TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali Mpya ya Lesotho yashauriwa
kutekeleza Mageuzi - SADC
Serikali
itakayoingia madarakani baada ya Uchaguzi
wa Wabunge uliofanyika nchini Lesotho Julai 3, imeshauriwa kutekeleza kikamilifu
na kwa nia ya dhati maazimio yote ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC yanayohusu mageuzi kwenye sekta muhimu za
katiba, sheria na mahakama, ulinzi na usalama, utumishi na sekta ya umma na
vyombo vya habari kwa muda muafaka ili kuimarisha utawala bora na wa
kidemokrasia nchini humo.
Mnamo
mwezi Machi mwaka 2017, baada ya Mfalme Letsie wa III wa Lesotho kutangaza
tarehe ya uchaguzi mkuu, kikao cha juu cha maamuzi cha Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC Summit), kilielekeza Serikali mpya itakayoshinda
uchaguzi na kuingia madarakani, itekeleze maazimio hayo kwa kuweka muda maalum
na vigezo vya utekelezaji ili kuepuka chaguzi za mara kwa mara.
Msimamo
huo wa Jumuiya ya SADC umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki wa Tanzania Mheshimiwa Augustine P. Mahiga, Mwenyekiti wa
Kamati ya Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC alipokuwa
akitoa taarifa ya awali ya timu ya uangalizi siku mbili baada ya zoezi la
upigaji kura kukamilika.
Mheshimiwa
Mahiga alisema, japokuwa zoezi la kuhesabu kura bado linaendelea, ni dhahiri
kuwa wapiga kura nchini Lesotho wanatarajia mageuzi makubwa kutoka kwenye
Serikali mpya yatakayoandika historia mpya nchini Lesotho, ambayo imafanya
chaguzi tatu kuu ndani ya miaka mitano.
Mapendekezo
mengine yaliyotolewa kwenye taarifa hiyo ya awali ya SADC yanaitaka Serikali
mpya kupitia na kufanyia mageuzi mfumo mzima wa uchaguzi ambao kwa sasa unatoa
fursa kwa wabunge kuhama chama bila kupoteza ubunge wao (Floor Crossing). Alisema
mfumo huo unayumbisha mfumo wa siasa na wa kibunge kwenye Falme ya Lesotho.
Kwenye
upande wa ulinzi na usalama wa raia wakati wa uchaguzi, taarifa hiyo ilisifu
Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho kwa kuendesha kwa weledi mkubwa zoezi la
upigaji kura na kushirikiana na Jeshi la Polisi kuimarisha usalama vituoni kwa
mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Hata
hivyo taarifa za awali za waangalizi wa kimataifa zimeeleza kuwa Jeshi la
Lesotho pia lilionekana kwenye baadhi ya maeneo, nje ya vituo wakiimarisha ulinzi kwa mujibu wa
sheria ya jeshi hilo. Balozi Mahiga
alieleza kuwa japokuwa uwepo wa jeshi hakuathiri
mwenendo mzima wa upigaji kura, bado kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ndani ya
vyombo hivyo ili kuainisha majukumu ya kila taasisi na kuondoa muingiliano wa
kimajukumu kama ilivyo sasa.
Mapendekezo
mengine yaliyotolewa na Jumuiya ya SADC kwa Serikali mpya nchini humo ni kuweka
mazingira bora yatakayowezesha wanawake na watu wanaoishi na ulemavu kushiriki
kikamilifu kwenye shuguli za kisiasa bila ubaguzi. Vilevile kuifanyia mageuzi
sekta ya habari nchini na kuwawezesha wananchi kupata habari za uhakika na kwa
wakati.
Matokeo
ya uchaguzi wa Wabunge yanaendelea kutangazwa ambapo na yanatarajiwa kukamilika
ndani ya siku mbili ambapo upinzani mkali unaonekana baina ya Chama cha
Democratic Congress kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa Mhe. Pakalitha
Mosisili na Chama cha All Basotho Convention kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa
zamani Mhe. Thomas Motsoahae Thabane.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Maseru, Lesotho, 05 Juni 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.