Thursday, January 31, 2019

Kampuni ya Kenya kununua tani laki moja za korosho Tanzania


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dkt. Hussein Mansoor (kushoto) kwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya, Bw. Brian Mutembei (kulia) wakisaini Mkataba wa mauziano ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa malipo ya Shilingii bilioni 418. Wanaoshuhudia tukio hilo muhimu ni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto), Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kakunda (kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Innocent Bashungwa (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Kilimo na Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini. Tukio hilo lilifanyika kwenye Ukumbi wa mikutano uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 30 januari 2019. Mawaziri hao wapo jijini humo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Dkt. Mansoor na Bw. Mutembei wakibadilishana Mkataba huo mara baada ya kusaini
Mhe. Prof. Kabudi akizungumza kabla ya kuanza kwa tukio hilo la kihistoria la kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho ghafi
Mhe. Kakunda nae akizungumza

Mhe. Dkt. Bashungwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)
Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Kazungu akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho kutoka Tanzania
Bw. Mutembei nae akieleza furaha yake katika kukamilisha ununuzi wa korosho kutoka Tanzania
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Buchweshaija akizungumza kwa ufupi kuhusu hafla hiyo ya uwekaji saini mkataba wa ununuzi wa korosho. Wengine katika picha ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Mhe. Prof. Florens Luoga ( kulia walioketi) akifuatiwa na Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mkutano ukiendelea. Kushoto ni Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka
=============================================================================================


Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imesaini mkataba wa mauzo ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa Kampuni ya Kenya ya INDO Power Solutions kwa malipo ya Shilingi bilioni 418.

Mkataba huo umesainiwa jijini Arusha tarehe 30 Januari 2019 kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Dkt. Hussein Mansoor kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Brian Mutembei, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power Solutions ya nchini Kenya.

Tukio hilo la kihistoria lilishuhudiwa na Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Kakunda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga,  Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

Viongozi wengine walioshuhudia ni Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Dan Kazungu, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Joseph Buchweshaija, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Prof. Siza Tumbo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Edwin Rutaberuka, Mkurugenzi wa TanTrade, Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini na Waandishi wa Habari.

Awali wakizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo Mawaziri hao wakiongozwa na Prof. Kabudi, kwa pamoja walipongeza kwa dhati uamuzi wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Serikali kununua korosho kutoka kwa wakulima ili kuepusha wakulima hao kuuza korosho zao kwa bei ya chini kwa watu wasio kuwa na nia njema kwa wakulima. Itakumbukwa kuwa, mwezi Novemba 2018, Mhe. Rais Magufuli alitoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo waratibu zoezi  la ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima kwa shilingi 3,300 kwa kilo moja.

Kwa upande wake Prof. Kabudi alisema kuwa anampongeza  Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi huo wa Serikali kununua korosho yote ili wakulima wapate bei inayolingana na jasho lao ambao hatimaye umezaa matunda kwa faida na maendeleo ya nchi.

Naye Mhe. Kakunda alieleza kuwa Bw. Mutembei ni mnunuzi wa kwanza kati ya wengi ambao walikuwa kwenye mazungumzo na Serikali kuhusu ununuzi wa korosho hizo. Mhe. Kakunda alisema katika majadiliano Serikali iliangalia kufanya biashara ya faida ambayo itawezehsa kulipa gharama mbalimbali ikiwemo gharama za upakiaji na upakuaji, malipo kwenye Serikali za Mtaa na michango mingine ya kijamii kwa mujibu wa makubaliano. Hivyo aliwataka watanzania na wenye viwanda kutokuwa na wasiwasi kwani Serikali ina nia njema ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan kupitia sekta ya kilimo cha korosho.

“Wakulima wa Korosho wanatakiwa kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi wake ambao unalinda maslahi ya mkulima na umewawezesha kuuza korosho zao kwa faida. Nawakaribisha wafanyabiasha makini kuja nchini kwani Serikali ipo tayari kuwasikiliza watu wa aina hiyo na kufanya nao biashara” alisema Mhe. Kakunda.

Kwa upande wake, Mhe. Bashungwa alieleza kuwa katika msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019 tayari zimekusanywa tani 213,159 ambazo kati ya hizo tani 126,194 zimehakikiwa na tayari  wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani wamelipwa fedha zao kwa zaidi ya asilimia 95.5. Mhe. Bashungwa aliongeza kuwa, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Wakulima wote kulipwa fedha zao hadi kufikia tarehe 05 Februari 2019.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Kazungu alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni faraja kubwa kwake katika historia ya mahusiano kati ya Tanzania na Kenya ambayo yanaendelea kuimarika siku hadi siku. Aidha, alieleza kuwa mkataba huo ni mfano mzuri wa kuimarika kwa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan katika masuala ya kilimo na biashara.

Kwa upande wake, mnunuzi wa korosho hizo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Indo Power Solutions, Bw. Mutembei alisema amekuja kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Magufuli za kumwinua mkulima wa Tanzania na kwamba anawataka wale wote wanaobeza jitihada hizo za Mhe. Rais Magufuli kuacha mara moja huku akilaani kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara kuendelea kuwakandamiza wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo wanazopanga wao huku wakijua wazi kuwa wakulima hao wametumia gharama kubwa katika uzalishaji wa mazao hayo.

Pia aliwataka wafanyabiashara kufuata taratibu na sheria katika kufanya biashara kama Serikali zinavyoelekeza na kuacha kuchanganya biashara na siasa.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka, Dkt. Mansoor alieleza kufurahishwa na tukio hilo ambalo limekuja wakati mwafaka wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikijiandaa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika jijini humo hivi karibuni. Aidha alisema kuwa, kwa kiasi kikubwa tukio hilo limeiinua Bodi yake na kwamba anatoa wito kwa wafanyabiasha wengine wa ndani na nje ya Tanzania kuja nchini na kushirikiana na Bodi hiyo ili kuwakomboa wakulima wengi Zaidi.

Mkataba huo umesainiwa wakati baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Tanzania wakiwa jijini Arusha kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika kwenye Kituo cha  Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) tarehe 1 Februari 2019.Wednesday, January 30, 2019

Waziri Mahiga ashiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EACWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza kama kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye  Kikao Maalum cha 38 cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 30 Januari 2019 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 1 Februari 2019. Wengine katika picha ni Kapt. Mstaafu, Mhe. George Mkuchika (kushoto), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maejimenti ya Utumishi wa Umma na Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango. Anayeonekana nyuma ya Mhe. Mkuchika ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.
Mawaziri hao wakipitia nyaraka mbalimbali wakati wa kikao hicho
Mwenyekiti wa Kikao Maalum cha 38 cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Mhe. Kirunda Kivejinja (wa pili kulia), ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza hilo.
Ujumbe wa Burundi ukiwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Mawaziri
Ujumbe wa Kenya nao ukifuatilia kikao
Mjumbe kutoka Sudan Kusini (kushoto) akiwa katika meza moja na ujumbe wa Rwanda wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri


Ujumbe wa Uganda nao ukifuatilia kikao

Wajumbe wa Tanzania wakiongozwa na Mawaziri wakifuatilia kikao. Kulia ni Naibuu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi Amina KH. Shaaban
Dkt, Aloyce Nzuki, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa na Bw. Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt. Aziz Mlima (kushoto) kwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao cha Baraza la Mawaziri 
Wajumbe wengine wa Tanzania
====================================================


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU MKUTANO MAALUM WA 38 WA  BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mkutano Maalum wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubabaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 1 Februari, 2019.

Mkutano huo ambao unaongozwa na Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Uganda ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Kirunda Kivejinja utajadili agenda mbalimbali muhimu ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda zingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa  kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2019.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 28 Januari kikifuatiwa na kikao cha Kamati ya Uratibu chini ya Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 29 Januri 2019.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo  unaongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuwahusisha pia Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa , Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Waziri Fedha na Mipango, Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Joseph Kakunda (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara na Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo.


Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Arusha.
30 Januari 2019
Tanzania yavutia makampuni ya Saudi Arabia kuja kuangalia fursa za uwekezaji

Baadhi ya wafanyabiashara wa Saudi Arabia wakisikiliza mada kuhusu fursa,vivutio, sheria na  kanuni  za  uwekezaji nchini  katika kongamano lililofanyika Jumatano tarehe 30 Januari, 2019, jijini Dar es salaam. Ziara hiyo inatokana na juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki  kupitia Ubalozi wa Saudi Arabia na wadau wengine wa Kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.Afisa Uhamasishaji Uwekezaji (TIC) Bi Diana Mwamanaga akiwasilisha mada katika kongamano hilo.


Baadhi ya wawakilishi wa taasisi za serikali wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.

Afisa Mipango na Uwekezaji wa Shirika la Viwanda Vidogo(SIDO) Bi. Johari Masenge  akiwasilisha mada katika kongamano hilo.

Tuesday, January 29, 2019

Katibu Mkuu aongoza ujumbe wa Tanzania kikao cha Makatibu Wakuu wa EACDkt. Faraji Kasidi Mnyepe (aliyekaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha maandalizi kabla ya kushiriki kikao cha Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Januari 2019. Pamoja na mambo mengine kikao cha Makatibu Wakuu kilipokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa kwao na wajumbe wa ngazi ya Wataalam. Kikao cha Makatibu Wakuu kitafuatiwa na kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachofanyika tarehe 30 Januari 2019 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 1 Februari 2019.
Bw. Stephen Mbundi (katikati), Kiongozi wa kikao cha ngazi ya wataalam ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitoa taarifa kwa Makatibu Wakuu. Wengine katika picha ni Dkt. Yamungu Kayandabila (kushoto), Naibu Gavana na Bw. Bernard Haule, Kaimu Mkurugenzi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Evaristo Longopa (wa pili kulia) akichangia jambo wakati wa kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wengine katika picha ni Prof. Sifuni Mchome (wa kwanza kulia), Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Joseph Buchweshaija, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na Prof. Siza Tumbo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo.
Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima (kulia) akifuatilia kikao hicho akiwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina KH. Shaaban
Wajumbe ambao ni Wataalam kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali wakifuatilia kikao

Kikao kikiendelea

Wajumbe wengine wakiwa kwenye kikao

Wajumbe wa kikao wakifuatilia kikao 

Wajumbe kutoak Wizara, Idara na Taasisi za Serikali walioshiriki kikao 


Wajumbe wengine nao wakifuatilia kikao


Wataalam wa masuala mbalimbali kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali wakiwa kwenye kikao

Wataalam wakinukuu masuala mbalimbali yaliyokuwa yanajadiliwa kwenye kikao hicho
Kikao kikiendelea


Kikao kikiendelea


Wasaudia watafuta Fursa za Kuwekeza katika Viwanda Tanzania

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wasaudia watafuta Fursa za Kuwekeza katika Viwanda Tanzania

Ujumbe wa wawekezaji wa makampuni makubwa 15 ya Saudi Arabia utafanya ziara nchini Tanzania tarehe 30 na 31 Januari 2019 kwa madhumuni ya kuangalia fursa ya kuwekeza kwenye viwanda.

Ziara hiyo inatokana na juhudi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Saudi Arabia na wadau wengine  wa kushawishi wafanyabiashara wakubwa kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Ujumbe huo wa watu 20, utakapokuwa nchini pamoja na mambo mengine, utashiriki kongamano la biashara litakalofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini Dar Es Salaam tarehe 30 Januari 2019 kuanzia saa mbili asubuhi. Kongamano hilo litafuatiwa na mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Saudi Arabia.

Kongamano hilo linaloratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) litatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kusikiliza mada mbalimbali kuhusu fursa, vivutio, sheria na kanuni za uwekezaji nchini kutoka taasisi zinazoratibu masuala ya uwekezaji ikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Ujumbe huo pia unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi mbalimbali; zikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Ziara ya ujumbe huo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi na inalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
29 Januari 2019
  

Monday, January 28, 2019

Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC yaanza jijini Arusha


Bw. Stephen Mbundi, Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiongoza  Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa  majadiliano kwa ngazi ya Watalaam wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa maandalizi ya  Mkutano Maalum wa 38 wa  Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika tarehe 30 Januari 2019 jijini Arusha. Mkutano huu utafuatiwa na ule wa Makatibu Wakuu tarehe 29 Januari 2019. Pamoja na mambo mengine  mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri utapitia na kujadili agenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo; taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na  masuala ya utawala na fedha. Mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Arusha tarehe 1 Februari 2019. Kulia ni Bw. Eliabi Chodota, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii na kushoto ni Bw. Bernard Haule, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam (wa pili kushoto)  akizungumza wakati wa mkutano wa maandalizi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha tarehe 28 Januari 2019
Wajumbe kutoka Burundi wakifuatilia mkutano huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwuliofanyika jijini Arusha tarehe 28 Januari 2019  ngazi ya wataalam
Wajumbe kutoka Kenya nao wakifuatilia mkutano wa wataalam
Wajumbe kutoka Uganda wakiwa kwenye mkutano
Wajumbe kutoka Tanzania nao wakifuatilia mkutano huo 
Wajumbe wengine kutoka Tanzania nao wakifuatilia mkutano


Wajumbe wa Tanzania kutoka Wizara, Taasisi na Sekta mbalimbali wakishiriki mkutano kwa ngazi ya wataalam

Wawekezaji kutoka Austria wavutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini

Afisa mwandamizi wa Ubalozi wa Austria wenye makazi yake Nairobi, Kenya. Bw. Kurt Muellauer akifungua Kongamano la Biashara lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda Tanzania (TCCIA) na Ubalozi wa Austria. Kongamano hilo nimwendelezo wa jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambao unawakilisha pia nchini Austria na wadau mbalimbali katika kutekeleza diplomasia ya uchumi. Pamoja na mambo mengine kampuni 8 kati 16 zinatarajiwa kufanya ziara jijini Dodoma tarehe 29 Januari kwa lengo la kukutana na Mawaziri wa Kilimo; Nishati; Fedha na Mipango; Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kongamano hilo limefanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa TIC, Bw. John Mnali, pamoja na wadau wengine wakimsikiliza kwa makini Bw.Muellauer (hayupo pichani). 
Baadhi ya wawekezaji kutoka Austria nao wakifuatilia kongamano hilo.
Kaimu Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na Wenyeviwanda Tanzania (TCCIA), Bw. Octavian Mshiu, akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, ambapo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji nchini na kuunga mkono Sera ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya Uchumi wa Viwanda nchini.  


 Juu na chini wadau wakiendelea kufuatilia mada mbalimbali wakati wa kongamano

Afisa wa Uhamasishaji Uwekezaji (TIC), Bi. Diana Ladislaus akizungumzia fursa za uwekezaji nchini wakati wa kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Tunataka tushirikiane ili tuweze kuwekeza nchini Tanzania 
Majadiliano yanayoonesha dalili ya kuzaa matunda ya ushirikiano kati ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Austria