Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB) ulioongozwa na Bw. Christian Elias Mkuu wa Kitengo cha Mashariki na Kusini mwa Afrika, katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma, tarehe 30 Novemba 2023.
Kupitia mazungumzo hayo ambayo ameyafanya kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) wamejadili kuhusu ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia Benki hiyo.
Aidha, wamejadili yatokanayo na Mkutano wa Pamoja wa Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki –OACPS na Umoja wa Ulaya – EU, uliofanyika tarehe 14 – 15 Novemba 2023 nchini Samoa, na baadae kufuatiwa na hafla ya kusaini Mkataba wa Ubia baina ya Nchi za OACPS na EU.
Vilevile, wamejadili juu ya utayari wa Tanzania kushirikiana na Umoja wa Ulaya ili kunufaika na Euro milioni 150 zilizotengwa kwa ajili ya Bara la Afrika kupitia mpango wake wa Global Gateway.
Pia, Balozi Shelukindo aliwasilisha shukrani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wawakilishi wa EIB kwa kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo katika uwekezaji wa miradi ya umma, ikiwemo: Awamu ya pili ya mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa Ziwa Victoria mkoani Mwanza; Mradi wa huduma za usafirishaji wa mabasi yaendayo haraka; Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira mkoani Tanga; ujenzi wa bandari mpya ya Mangapwani, Zanzibar na mradi wa umeme mkoani Kigoma.
Mazungumzo yakiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.