Wednesday, November 22, 2023

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA BARAZA LA MAWAZIRI EAC JIJINI ARUSHA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) akiteta na jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angela Kairuki muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 22 Novemba 2023.

Mkutano huo ambao ulianza tarehe 18 Novemba 2023 kwa ngazi ya wataalam na kufuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu umepitia na kujadili mapendekezo yatakayowasilishwa katika Kikao cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha tarehe 24 Novemba 2023.

Mkutano wa 44 wa Baraza la Mawaziri wa EAC pamoja na mambo mengine umejadili masuala kuhusu Utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya mkutano cha Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 hadi 24 Novemba, 2023; utekelezaji wa maazimio na maelekezo ya Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya kuhusu Majadiliano ya Ombi la Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kujiunga na EAC; juhudi za utafutaji wa Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo; Hali ya Kifedha ya Mfuko wa Akiba wa Jumuiya; majadiliano kuhusu Katiba ya Fungamano la kisiasa la Jumuiya; Tathmini ya miswada iliyopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki; na Utoaji wa Tuzo kwa washindi wa mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri ambao ni Wajumbe kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni mwenyeji Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Kenya, Rwanda, Sudan Kusini na Uganda.

Kukamilika kwa Mkutano huo wa Kawaida wa 44 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutafuatiwa na Mkutano wa 23 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya EAC uliopangwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2023 jijini Arusha.

Mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Majadiliano ya Juu kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula na Uendelevu wa Mazingira ambao pia utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya EAC.

Mkutano huo unalenga kupata msimamo wa pamoja wa Jumuiya ya EAC kuelekea katika Mkutano wa Kimataifa wa 28 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) utakaofanyika kuanzia Novemba 28, 2023 nchini UAE.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifuatilia Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha 
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ukiwa umesimama wakati wimbo wa Jumuiya unapigwa kwenye Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehenu ya ujumbe wa Sudan Kusini wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha 
Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Jumuiya unapigwa kwenye Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha 
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha 
Katibu Mkuu wa Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha
Waziri Burundi anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Balozi Gervais Abayeho akifungua Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha
Sehemu ya Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano wa 44 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokuwa ukiendelea jijini Arusha

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.