Wednesday, November 8, 2023

DIPLOMASIA YA UCHUMI NI UTEKELEZAJI WA SERA YA MAMBO YA NJE- BYABATO


Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato (Mb) amesema Diplomasia ya uchumi ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojumuisha mipango na mikakati ili kunufaisha taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa unaofanyika kupitia ushirikiano baina ya Tanzania, mataifa mbalimbali, jumuiya za kikanda na za kimataifa.

Amesema utekelezaji huo unajumuisha utafutaji wa masoko nje ya nchi, kuvutia uwekezaji, biashara, watalii, kutafuta mikopo ya fedha ya masharti nafuu, ufadhili wa masomo nje ya nchi na uhaulishaji wa teknolojia za kisasa ambazo hutumiwa na sekta za uzalishaji zikiwemo viwanda, kilimo na nishati. 

Mhe. Byabato ameongeza kuwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi Tanzania inapata mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia na kuchangia maendeleo ya Taifa na kufafanua kuwa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani inakamilisha taratibu za ujenzi wa kiwanda cha kuchakata madini ya kutengenezea betri za magari ya umeme kinachotarajiwa kukamilika mwaka 2026. 

“Kiwanda hiki kitaleta teknolojia mpya ya utengenezaji wa vifaa vya magari, kuhaulisha teknolojia nchini na kuibua vipaji vipya kwa vijana watakaopata ajira katika Kiwanda hicho,” alisema Mhe. Byabato. 

Amesema diplomasia ya uchumi inasaidia upatikanaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kuongeza kuwa hadi kufikia mwezi Septemba, 2023 Tanzania imeuza tani 13,708 za nyama ikilinganishwa na tani 1,777 zilizouzwa mwaka 2020/21. 

“Masoko hayo yamepatikana katika nchi za China, Kuwait, Oman, Qatar, Vietnam na Umoja wa Falme za Kiarabu, masoko haya yamechochea sekta ya uzalishaji kwa ujumla wake,” alisisitiza Mhe. Byabato.

Mhe. Byabato alikuwa akijibu swali Bungeni lililoulizwa na Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ameir Abdallah Ameir aliyetakla kujua mchango wa diplomasia ya uchumi katika kuleta mapinduzi ya Sayansi na Teknolojia na sekta za uzalishaji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifafanua jambo wakati akijibu swali Bungeni
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akijibu swali Bungeni 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akisikiliza swali Bungeni
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifafanua jambo wakati akijibu swali Bungeni
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato akifafanua jambo wakati akijibu swali Bungeni

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.