Thursday, November 30, 2023

NIGERIA YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Nigeria imeoneshwa kuridhishwa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa alipokuwa akimuga Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi Ndogo za Wizara baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini.

Balozi Takamawa ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha Sera ya Mambo ya Nje pamoja na kuanzisha Tume ya kuboresha Haki Jinai nchini.

“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli imefanya mambo ambayo nadhani mataifa mengine tunapaswa kuiga hususan masuala ya kuboresha haki jinai, hili ni jambo kubwa na jema ambalo taifa lolote lile linapaswa kuiga mfano huo hapa Tanzania,” alisema Balozi Takamawa

Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje, Balozi Takamawa amesema kuwa kuboreshwa kwa sera hiyo kunatoa mwanga wa kuimarisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kuongeza wigo wa biashara za kimataifa, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi. 

Pamoja na mambo mengine, Balozi Takamawa ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano iliompatia wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.

Kwa Upande wake, Balozi Mbarouk amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Nigeria ni matunda yalijengwa kwa misingi imara ya viongozi wa mataifa haya mawili (Hayati Mwl. Julius Nyerere na hayati Dkt. Nnamdi Azikiwe) ambao umedumu kwa takriban miaka 60.

Kadhalika, Balozi Mbarouk alimpongeza Balozi Takamawa kwa kuimarisha misingi ya ushirikiano wa Nigeria na Tanzania wakati wa uwakilishi wake hapa nchini ambapo katika kipindi chake uhusiano uliimarika katika sekta mbalimbali hususan elimu, bishara na uwekezaji.

“Tanzania na Nigeria zimekuwa na ushirikiano mzuri kibiashara na wewe ni shahidi wa hilo, ambapo benki ya ‘United Bank of Afrika’ kutoka Nigeria imewekeza nchini, kadhalika Kiwanda cha kuzalisha Cement cha Dangote pia kimewekeza Tanzania na kutoa ajira…..huu ni Ushahidi tosha kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Nigeria ni Imara,” amesema Balozi Mbarouk.

“Naamini kuwa ukiwa nchini Nigeria utakuwa balozi mwema wa Tanzania, nakutakia kila la kheri katika utumishi wako,” amesema Balozi Mbarouk

“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia. 

Tanzania na Nigeria zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akisalimiana na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa alipokuwa akimuga 
katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa 
katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa yakiendelea katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini



BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA BENKI YA UWEKEZAJI YA ULAYA (EIB)


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) ulioongozwa na Bw. Christian Elias Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika, katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma, tarehe 30 Novemba 2023.

Kupitia mazungumzo hayo ambayo ameyafanya kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) wamejadili kuhusu ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia Benki hiyo.

Aidha, wamejadili yatokanayo na Mkutano wa Pamoja wa Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki –OACPS na Umoja wa Ulaya – EU, uliofanyika tarehe 14 – 15 Novemba 2023 nchini Samoa, na baadae kufuatiwa na hafla ya kusaini Mkataba wa Ubia baina ya Nchi za OACPS na EU.


Vilevile, wamejadili juu ya utayari wa Tanzania kushirikiana na Umoja wa Ulaya ili kunufaika na Euro milioni 150 zilizotengwa kwa ajili ya Bara la Afrika kupitia mpango wake wa Global Gateway.

Pia, Balozi Shelukindo aliwasilisha shukrani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wawakilishi wa EIB kwa kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika uwekezaji wa miradi ya umma, ikiwemo: Awamu ya pili ya mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Ziwa Victoria mkoani Mwanza; Mradi wa huduma za usafirishaji wa mabasi yaendayo haraka; Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira mkoani Tanga; ujenzi wa bandari mpya ya Mangapwani, Zanzibar na mradi wa umeme mkoani Kigoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya yaliyofanyika Wizarani jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendelea 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimsikiliza Bw. Christian Elias Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) kwenye mazungumzo yaliyofanyika Wizarani jijini Dodoma 
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America Balozi Swaiba Mndeme wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifafanua jambo wakati wa mazungumzo kati ya Wizara na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya yaliyofanyika Wazarani jijini Dodoma

SERIKALI YAKITAKA KITUO CHA UHUSIANO WA KIMATAIFA CHA DKT. SALIM KUTOA ELIMU BORA YA DIPLOMASIA, STRATEJIA

Serikali imekitaka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuhahikisha kinaendelea kutoa elimu bora ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia na Stadi za Stratejia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) ametoa agizo hilo katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kuwatunuku vyeti wahitimu 1,008.

Wahitimu hao wamwtunukiwa vyeti katika maeneo ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Diplomasia ya Uchumi, Usimamizi wa Amani na Migogoro na Utawala wa Kimkakati.

“Wizara inapenda kusisitiza umuhimu wa Kituo kuendelea kuelimisha Taifa kupitia mijadala na makongamano kwa lengo la kupanua uelewa wa masuala mbalimbali. Kituo kinapaswa pia kuendelea kusimamia na kutekeleza Majukumu ya Msingi ya kuanzishwa kwake ambayo yanajumuisha Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi,” alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa ni vyema Kituo kikaboresha progamu zake ili kukidhi mahitaji ya Wizara, Nchi na watanzania kwa ujumla wake, ambapo alishauri kuwa Kituo kiendelee kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi wetu. 

“Naelekeza usimamie utekelezaji wa mabadiliko yanayoendelea kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutathmini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zilizo chini yake,” Aliongeza Balozi Mbarouk.

Kadhalika Balozi Mbarouk aliwasihi wahitimu kutambua kuwa soko la ajira serikalini na sekta binafsi kwa sasa ni ngumu, hivyo watumie ujuzi na elimu waliyoipata kujiajiri.

“Maarifa mliyoyapata ni mtaji mzuri kwenu unaowapa mwanga wa kutumia fursa za ndani na nje ya nchi katika kufanya biashara na kutoa huduma mbalimbali kwa mujibu wa kile mlichosomea,” alisema Balozi Mbarouk.

Kwa Upande wake Dkt. Reweta Wande ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Balozi Ramadhani M. Mwinyi, amesema Kituo kinaendelea kutoa elimu Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia ya uchumi pamoja na Stadi za Stratejia ambapo jitihada hizo zimetoa matunda ya ongezeko la wahitimu 1,008 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na wahitimu 990 kwa mwaka 2022.

“Lengo la kuanzishwa kwa Kituo ni kutoa elimu ya masuala ya Diplomasia kati ya Tanzania na Msumbiji. Ila kwa sasa Jukumu la Kituo ni kukuza maendeleo, ufahamu na uelewa wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa katika ngazi za kikanda na kimataifa kwa wataalamu wanaoendelea na wanaochipukia na umma kwa ujumla,” alisema Dkt. Wande

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Wande ameahidi kuwa Kituo kitaendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia ya Uchumi na Stratejia kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kusaidia kukuza ujuzi wa wananchi kwa ujumla.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiwasilisha hotuba yake katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akiwasilisha hotuba yake katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akimkabidhi cheti mmoja kati ya wahitimu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim wakati wa Mahafali ya 26 ya Kituo hicho Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali katika mahafali ya 26 ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim Jijini Dar es Salaam


Sehemu ya wahitimu


TANZANIA NA VENEZUELA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi za Wizara jijini Dodoma

Serikali ya Tanzania na Venezuela zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizo ili kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote.

Ahadi hiyo imetolewa katika mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za nishati hususan mafuta na gesi, kukuza teknolojia na maendeleo ya miji, elimu na utamaduni.

Pia, kupitia mazungumzo hayo Balozi Shelukindo amewakaribisha wawekezaji kutoka Venezuela kuja kuwekeza katika sekta za utalii, viwanda, madini, afya na kilimo.

Vilevile, kupitia mazungumzo hayo wamependekeza kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Venezuela, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaokubaliwa kati ya pande mbili.
Mazungumzo yakiendelea
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akimsikiliza Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Venezuela nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya, Mhe. Jesus Manzanilla Puppo yaliyofanyika jijini Dodoma

Monday, November 27, 2023

WAZIRI MAKAMBA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO ZA BALOZI MTEULE WA LIBYA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makamba amemkaribisha nchini Mhe. Alshatewi na kumuahidi ushirikiano wa Wizara na Serikali kwa ujumla wakati wote atakaokuwa akitekeleza majukumu yake nchini.

Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Libya umedumu kwa zaidi ya miaka 50 na na wakati wote umekuwa imara. “Tunaamini kuwa Mhe. Balozi wakati wa uwakilishi wako uhusiano baina ya mataifa yetu utaendelea kuimarika zaidi katika sekta mbalimbali za kimkakati,” aliongeza Waziri Makamba.

Kwa upande wake Balozi Mteule, wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano na Tanzania wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi hapa nchini.

Ni faraja kwangu kuja kufanya kazi Tanzania naahidi wakati wote wa uwakilishi wangu hapa Tanzania kama Balozi tutafanya kazi kwa ushirikiano katika kuendeleza sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, kilimo na nyingine.

Katika tukio jingine, Waziri Makamba amekutana kwa Mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot, Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino pamoja na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Robert Raines.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Makamba amejadiliana na Mabalozi hao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa uwili, kikanda na ushirikiano wa kimataifa baina ya Tanzania na nchi zao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Libya nchini, Mhe. Abulmajed Albhloul Alshatewi pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Maafisa kutoka Ubalozi wa Libya baada ya Balozi Mteule kuwasilisha nakala za hati za utambulisho 

Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiteta jambo na Balozi wa Vatican nchini, Mhe. Askofu Mkuu Angelo Accattino katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Bw. Robert Raines katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam



Sunday, November 26, 2023

WAZIRI MAKAMBA APOKEA TAARIFA MAALUM YA KUTATHMINI HALI YA UTUMISHI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akipokea taarifa Maalum ya kutathmini hali ya utumishi, majengo na uwakilishi katika Balozi zote za Tanzania kutoka kwa Kamati Maalum iliyoongozwa na Balozi Saidi Othman Yakubu katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.






Friday, November 24, 2023

SHIRIKISHO LA JAMHURI YA SOMALIA LAKUBALIWA KUJIUNGA NA JUMUIYA YA EAC



Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeridhia ombi la Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kujiunga na Jumuiya hiyo katika Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Arusha.

Mkutano uliopitisha ombi hilo umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evereste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Silver Kiir, Waziri Mkuu wa Rwanda aliyemwakilisha Rais Paul Kagame na Makamu Rais wa DRC aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Antonie Tshisekedi.

Mkutano huo pia ulihudhuria na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mahmoud ambaye alialikwa kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huu pia ulipokea na kuridhia kwa kauli moja mapendekezo ya Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi na Usalama wa Chakula yaliyofanyika jijini Arusha tarehe 23 Novemba na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Mawaziri wa Kisekta.

Kuridhiwa kwa mapendekezo hayo kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP28) utakaofanyika nchini UAE kuanzia tarehe 28 Novemba 2023 na msimamo mmoja wa nchi wanachama.

Mkutano huo ulijadili na kukubaliana juu ya masuala mbalimbali ya Mtangamano wa Afrika Mashariki ambapo wameazimia kuendelea kuulinda na kuukuza mtangamano huo kwa lengo la kuwaenzi waasisi wake na kuinua kipato cha watu na kutoa rai za kutokuruhusu tofauti ndogondogo kuleta mtafaruku ndani ya Jumuiya

Viongozi hao wameitakia heri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika nchini humo.

Katika Mkutano huo Wanafunzi sita kutoka nchi wanachama walishinda tuizo ya uanjdishi wa Insha na kupatiwa vyeti na zawadi ya fedha taslimu. Wanafunzi walioshinda tuzo hizo ni Lalom Joselin kutoka Sudani Kusini aliyepata Dola 550 za Marekani, Ilimfuwe Aija kutoka Burundi alipata dola 600 za Marekani, Amoron Evelyn kutoka Uganda alipata Dola 770 za Marekani, Irasore sania kutoka Rwanda alipata Dola 1000, Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania alipata Dola 1200 za Marekani na Austin Alego Angoya 1kutoka Kenya alipata Dola 1500 za Marekani.

Wanafunzi hao washindi wa Tuzo hizo pia wamepata zawadi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro kuanzia tarehe 25 -27 Novemba 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye ambaye amemaliza muda wake wa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya hiyo Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit wakati wa Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha.
Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Afrika Mashariki unapigwa kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokuwa ukiendelea katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Ruto akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akizungumza kwenye Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha. Somalia imekuwa Mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya ombi lake la kujiunga na Jumuiya hiyo kuridhiwa kwenye mkutano.
Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha
Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni akihutuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha

Idirisa Musa Hamadi kutoka Tanzania akipokea zawadi ya uandishi wa Insha

NAIBU WAZIRI BYABATO AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAMHURI YA KOREA

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju, pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea kwa manufaa ya pande zote mbili.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri Mhe. Byabato alimuelezea Bi. Youngju kuridhishwa kwa Tanzania juu ya ushirikiano na uhusiano uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea na kuahidi kuendelea kushirikiana na nchi hiyo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Naye Bi. Youngju alimuelezea Naibu Waziri Byabato juu ya mpango wa Jamhuri ya Korea wa kuandaa Mkutanoo kati ya Nchi yake na Viongozi wa Bara la Afrika uliopangwa kufanyika mapema mwezi Juni 2024 na kwamba anaialika rasmi Tanzania ishiriki katika mkutano huo.
 Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju walipokutana kwa mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha.
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Bi. Oh Youngju yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Mazungumzo yakiendelea

KISWAHILI NYENZO MUHIMU KATIKA KUKUZA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MALAWI

Serikali ya Tanzania itaendelea kukuza na kuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili ili kuimarisha biashara inayovuka mipaka hususan katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Malawi.



Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola alipokitembelea Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha nchini humo kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.



Katika mazungumzo yake na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo hicho, Dkt. Kizito Elijah, Mhe. Balozi Kayola alisema kuwa, upo mwingiliano mkubwa wa kibiashara baina ya Tanzania na Malawi unaosababisha mahitaji makubwa ya kujifunza lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano katika biashara.



Aliongeza kusema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia na kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini humo mwezi Julai 2023 ikiwemo masuala ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Malawi.



Kwa upande wake, Dkt. Elijah alisema kuwa, Chuo hicho kimepanga kuanzisha Kituo cha Lugha na kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania hususan Taasisi za Elimu na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili kutekeleza azma ya kufundisha Lugha ya Kiswahili chuoni hapo na kwamba chuo hicho kipo tayari kuanzisha ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania ikiwa ni pamoja na kubadilishana wakufunzi na wanafunzi.



Wakati huohuo, Mhe. Balozi Kayola ameitembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 katika viwanda vya uzalishaji Unga wa ngano, sabuni za kufulia na inatarajia kukamilisha kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia mwezi Mei 2024.



Akiwa katika Kampuni hiyo Mhe. Balozi Kayola amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika na kuwahamasisha kuendelea kukuza wigo wa uwekezaji wa bidhaa mbalimbali nchini humo kwani mahitaji bado ni makubwa.



Kadhalika, Mhe. Balozi Kayola alipata fursa ya kukutana na Jumuiya ya Watanzania waishio katika Mkoa Kusini, Malawi ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo.



Katika mazungumzo yake na Jumuiya hiyo aliwaasa kuendelea kuwa wawakilishi wazuri wa nchi yao kwa kufuata sheria za nchi waliyopo  ili kulinda taswira nzuri ya Tanzania.



Pia alisisitiza umuhimu wa wao kuendelea kujiandikisha kwenye Mfumo wa Kidigitali wa kuwatambua Diaspora (Diapora Digital Hub) ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa mbalimbali za biashara, masoko, na uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kurahisisha utoaji wa msaada wakati wa dharura zinazoweza kuwapata katika nchi wanazoishi.



Mhe. Balozi Kayola alitumia fursa hiyo pia kuwajulisha kuhusu hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa  na Mhe. Rais Dkt. Samia huku akitaja Miradi mikubwa inayokamilishwa ikiwemo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR na miradi mingine kwenye sekta ya Kilimo, Biashara na Uwekezaji.



Vilevile, Mhe. Balozi Kayola aliwaeleza Diapora hao kuwa, Ubalozi upo tayari kushirikiana nao na kuwasisitiza kuwa huru katika kuwasilisha maoni, mapendekezo na ushauri kwa manufaa mapana ya Tanzania. 

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza  na Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi,  Dkt. Kizito Elijah alipokitembelea Chuo hicho kwa lengo la kujadiliana na Uongozi wa Chuo hicho kuhusu namna bora ya kuanzisha ushirikiano baina na taasisi za elimu za Tanzania hususani katika kufundisha Lugha ya Kiswahili.
Mkuu wa Kitivo cha Elimu, Mawasiliano na masuala ya Habari wa Chuo Kikuu cha Biashara na Sayansi cha Malawi,  Dkt. Kizito Elijah wakati wa mkutano kati yake na Balozi Kayola (hayupo pichani)
Mhe. Balozi Kayola akiagana na Dkt. Elijah mara baada ya kukamilisha mazungumzo baina yao 

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akipata maelezo alipotembelea Kampuni ya Kitanzania ya Bakhresa iliyowekeza nchini Malawi tangu mwaka 2003 kwenye viwanda vya kutengeneza unga wa ngano na sabuni za kufulia.
Mhe. Balozi Kayola akiendelea kupata maelezo wakati wa ziara yake kwenye moja ya kiwanda cha Kamapuni ya Kitanzania ya Bakhresa ambayo imewekeza nchini Malawi

Mhe. Balozi Kayola akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kampuni ya Bakhresa Malawi Limited akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Mahesh Josyabhatla (wa pili kulia)
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini mwa Malawi alipowatembelea kwa ajili ya kujitambulisha ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kuiwakilisha Tanzania nchini humo
Sehemu ya Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini, Malawi wakifuatilia mkutano kati yao na Mhe. Balozi Kayola (hayupo pichani)

Mwenyekiti wa Watanzania wanaoishi Mkoa wa Kusini Malawi, Bw. Suleiman Marijani akizungumza wakati wa Mkutanoo kati ya Jumuiya hiyo na Balozi Kayola