya wa taifa wa maendeleo, kuna haja ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaelewa na kumiliki mpango huo ambao umejumuisha  malengo ya maendeleo endelevu.

Alisema: “Tanzania imeshirikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) katika sera za taifa na pia katika mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo ya msingi yanayohitaji uangalizi kufanikisha maendeleo endelevu”. 

Hata hivyo aliongeza kusema kwamba: “ Hiyo inajulikana wazi kwamba serikali pekee haiwezi kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu bila msaada wa sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo, na hivyo iko haja ya kushirikishana.  Tunaitaka sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo kujiunga nasi katika juhudi hizi kwa kutuwezesha kifedha ili tuweze kutekeleza mipango yetu ya maendeleo. Tunachohitaji sisi tunaofanyakazi katika ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha kwamba hatutamwacha yeyote nyuma katika harakati zetu za kuleta maendeleo”.

Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez akizungumzia maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa na uhusiano wake alisema: “Tanzania na Umoja wa Mataifa zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa miongo mingi. Wakati Tanzania sasa inabadilika, msaada unaotolewa na Umoja wa Mataifa unatakiwa kukidhi haja mpya, hasa taifa linapoelekea katika uchumi wa kati”.
Pia katika hotuba yake aliongeza kwamba: “Malengo ya maendeleo endelevu ni muhimu katika ushirikiano wetu kwani unaweka umuhimu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania za kusaidia kupatikana kwa mafanikio katika nyanja za uchumi, ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.”

Angalizo kwa wahariri:
Umoja wa Mataifa wa sasa ulianza shughuli zake Oktoba 24, 1945 na katika miaka yake 71 imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba duniani kunakuwa mahali bora pa kuishi kwa kuwa na amani, maendeleo na kulinda heshima ya kila mwanadamu. Nchini Tanzania, Umoja wa Mataifa unanufaika na ushirikiano wake na serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kuhudumia wananchi.

Kwa taarifa zaidi  kuhusu juma la Umoja wa Mataifa, tafadhali wasiliana na:
Nguse Nyerere/ Sekela (sekela.mwambegele@nje.go.tz)
Wizara ya mambo ya nchi za nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki -MOFAIC - 0715371853
hoyce.temu@one.un.org Mtaalamu wa mawasiliano wa Umoja wa Mataifa -0682262627


Tuesday, October 18, 2016

Mchakato wa kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Kaimu Mkurugenzi, Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule (kulia) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkuu, wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Robi Bwiru
Kaimu Mkurugenzi, Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw.  Bernard Haule akiongea na waandishi
=========================================================================

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
 


Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 


                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM, 
                                    Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mchakato wa kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu wanahabari:
Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii ya hapa nchini na nje ya nchi iliandika taarifa kuhusu Tanzania kujitoa au kugomea utaratibu wa visa ya pamoja ya utalii (Single Tourist Visa) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kufuatia taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa ikipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kutaka kufahamu ukweli wa jambo hilo. Hivyo, Wizara imeona leo itoe taarifa rasmi kufafanua namna ya mchakato wa uanzishwaji wa viza ya pamoja ya utalii ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unavyoendelea.

Suala la Uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bado liko katika majadiliano ya Nchi Wanachama kupitia Vikao vya Sekta ya Utalii na Wanyamapori. Katika kufanikisha azma hii,  Baraza la Kisekta la Mawaziri wa  Maliasili na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika  tarehe 1 Novemba 2008 liliunda Kikosi Kazi kwa ajili ya kufanya  utafiti kwa lengo la kubainisha mahitaji na utayari wa Nchi wanachama juu ya kuanzisha  Viza ya Pamoja ya Utalii.  Utafiti uliofanyika mwaka 2010, ulibainisha masuala muhimu yafuatayo ya kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Viza ya Pamoja ya Utalii:

a)    Kurazinisha  (harmonization) sheria za Viza za Nchi Wanachama;
b)     Idara ya Uhamiaji  kuanzisha Mfumo  wa  kudhibiti Usalama;
c)     Utoaji wa Viza kuwa wa kielektroniki;
d)   Kuwepo kwa mfumo wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato pamoja na namna ya kulipa;
e)     Kuwepo kwa maafisa uhamiaji katika kila ofisi za ubalozi;
f)      Kujenga uwezo wa watumishi kwenye suala la  mfumo wa kieletroniki  wa utoaji wa viza ya pamoja ya Utalii.

Kufuatia matokeo ya utafiti huo, Mkutano wa 5 wa Baraza  la Kisekta la Mawaziri wa Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori  uliofanyika  mwezi Julai 2013  jijini Bujumbura, Burundi pamoja na mambo mengine uliagiza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kitajumuisha wataalamu kutoka Taasisi za Uhamiaji, Utalii, Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tehama, Usalama, na Sheria katika nchi wanachama ili  kuandaa mpango kazi  na  kushughulikia masuala yote ambayo  yatajitokeza kuhusiana  na uanzishwaji wa  Viza ya Pamoja ya Utalii. Hata hivyo, kabla ya utekelezaji wa maagizo hayo, Nchi za Uganda, Kenya na Rwanda zilianzisha  Viza ya Pamoja ya Utalii baina yao nje ya vikao vya Jumuiya.

Ni vema ikaeleweka kwa umma wa Watanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla kuwa kwa kuzingatia Mfumo wa Maamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao ni wa kukubaliana kwa pamoja (consensus) hakuna Mfumo wowote wa uanzishwaji wa Visa ya Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioanzishwa. Hii inamaanisha kuwa hakuna Visa ya Pamoja ya Utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokubalika. Kwa mantiki hiyo, taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hazina ukweli wowote na zilikuwa na lengo la kuichafua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawawahakikishia umma wa Tanzania kuwa itaendelea kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya Jumuiya na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha visa ya pamoja ya utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 18 Oktoba  2016.