TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Tanzania
yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India
Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Taasisi za Serikali
na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini zimeshiriki Maonesho ya
Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 nchini India yajulikanayo kama OTM 2019
[Outbound Travel Mart-2019] kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za
soko la utalii nchini humo.
Maonesho hayo maarufu na makubwa kabisa katika
ukanda wa Asia-Pasifiki yalianza tarehe 23 Januari, 2019 na yamemalizika leo
tarehe 25 Januari, 2019, Maonesho haya hufanyika kila mwaka katika Jiji la
Mumbai na kushirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani.
Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) na Kituo cha Kutangaza Utalii wa Zanzibar India [Zanzibar Tourism
Promotion Centre]. Kwa upande wa kampuni binafsi ni Leopard Tours, Zara Tours,
Ngarawa Hotel and Resort, DOTCOM Safaris Ltd na Jackal Adventures.
Katika Maonesho hayo, Banda la Tanzania limeibuka
Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia
watu wengi [The winner of Best Decoration Award].
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda
amesema kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya
utalii ambapo wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya
utalii walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Washiriki
wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya
biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na
kufanya biashara.
Akiwa katika maonesho hayo, Balozi Luvanda alieleza
kuwa maonesho yalisaidia washiriki kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa
kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao
kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida
zake. Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Tunategemea idadi ya
watalii kutoka India wanaokwenda Tanzania itaongezeka mara dufu baada ya kuanza
kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] moja kwa
moja kutoka Tanzania kuja India ambapo zinategemewa kuanza kabla ya mwezi wa
Juni 2019.
‘Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana
Maafisa wote walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi
nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Banda bora
lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration
Award]”, alisema Balozi Luvanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
25 Januari 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.