Wednesday, November 22, 2023

TANZANIA YAIHAKIKISHIA UAE MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA, UWEKEZAJI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuhakikishia Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mazingira salama ya biashara na uwekezaji nchini.  

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amebainisha hayo aliposhiriki katika kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam na kuwasihi kuendelea kufanya biashara na kuwekeza kwa wingi nchini.

Balozi Mbarouk alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji yanaboreshwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza nchini.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka sera imara, sheria na taratibu rafiki pamoja na kuweka misingi thabiti ya kustawisha mazingira ya biashara,” alisema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Tanzania na Falme za Kiarabu zina ushirikiano mzuri wa kiuchumi katika eneo la biashara na uwekezaji ambapo UAE ni mshirika wa saba (7) wa kibiashara wa Tanzania kwa kiasi cha biashara baina ya nchi hizo kinachofikia Dola za Marekani bilioni 3.2. Kadhalika, kuhusu uwekezaji, UAE ni miongoni mwa nchi zilizowekeza kwa kiasi kikubwa nchini.

Balozi Mbarouk alipongeza juhudi za viongozi wa mataifa hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa UAE, Mheshimiwa Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, kwa uongozi wao imara wenye maono na juhudi za kuimarisha na kudumisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili 

Kwa Upande wake, Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini, Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa uhusiano baina ya UAE na Tanzania mwaka 1974, nchi hizo zimejitahidi kuendeleza na kuimarisha uhusiano huo katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Katika jitihada ya kuonesha azma ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, mikataba mbalimbali imesainiwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi zetu. Ambapo ushirikiano huu umesababisha ongezeko la kiasi cha kubadilishana biashara kati ya nchi hizi mbili kufikia Dola za Marekani Bilioni 2.2,” alisema Balozi Marzouqi

Aidha, Balozi Marzouqi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiutoa kwa UAE ambapo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uhusiano baina ya mataifa hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza wakati wa hafla ya kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini, Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi akizungumza wakati wa hafla ya kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na viongozi mbalimbali wakishiriki katika hafla ya kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam

Mabalozi pamoja na viongozi mbalimbali wakimsikiliza Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini, Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi katika hafla ya kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam

Sehemu ya Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na viongozi mbalimbali wakishiriki katika hafla ya kumbukizi ya miaka 52 ya Siku ya Taifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaliyofanyika jana jioni Jijini Dar es Salaam



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.