Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga akichangia agenda wakati wa Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Mkutano wa 48 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeanza leo, Mei 29, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.
Mkutano huo umeanza kwa kikao cha ngazi ya Wataalamu kitakachofanyika kuanzia Mei 29 hadi Juni 1, 2026, nakufuatiwa na Makatibu Wakuu kinachotarajiwa kufanyika Juni 2 hadi 3, 2026, kabla ya Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika Juni 4, 2026.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unatarajiwa kupokea na kujadili taarifa mbalimbali ikiwemo; utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa SCTIFI, taarifa za Kamati ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki, Kamati ya Uwekezaji, Kamati ya Masuala ya Ushindani ya Afrika Mashariki pamoja na Kamati ya Viwanda.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Forodha katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Flavia Busingye, amewataka wataalamu hao kujikita katika majadiliano yatakayotoa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazoathiri ukuaji wa biashara ndani ya Jumuiya.
Bi. Busingye amesema ni muhimu kwa Nchi Wanachama kuendelea kushirikiana katika kuondoa vikwazo vya kibiashara, ikiwemo changamoto zinazohusiana na masuala ya kodi, pamoja na kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo na maamuzi yaliyotolewa katika vikao mbalimbali vya Jumuiya, hususan maamuzi ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC.
Kupitia mkutano huo wa SCTIFI, Jumuiya inalenga kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kukuza biashara ya mipakani, kuondoa vikwazo vya biashara na kuchochea maendeleo ya viwanda katika Nchi Wanachama.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ngazi ya Wataalamu unaongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga, akiwa ameambata na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Ulimwengu katika Wizara hiyo, Balozi Thobias Makoba, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.





