Wednesday, January 31, 2018

Ban Ki-moon ashiriki kwenye ufunguzi wa Ubalozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea

Picha ya pamoja baada ya Mawaziri wa Tanzania na Korea Kusini kukata utepe na kuzindua rasmi majengo ya Ubalozi wa Tanzania tarehe 31 Januari, 2018. Kutoka kushoto ni Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika; Mhe. Silvester Bile, Kiongozi wa Mabalozi wa Afrika na Balozi wa Ivory Coast; Mhe. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mstaafu; Mhe. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania; Mhe. Lim Sung-nam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Korea Kusini; Mhe. Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini; na Mhe. Salim Alharthy, Kiongozi wa Mabalozi na Balozi wa Falme ya Oman nchini Korea ya Kusini.  

Mheshimiwa Matilda Masuka (kushoto) Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Korea akiwakaribisha na kuwashukuru wageni waalikwa waliohudhuria kwa wingi kwenye ufunguzi rasmi wa Ofisi za Ubalozi tarehe 31 Januari 2018. Awali Tanzania ilikuwa inawakilishwa nchini humo kutokea Japan. Mheshimiwa Balozi Matilda Masuka aliteuliwa Desemba 3, 2016 na baadaye kuapishwa kuwa Balozi wa kwanza mwenye makazi yake Mji Mkuu wa Seoul, Jamhuri ya Korea. Anayeangalia (kulia) ni mfanyakazi wa Ubalozini Debora Mikwenda.  

Mheshimiwa Lim Sung-nam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea akizungumza kwa niaba ya Serikali yake wakati wa ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo. Kwenye salamu zake za ufunguzi, Mheshimiwa Sung-nam amesifu jitihada za Serikali ya Tanzania kukuza uchumi na kusifu ushawishi na karisma ya Balozi Masuka ambayo imewezesha kuvutia Mabalozi na wanadiplomasia wengi Jijini Seoul kushuhudia ufunguzi wa ofisi za Ubalozi. 

Mheshimiwa Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mstaafu akihutubia wageni waliofika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania. Mheshimiwa Ki-moon, ambaye alitambulishwa kama rafiki mkuu wa Tanzania nchini humo, alipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanikiwa kusimika bendera ya Tanzania nchini mwake baada ya miaka 25 ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi. 


Viongozi wakikata utepe


Kibao cha uzinduzi kikifunguliwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Jamhuri ya Korea kwa pamoja. 

Juu ni picha ya pamoja ya Mabalozi wanawake wenye makazi yao Seoul na chini ni Mabalozi wa nchi za Kiafrika wenye makazi yao Seoul. 


Jumuiya ya Wanafunzi wa Kitanzania (diaspora) walioshiriki kikamilifu katika uzinduzi wa ofisi hizo, walitumbuiza kwa kuimba nyimbo mbalimbali za Kitanzania na kucheza muziki wa dansi wa Kitanzania. 



Kongamano la Biashara la Tanzania na Jamhuri ya Korea katika Picha

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Bw. Jundong Kim, Makamu Mwenyekiti wa "Korea Chambers of Commerce and Industry" muda mfupi kabla ya uzinduzi wa Kongamano la kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini tarehe 31 Januari 2018.  

Bw. Kim akimuelezea Mheshimiwa Waziri Mahiga na ujumbe wake kwa kifupi kuhusu kazi za KCCI kabla ya kufungua Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini. 

Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea akiwakaribisha wajumbe waliofuatana na Mheshimiwa Waziri kwenye ziara hiyo kuingia kwenye ukumbi wa Kongamano.

Watanzania wanaoishi nchini Korea wakiwa kwenye mashati maalum ya kutangaza Kongamano ambao pia walikua wakitoa huduma mbalimbali wakati Kongamano likiendelea.









Pichani juu na chini Mheshimiwa Waziri Mahiga akiagana na Watanzania walioshiriki kwenye Kongamano hilo baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya majadiliano.



Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Korea Kusini


Mheshimiwa Augustine Phillip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akilakiwa na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, mara baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mazungumzo ya kikazi tarehe 31 Januari 2018. 


Mheshimiwa Augustine Mahiga na mwenyeji wake Mheshimiwa Kang Kyung-hwa wakiwa kwenye mazungumzo ya kikazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea tarehe 31 Januari 2018. Wakwanza kushoto ni Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Korea. Wakwanza kulia ni Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea





Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania akimkabidhi zawadi ya picha ya mlima Kilimanjaro na kinyago cha mnyama waziri mwenzake wa Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Kang Kyung-hwa baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uchumi baina ya nchi hizo mbili. 


Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha mazungumzo ya kikazi. Wakwanza kulia ni Mheshimiwa Balozi Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bi. Bertha Makilagi, afisa dawati wa Korea Kusini, Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Park Young min, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Wizara ya Mambo  ya Nje ya Korea Kusini na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Tuesday, January 30, 2018

WAZIRI MAHIGA AANZA ZIARA YA SIKU 3 NCHINI KOREA KUSINI

Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akipokelewa na maua na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Jamhuri ya Korea Kusini. Kushoto ni Ndugu Masuka, mume wa Balozi Masuka. 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI MAHIGA KOREA KUSINI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

                                                                                                                                                                                                                                                                                
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Jamhuri ya Korea Kusini yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Korea ya Kusini.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon Mjini Seoul, Mheshimiwa Waziri Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya GS E&C Bw. Min Jeong na timu yake inayoshugulikia uwekezaji na biashara nchini Tanzania.

Waziri Mahiga aliyeongozana na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) na Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji  cha Tanzania alielezea utayari wa Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama ule wa ujenzi wa reli ya kisasa ya viwango vya kimataifa wa “Standard Gauge Railway” inayohusisha makampuni makubwa ya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Jeong alielezea kuwa Kampuni ya GS E&C iliyojikita kwenye ujenzi wa miundombinu ya viwango vya kimataifa, ufuaji na usambazaji wa umeme, usafishaji wa mafuta n.k., sasa imejipanga pia kushiriki katika Ujenzi wa SGR (kupitia ushirikiano na kampuni ya Uturuki (awamu ya 3-5), na Ujenzi wa Daraja la Selanda.

Mbali na mpango huo, kwa sasa Kampuni hiyo yenye makao yake makuu kwenye mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul, imeshiriki katika Mradi ya Umeme nchini Tanzania wa Dar-Arusha “Transmition Line”.

Waziri Mahiga alisisitiza nia ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kusimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Viwango na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Vilevile alitumia fursa hiyo kumuelezea Mkurugenzi Jeong na timu yake kuhusu mpango wa uendelezaji wa ujenzi wa reli hiyo ya viwango kutoka Isaka hadi Kigali, mpango ambao ulitangazwa na Waheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli na Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Tanzania na Rwanda hivi karibuni.

Mheshimiwa Mahiga alimhakikishia mkurugenzi huyo na kundi la makampuni anayoyaongoza, ushirikiano wake na kumkaribisha kuwekeza zaidi nchini Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya umeme na miundombinu mingine.

Kampuni ya GS E&C ni miongoni mwa makampuni kumi “Top Ten” yanayofanya vizuri zaidi nchini Korea Kusini inayokusanya faida ya kiasi cha $10 bilioni kwa mwaka.

Mheshimiwa Waziri Mahiga ambaye yupo nchini hapa kuanzia leo tarehe 30 Januari hadi tarehe 2 Februari, 2018, kufuatia mwaliko wa Mhe. Dkt. Kang Kyung-wha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea anatarajiwa pia kuzindua Kongamano la kwanza la wafanyabiashara, kufungua majengo ya Ubalozi wa Tanzania na kufanya mazungumzo maalum na mwenyeji wake Waziri Kang Kyung-wha.

Mheshimiwa Mahiga atatumia sehemu kubwa ya ziara hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na makampuni makubwa yalikwisha onesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania. Mwishoni mwa ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Mahiga anategemewa kutembelea Chuo cha Taifa cha Diploamasia cha Korea Kusini, kabla ya kurejea nchini Tanzania.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul, Korea Kusini,

30 Januari 2018.


Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na wawakilishi wa kampuni ya GS E&C waliofika hotelini kwake na kufanya naye mazungumzo ya kikazi kwenye Mji Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Seoul. Pichani wawili ni Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni hayo Bw. Min Jeoung. 





Ujumbe wa Mheshimiwa Mahiga ukiongozwa na Mheshimiwa Matilda Masuka, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC na Bw. Edwin Rutageruka, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE wakiwa kwenye mazungumzo na wawakilishi wa makampuni ya GS E&C.

Picha ya Pamoja

Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Singapore

Kaimu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi akizungumza na Balozi wa Singapore nchini mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Tan Puay Hiang alipomtembelea leo katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao yalijikita katika kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuweza kuinua uchumi wa mataifa hayo.
Mazungumzo yakiendelea.

Mhe. Tan Puay Hiang akimkabidhi Balozi Mwinyi zawadi ya kitabu.

Picha ya pamoja Kaimu Katibu Mkuu, Mhe. Balozi Tan Puay Hiang, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Luhangisa (kulia) na Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wa Singapore, Bw. Lucien Hong(kushoto) 

Naibu Waziri akutana na Balozi wa Singapore nchini

 Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Suzan Kolimba akizungumza na Balozi wa Singapore nchini Mhe. Balozi Tan Puay Hiang, alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam, tarehe 29/11/2018. 
Katika mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Kolimba alishukuru Serikali ya Singapore kwa misaada wanayoitoa kwa Tanzania hasa katika eneo la elimu, Mhe. Dkt Suzan alitumia nafasi hiyo kumwalika Balozi huyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyo nchini ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Watalii kutoka nchi hiyo kutembelea Tanzania. 
Kwa upande wake Mhe. Puay Hiang aliikaribisha Tanzania kujifunza Singapore hasa katika eneo la Utalii na alimhakikishia Mhe. Waziri kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali.

Mhe. Dkt Suzan Kolimba na Mhe. Balozi Puay Hiang wakiendelea na mazungumzo, wanaofuatilia ni Bw. Emmanuel Luangisa; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia (Kushoto), Bw. Charles Faini Msaidizi wa Naibu Waziri ( Mwisho kushoto) na Bw. Lucien Hong Mkurugenzi msaidizi kutoka ubalozi wa Singapore ( kulia).    
                                     
Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo.

Monday, January 29, 2018

Mhe. Naibu Waziri amuaga Balozi wa Zimbabwe.

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Suzan Kolimba akimkabidhi zawadi Balozi wa Zimbabwe nchini anayemaliza muda wake Mhe. Balozi Edzai Chimonyo katika hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika Serena Hotel tarehe 29/01/2018. 

Katika hafla hiyo Mhe. Dkt Suzan alimshukuru kwa ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote alichokuwa Balozi hapa nchini na kumtakia heri katika majukumu yake mapya. Mhe. Balozi  alimshukuru Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Ushirikiano mkubwa alioupata wakati akitekeleza majukumu yake hapa nchini.

Waheshimiwa Mabalozi, Mhe. Brahim Buseif Balozi wa Sahara Magharibi nchini (wa kwanza kushoto) na Mhe. Benson Keith Chali Balozi wa Zambia Nchini wakifuatilia hafla hiyo

Mhe. Naibu Waziri Dkt Suzan Kolimba akiteta jambo na Mhe. Balozi Edzai Chimonyo katika hafla hiyo.


 Baadhi ya Maafisa kutoka Wizarani Bi. Elizabeth Mutunga na Bi. Robi Bwiru wakifuatilia hafla hiyo.

 Bw.Ayoub Mdeme Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika (Kulia) na Bw. Martin Tavenyika kutoka Ubalozi wa Zimbabwe nchini (kushoto) wakiwa katika hafla hiyo.

Bw. Suleiman Saleh Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika akiteta jambo na Mhe. Thamsanga Dennis Msekelu Balozi wa Afrika Kusini nchini, anayefuatilia ni Mhe. Balozi Edzai Chimonyo.

Maafisa kutoka Wizarani Bw. Charles Faini na Bi. Mercy Kitonga nao wakiwa katika hafla hiyo.