Tuesday, June 2, 2026

Makatibu Wakuu EAC Wakutana Kukamilisha Maandalizi ya SCTIFI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akichangia hoja kwenye Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) ngazi ya Makatibu Wakuu.

Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaosimamia masuala ya mtangamano wamekutana katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) unaotarajiwa kufanyika tarehe 4 Juni 2026.

Kikao hicho cha Makatibu Wakuu, kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 2 hadi 3 Juni 2026, ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya mkutano wa mawaziri unaotarajiwa kutoa mwelekeo wa kisera na maamuzi yatakayochochea ukuaji wa biashara, maendeleo ya viwanda na ongezeko la uwekezaji katika Jumuiya, sambamba na kuimarisha ushindani wa uchumi wa kanda.

Makatibu Wakuu hao wamepokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa SCTIFI. Miongoni mwa taarifa zilizojadiliwa ni pamoja na; taarifa Kamati ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Ushindani ya Afrika Mashariki na Kamati ya Maendeleo ya Viwanda.

Aidha, kikao hicho kimejadili taarifa ya mapitio ya Kanuni za Uasili wa Bidhaa za Afrika Mashariki (Rules of Origin) iliyowasilishwa na Kikosi Kazi cha Kikanda cha Wataalamu. Mapitio hayo pamoja na masuala mengine yanalenga kulinda soko la bidhaa zinazozalishwa ndani ya EAC kwa kuhakikisha bidhaa zinazostahili kunufaika na upendeleo wa biashara ndani ya Jumuiya. Hatua hiyo pia inalenga kuchochea uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, kuvutia uwekezaji wa viwandani na kuimarisha ushindani wa bidhaa za EAC katika masoko ya kikanda na kimataifa. 

Baraza hili ni moja ya vyombo muhimu vya maamuzi katika Jumuiya chenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa ajenda za mtangamano wa kiuchumi. Baraza hilo husimamia maendeleo ya Soko la Pamoja, Umoja wa Forodha na mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza biashara ya ndani ya Jumuiya, kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kodi (NTB’s), kuimarisha ushindani wa viwanda vya kikanda na kuvutia uwekezaji unaochochea ukuaji wa uchumi na ajira.

SCTIFI imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha biashara ya kikanda kwa kuwezesha urahisishaji wa biashara mipakani, kurasinisha viwango vya bidhaa, kuimarisha mifumo ya forodha na kuendeleza sera zinazolenga kukuza sekta binafsi na ushiriki wa wawekezaji katika maendeleo ya uchumi wa Jumuiya.

Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, ukijumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides R. Mbwasi, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.













Friday, May 29, 2026

Mkutano wa 48 wa SCTIFI Waanza Jijini Arusha



Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga akichangia agenda wakati wa Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)


Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeanza leo, Mei 29, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Mkutano huo umeanza kwa kikao cha ngazi ya Wataalamu kitakachofanyika kuanzia Mei 29 hadi Juni 1, 2026, nakufuatiwa na Makatibu Wakuu kinachotarajiwa kufanyika Juni 2 hadi 3, 2026, kabla ya Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika Juni 4, 2026.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa mbalimbali ikiwemo; utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa SCTIFI, taarifa za Kamati ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Masuala ya Ushindani ya Afrika Mashariki pamoja na Kamati ya Viwanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Forodha katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Flavia Busingye, amewataka wataalamu hao kujikita katika majadiliano yatakayotoa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazoathiri ukuaji wa biashara ndani ya Jumuiya.

Bi. Busingye amesema ni muhimu kwa Nchi Wanachama kuendelea kushirikiana katika kuondoa vikwazo vya kibiashara, ikiwemo changamoto zinazohusiana na masuala ya kodi, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo na maamuzi yaliyotolewa katika vikao mbalimbali vya Jumuiya, hususan maamuzi ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC.

Kupitia mkutano huo wa SCTIFI, Jumuiya inalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kukuza biashara ya mipakani, kuondoa vikwazo vya biashara na kuchochea maendeleo ya viwanda katika Nchi Wanachama.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ngazi ya Wataalamu unaongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga, akiwa ameambata na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu katika Wizara hiyo, Balozi Thobias Makoba, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.











Thursday, February 19, 2026

WAZIRI KOMBO AKUTANA NA BALOZI WA JAMHURI YA ZIMBABWE, HELEN BAWANGE DINGANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa na  Balozi wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Tanzania Mhe. Helen Bawange Dingani (Kushoto).


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alikutana na kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Balozi wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Tanzania Mheshimiwa Helen Bawange Dingani.

Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 18 Februari 2026 katika ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mkutano huo ulijikita katika kuendeleza uhusiano wa pande mbili kwa kuangazia utambuzi wa vipaumbele vya pamoja, kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, na kuchunguza njia za vitendo za ushirikiano.

Lengo kuu lilikuwa ni kujadili namna ya kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano ambao pande zote mbili zinauona, kuwa wa kimkakati katika mazingira ya kikanda yanayobadilika.

Pande zote mbili zilithibitisha tena dhamira yao ya kuendeleza mazungumzo ya pande mbili yaliyo imara na yenye kuleta matokeo chanya.

Ushirikiano huu unaashiria nia endelevu ya kuimarisha mahusiano kupitia diplomasia ya busara, huku ikisisitiza nafasi ya Tanzania kama jukwaa la ushirikiano wa kikanda na kimataifa.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa na  Balozi wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Tanzania Mhe. Helen Bawange Dingani (Kushoto) wakati mazungumzo yakiendelea katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar-es-Salaam.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo


Balozi wa Jamhuri ya Zimbabwe nchini Tanzania Mhe. Helen Bawange Dingani




TANZANIA NA MSUMBIJI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa  na Balozi wa Msumbiji nchini  Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida (Kushoto).


Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msumbiji zimeeleza dhamira ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili katika maeneo ya kimkakati, ikiwemo Sekta ya Afya ili kuleta maendeleo ya wananchi wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida, wameeleza dhamira hiyo walipokutana na kufanya mazungumzo tarehe 18 Februari, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kubainisha maeneo ya ushirikiano zaidi kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kuongeza ushirikiano katika Sekta ya afya, kukuza uchumi, na kujadili maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja unaotarajiwa kufanyika nchini mwaka huu.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Kombo pia amewakaribisha wananchi wa Msumbiji kunufaika na huduma za Afya za kibingwa na kibobezi zinazopatikana nchini ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji.

Naye Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe. Ricardo Mtumbuida, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano wa kindugu unaoendelea kuipatia nchi yake, na kusisitiza azma ya Msumbiji ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania ili kukuza ustawi wa wananchi wa mataifa yote mawili


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo 


Balozi wa Msumbiji nchini Mhe. Ricardo Mtumbuida


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Kulia) akiwa  na Balozi wa Msumbiji nchini  Tanzania Mhe. Ricardo Mtumbuida (Kushoto) wakati mazungumzo yakiendelea kwenye Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar-es-Salaam.