Friday, June 30, 2017

Tanzania na Norway kushirikiana katika masuala ya siasa na diplomasia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufalme wa Norway, Mhe. Borge Brende wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano kuhusu kushirikiana katika Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.Ttukio hilo lilifanyika jijini Dar Es Salaam kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Dora Msechu, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Hanne Marie Kaarstad, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Bi. Mary Matari, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga (hawapo pichani).
Waheshimiwa Mawaziri wakibadilishana mikataba mara baada ya kuweka saini
Dkt. Mahiga akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza zoezi la uwekaji saini na Mgeni wake.
Mhe. Brende naye akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa Habari.
Balozi wa Tanzania nchini Norway mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Dora Msechu (wa pili kutoka kulia), Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Hanne Marie Kaarstad (wa kwanza kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Bi. Mary Matari (wa kwanza kushoto) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga wakifuatilia kwa makini mkutano wa waandishi wa habari na Mawaziri wa Mambo ya Nje.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Waziri wa Norway nao wakifuatilia mkutano wa waandishi wa habari na Mawaziri wa Mambo ya Nje.
sehemu ya waandishi wa habari wakiwasikiliza kwa makini Mawaziri walipokuwa wakiendelea kuzungumza (hawapo pichani).


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Norway kushirikiana katika masuala ya siasa na diplomasia

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ameeleza kuwa kusainiwa kwa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu kushirikiana katika Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway kumefungua sura mpya ya mahusiano kati ya nchi hizo mbili. 

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar Es Salaam wakati anaongea na waandishi wa habari baada ya shughuli ya uwekaji saini wa makubaliano hayo aliyoifanya kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Borge Brende kukamilika.

Alisema kusainiwa kwa MoU hiyo kutazifanya nchi hizo kuwa na mahusiano ya karibu zaidi katika kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kisiasa na kidiplomasia ambayo kimsingi yalikuwepo tokea zamani lakini leo yamerasimishwa. 

Mhe. Mahiga amewambia wanahabari kuwa Tanzania na Norway zimekuwa zikishirikiana kiuchumi, kiteknolojia na kijamii kwa takribani miaka 55 sasa. Baadhi ya maeneo aliyoyataja ambayo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika kipindi hicho ni pamoja na uzalishaji wa nishati ya umeme hususan vijijini, afya, elimu, kilimo na utunzaji wa misitu.  

Mhe. Mahiga aliendelea kueleza kuwa katika kikao chao, wamejadili maeneo mapya ya ushirikiano yakiwemo utunzaji wa mazingira na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa sekta binafsi za nchi hizo mbili kinyume na awali mahusiano zaidi yalikuwa baina ya Serikali mbili.
Waziri Mahiga ameishukuru Norway kwa jitihada zake ziliozasaidia uvumbuzi na uchimbaji wa gesi asilia nchini kupitia kampuni ya Statoil ambayo imewekeza nchini mtaji mkubwa kuliko mahali popote Afrika.

Alihitimisha hotuba yake kwa kusema kuwa Tanzania itaendelea kufaidika kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wake na Norway kwa kuwa nchi hiyo ina utajiri mkubwa katika sekta ya mafuta misitu na teknolojia ya hali ya juu katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway alieleza kuwa Norway imekuwa ikishirikiana na Tanznaia katika sekta za maendeleo tokea mwaka 1964 na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania hadi hapo nchi hiyo itakapokuwa na uwezo wa kugharamia miradi yake yenywe. 

Waziri Borge kabla ya kuondoka nchini leo jioni, atashiriki uzinduzi wa programu ya kushirikiana katika masuala ya kodi na uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kuendeleza mafuta(oil for development program) utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.  

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 30 Juni 2017



Thursday, June 29, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway kuzuru Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufalme wa Norway, Mhe. Borge Brende atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini tarehe 29 na 30 Juni 2017. Madhumuni ya ziara ya Mhe. Brende ambaye atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 29 saa tatu usiku ni kuimarisha mahusiano kati ya Norway na Tanzania.

Wakati wa ziara yake, Mhe. Waziri Brende pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Juni 2017. 

Aidha, siku hiyo hiyo asubuhi, mgeni huyo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere na baadaye wataweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu Ushirikiano wa Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili. 

Mhe. Borge pia atakutana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango (Mb.) ambapo kwa pamoja watashiriki katika uzinduzi wa programu ya kushirikiana katika masuala ya kodi na uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kuendeleza mafuta(oil for development program) utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro tarehe 30 Juni 2017.  Uzinduzi wa programu hizo pia utahudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb.) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Charles Kichere. 

Ratiba ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway inaonesha pia kwa kushirikiana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb.) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani watashiriki katika shughuli za kufunga semina ya Mradi wa Kusindika Gesi asilia (LNG) iliyoandaliwa na kampuni ya mafuta ya kutoka Norway inayoitwa Statoil ambayo pia inaendesha shughuli zake hapa nchini. Semina hiyo inafanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri baada ya kukamilisha ratiba yake nchini atarejea Norway siku ya Ijumaa tarehe 30 Juni 2017 saa nne usiku.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29 Juni 2017



Waziri Mahiga akutana na kaimu Balozi wa Marekani nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dkt. Inmi K. Patterson, alipokutana naye Wizarani Jijini, Dar es Salaam, tarehe 29 Juni, 2017. Mazungumzo yao yalijikita katika masuala ya ushirikiano ambapo wameahidi kuendeleza ushirikiano katika sekta za maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi ili kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali zao.   

Mazungumzo yakiendelea, kushoto ni ujumbe uliombatana na Kaimu Balozi, wa kwanza kushoto ni afisa tawala wa ubalozi wa Marekani Bw.Jay Zimmerman, pembeni yake ni afisa habari wa Ubalozi huo, Bi. Lauren Ladenson na kulia ni afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Redempta Tibaigana.

Wednesday, June 28, 2017

Waziri Mahiga ampokea Mjumbe Maalum kutoka Sahrawi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) amepokea Ujumbe Maalumu kutoka kwa Rais wa Sahrawi ambao uliwasilishwa kwake na Mjumbe Maalum ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Hamdi Mayera. Baada ya kuwasilisha ujumbe huo viongozi hao wawili walifanya mazungumzo yaliyojikita kwenye kuendeleza mahusiaono ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Saharawi. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Balozi wa Sahrawi nchini Tanzania Mhe. Brahim Buseif.
Dkt. Mahiga akimsikiliza Mhe.Mayera
Balozi wa Sahrawi hapa nchini Mhe. Buseif (wa kwanza kushoto) pamoja na Dkt. Mahiga wakimsikiliza Mhe. Mayera alipokuwa akiendelea kuzungumza.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Suleiman Salehe (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Afisa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Nicholus Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Gerald Mbwafu na katikati ni  nao kwa pamoja wa kisikiliza mazungumzo kati ya Mhe. Mayera na Dkt. Mahiga (hawapo pichani).
Waziri Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum, Mhe. Mayera (wa tatu kushoto) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Balozi Buseif.

Balozi wa Tanzania nchini Brazil awasilisha Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Brazil Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Brazil Mhe. Michel Temer, Tarehe 26 Juni, 2017. Rais Temer alisifu jitihada za Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupigana na umasikini na kuleta maendeleo kwa wananchi. Brazil imeihakikishia kuunga mkono juhudi za Serikali  ya Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya ushirikiano.
Mhe. Rais Michel Temer na Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil Mhe. Aloysio Nunes Ferreira Filho (wa tatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, watatu kutoka kulia ni Mama Balozi Jane Nchimbi, Bw. Frank J. Mhina, Afisa Ubalozi na Mkuu wa Utawala; na Bw. Suleiman Mombo, Afisa Mwandamizi wa Ubalozi.
Balozi Dkt. Nchimbi na Mama Balozi Jane Nchimbi, wakisindikizwa Mara baada ya kumaliza kuwasikisha hati za Utambulisho kwa Rais.

Friday, June 23, 2017

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA NGAZI ZA JUU WA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima (wa kwanza kushoto), akiwa pamoja na wageni waalikwa wengine wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa.
Sehemu nyingine ya wageni waalikwa walio hudhuria mkutano huo.
Rais wa zamani wa nchi ya Georgia, Mhe. Mikheil Saakshvili akihutubia na kutoa uzoefu wa nchi yake kuhusu mapambano dhidi ya rushwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Sehemu nyingine ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akielezea ratiba nzima ya Mkutano huo.
Sehemu ya Wajumbe waliohudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa  wa Ngazi ya Juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa , Rais huyo wa zamani alitoa uzoefu wake na wa nchi yake katika kupambana na rushwa.
Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa tatu kutoka kushoto), Mhe. Mikheil Saakshvili (mwenye tai nyekundu),
wakifurahia jambo kwa pamoja na Mhe. Angela Kairuki Waziri Ofisi ya Rais na Manajimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora wa tatu kutoka kulia.
Bi Mindi Kasiga akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anaye hudumia nchi za Tanzania, Malawi, Burundi, Bella Bird mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu wa Mapambano dhidi ya Rushwa.