Ujumbe wa Tanzania ukiendelea na Mkutano wa Ngazi ya
Wataalam wa Jumuiya ya Afrika Mashriki kuandaa Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la
Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 22 Novemba 2023 |
Wajumbe wa Mkutano wa Ngazi ya
Wataalam wa Jumuiya ya Afrika Mashriki wakiendelea na mkutano huo kuandaa Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la
Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 22 Novemba 2023 |
Mkutano wa Ngazi ya Wataalam kutoka katika Jumuiya ya Afrika Mashriki unaendelea jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo.
Mkutano huo ulianza tarehe 18 Novemba, 2023 unatarajiwa kukamilisha nyaraka kwa ajili ya Kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 21 Novemba 2023 na kufuatiwa na mkutano wa Baraza hilo tarehe 22 Novemba 2023.
Mkutano huo wa ngazi ya wataalam unapitia na kujadili masuala mbalimbali kuhusu Mtangamano wa Afrika Mashariki ambayo yatawasilishwa katika Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu kwa majadiliano kabla ya kuwasilishwa kwenye Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri kwa mapendekezo.
Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ni chombo kinachotoa miongozo ya kisera kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa uanzishwaji wake.
Mkutano wa 43 wa Baraza ulielekeza nchi wanachama, Taasisi, na Mashirika kutekeleza maamuzi yote na maelekezo yaliyosalia na kutoa taarifa ya utekelezaji wake kwenye Mkutano 44 wa Baraza hilo.
Katika kutekeleza maelekezo hayo Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikisha na Nchi wanachama, Taasisi, na Mashirika ilifanya uchambuzi wa maamuzi na maelekezo yote ambayo hayajatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano na kuwasilisha taarifa hiyo kwa Baraza kwa miongozo na maelekezo.
Mkutano huo unahudhuriwa na Wajumbe kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni mwenyeji Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Kenya, Uganda, Rwanda, na Sudan Kusini.
Baada ya kukamilika kwa Mkutano huo wa Kawaida wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 24 Novemba, 2023 utafanyika Mkutano wa kawaida wa 23 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya.
Mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Usalama wa Chakula na Uendelevu wa Mazingira utakaofanyika tarehe 23 Novemba, 2023
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.