Friday, February 28, 2020

MASENETA WA UFARANSA KUFANYA ZIARA NCHINI


Ujumbe wa maseneta sita (6) kutoka Ufaransa unatarajiwa kufanya ziara nchini kuanzia tarehe 01 hadi 08 Machi, 2020.  

Ujumbe huo utawasili nchini tarehe 29 Februari, 2020 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar utaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Ufaransa inayoshughulikia masuala ya Maendeleo Endelevu na Naibu Rais wa Kikundi cha Kirafiki na nchi za Bahari ya Hindi Seneta Harve Maurey.


PROF. KABUDI AHUTUBIA BARAZA LA HAKI ZA BINADAMU LA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akihutubia katika Kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea Geneva,nchini Uswisi ambalo linatarajiwa kumalizika March 20,2020 ambapo masuala kadhaa kuhusu haki za binadamu yanajadiliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akitoa hotuba ya Tanzania katika Kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea Geneva,nchini Uswisi ambalo linatarajiwa kumalizika March 20,2020 ambapo masuala kadhaa kuhusu haki za binadamu yanajadiliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipongezwa na Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Maimuna Tarishi pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mara baada ya kutoa hutuba katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipongezwa na baadhi ya viongozi wa Mataifa ya Afrika wanaohudhuria Mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea Geneva,Uswisi
Wednesday, February 26, 2020

PROF. KABUDI AKUTANA NA KATIBU MKUU JUMUIYA YA MADOLA


Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (katikati aliyeshika kalamu) akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland. Kushoto kwa Prof. Kabudi ni Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Balozi Maimuna Tarishi pamoja na Wakurugenzi na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland akiwa katika mazungumzo na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (hayupo pichani) Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi. Kulia ni msaidizi wa Bi Patriacia Scotland.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb)akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland.Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi. Kushoto kwa Bi. Patricia Scotland ni Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Balozi Maimuna Tarishi
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi.
TANZANIA YAKABIDHIWA TAKWIMU ZA UFANYAJI BIASHARA KATI YAKE NA JUMUIYA YA MADOLA.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland mazungumzo yaliyolenga masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mradi ambao Jumuiya ya Madola umeufanya kuhusu Tanzania.

Mradi huo umelenga kuangalia takwimu mbalimbali zinazohusu biashara kwa kuangalia nchi ambazo Tanzania inaagiza ama kuuza bidhaa zake kwa wingi katika nchi za Jumuiya ya Madola mradi ambao umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania ambapo kwa sasa nchi za India na Afrika kusini ndizo kinara.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland amesema Tanzania ni mdau muhimu katika jumuiya hiyo na kwamba amefurahi kumkabidhi Prof. Kabudi nakala ya utafiti huo kwa niaba ya Tanzania jambo litakaloifanya Tanzania kuendelea kuangalia maeneo ya kujiimarisha katika ufanyaji wa biashara na nchi za Jumuiya ya Madola.

Mbali na masuala hayo ya mradi huo wa takwimu wa biashara kuhusu Tanzania uliofanywa bure na Jumuiya hiyo ya Madola pia wawili hao wamezungumzia masuala mengine ikiwa ni pamoja na namna Jumuiya hiyo na Tanzania zitakavyofanya kuongeza usawa wa jinsia,masuala ya haki za binadamu pamoja na uimarishaji wa mfumo wa mahakama nchini Tanzania.
Tuesday, February 25, 2020

TANZANIA YASHIRIKI KWA MARA YA KWANZA KATIKA MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIDHAA ZA KILIMO YA PARIS

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo (katikati) akiwa  kwenye picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki kwa mara ya kwanza katika Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Kilimo ya Paris yanayofanyika mjini humo kuanzia tarehe 22 Februari 2020 hadi tarehe 1 Machi 2020.
Wageni mbalimbali wakipata maelezo kuhusu fursa za bidhaa za kilimo zinazopatikana Tanzania walipotembelea Banda la la Tanzania wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Kilimo yanayofanyika jijini Paris kuanzia tarehe 22 Februari 2020 hadi tarehe 1 Machi 2020.
======================================================


TANZANIA YASHIRIKI KWA MARA KWANZA KATIKA MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIDHAA ZA KILIMO YA PARIS 2020, UFARANSA

Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza katika Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Kilimo ya Paris 2020 yanayofanyika jijini Paris, Ufaransa kuanzia tarehe 22 Februari 2020 hadi tarehe 1 Machi 2020.

Maonesho hayo ambayo yalifunguliwa na Mhe. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, yanatarajiwa kutembelewa na zaidi ya watu 600,000.

Wakati wa maonesho hayo, Tanzania itapata fursa ya kuonyesha bidhaa zake yakiwemo mazao ya kimkakati. Ujumbe wa Tanzania katika maonyesho hayo unaongozwa na Bw. Victor Rugemalila kutoka TANTRADE.

Ubalozi wa Tanzania ambao unaratibu maonesho hayo kupitia  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, unaishukuru Kampuni ya Tanzania Re-assurance (TAN-RE) ya Dar es Salaam, Tanzania, kwa kufadhili kwa kiasi kikubwa ushiriki wa Tanzania katika maonyesho. Aidha, Ubalozi unatambua mchango wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Kahawa  ya Inter State.


Monday, February 24, 2020

PROF. KABUDI AKUTANA NA VIONGOZI MBALIMBALI AKIWA GENEVA - USWISI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb) akisaini katika kitabu cha wageni katika ubalozi  wa kudumu wa Tanzania umoja wa Mataifa uliopo Geneva Nchini Uswisi

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Geneva,Uswisi


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Filippo Grand(hayupo Pichani). Mazungumzo hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya Ofisi za UNHCR zilizopo Geneva-Uswisi

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Filippo Grand akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (hayupo pichani)
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya Ofisi za UNHCR zilizopo Geneva-Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Filippo Grand Mazungumzo hayo yamefanyika katika Makao Makuu ya Ofisi za UNHCR zilizopo Geneva-Uswisi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw. Filippo Grand mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Makao Makuu ya Ofisi za UNHCR zilizopo Geneva-Uswisi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland Mhe. Simon Coveney. Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu Geneva,Uswisi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland Mhe. Simon Coveney akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu Geneva,Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiagana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland Mhe. Simon Coveney mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu Geneva,Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akizungumza na Waziri wa mambo ya Nje wa Denmark Bw. Jeppe Kofod.Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Binadamu Geneva,Uswisi. Anayeshuhudia kulia ni Balozi wa kudumu wa Tanzania umoja wa Mataifa Geneva,Balozi Maimuna Tarishi.

Sunday, February 23, 2020

TANZANIA YASHINDA TUZO YA UTALII NCHINI INDIA

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda (kulia) akipokea Tuzo ya Utalii baada ya Tanzania kuibuka mshindi kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la Utalii wa Wanyamapori duniani nchini India kwa mwaka 2020 (The Best International Wildlife Destination) iliyotangazwa katika hafla ya kutoa tuzo hizo zilizotolewa na Jarida la Utalii la "Outlook Traveller Magazine" na kufanyika katika Hoteli ya Rossette jijini New Delhi, India tarehe 22 Februari 2020.
Mhe. Balozi Luvanda akifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika hafla ya kutoa tuzo za utalii zilizotolewa na Jarida la "Outlook Traveller Magazine" na kufanyika katika Hoteli ya Rossette jijini New Delhi, India tarehe 22 Februari 2020. Tanzania iliibuka mshindi kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani nchini India kwa mwaka 2020.
===============================================================


TANZANIA YASHINDA TUZO YA UTALII NCHINI INDIA

Tanzania imeshinda tuzo ya utalii kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani nchini India kwa mwaka 2020 (The Best International Wildlife Destination).

Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka H. Luvanda amepokea Tuzo hiyo kutoka Jarida la kihindi la “Outlook Traveller Magazine” katika hafla maalum iliyofanyika katika Hoteli ya Roseate jijini New Delhi kwa niaba ya Tanzania. Hafla hiyo ilihudhuriwa na takriban washiriki 200.  

Tanzania imepata ushindi huo kutokana na kura zilizopigwa kwenye mtandao wa jarida hilo la “Outlook Traveller” lililoshirikisha wapiga kura 1,200,000 kwa njia ya mtandao.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushinda tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka nchini India, washiriki kupitia jarida hilo wameichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani.

Aidha, Shelisheli na Indonesia kwa pamoja zilishinda tuzo kama maeneo bora zaidi duniani kwenye utalii wa fukwe.

The Outlook Traveller Award ni tuzo ya kifahari zaidi katika sekta ya utalii nchini India na hutolewa na Jarida la Utalii la “Outlook Traveller Magazine” ambalo ni jarida namba moja nchini India linalojishughulisha kutangaza utalii, ndani na nje ya India.

Wakati akipokea tuzo hiyo, pamoja na mambo mengine Balozi Luvanda aliushukuru uongozi wa Jarida hilo kwa kuandaa tuzo hizo muhimu ambazo zinasaidia kutanganza utalii wa nchi mbalimbali nchini India na akaeleza kuwa kupitia tuzo hiyo, watu wengi zaidi wataijua Tanzania na vivutio vingi vya utalii vilivyopo nchini na kuwavutia kutembelea Tanzania.

Mafanikio hayo yanatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini India, Wizara za Utalii za Tanzania Bara na Zanzibar, na Taasisi zote zinazosimamia masuala ya utalii za ndani na nje ya nchi katika kutangaza vivutio vya utalii kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo India.

Kupitia juhudi hizi, idadi ya watalii wanaokuja Tanzania kutoka India imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, idadi hiyo iliongezeka kutoka watalii 39,115 mwaka 2016 hadi watalii 69,876 mwaka 2017.  

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi zake ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini India na wadau wengine itaendelea kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ili kuhakikisha idadi ya watalii kutoka India na nchi zingine duniani inaongezeka. Hii ni pamoja na kutumia Shirika la Ndege la Tanzania ambalo limeanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai kuanzia mwezi Julai 2019 kwa upande wa India.UNESCO YATAMBUA KISWAHILI KAMA LUGHA ITAKAYOSAIDIA KUKUZA UTANGAMANO BARANI AFRIKA

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Mhe. Samwel Shelukindo akizungumza kwenye Mjadala kuhusu "Fursa na Changamoto za Kukitambua Kiswahili kama Lugha rasmi ya Bara la Afrika kwa ajili ya kukuza Utangamano. Mjadala huo uliandaliwa na Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yaliyofanyika jijini Paris, Ufaransa hivi karibuni.
Sehemu ya Wataalam wa Lugha ya Kiswahili akiwemo Prof. Aldin Mutembei (wa pili kushoto) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakishiriki kwenye mjadala kuhusu Lugha ya Kiswahili wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yaliyofanyika Paris, Ufaransa hivi karibuni
Sehemu ya washiriki wa Mjadala huo wakifuatilia kama wanavyoonekana katika picha


Mhe. Balozi Shelukindo (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya Wajumbe kutoka UNESCO  wakiangalia machapisho mbalimbali ya Lugha ya Kiswahili yaliyoandaliwa  na Ubalozi baada ya kushiriki mjadala kuhusu Lugha ya Kiswahili ulioandaliwa na Ubalozi kwa kushirikiana na UNESCO.
===========================================================================

UNESCO YATAMBUA KISWAHILI KAMA LUGHA ITAKAYOSAIDIA KUKUZA UTANGAMANO BARANI AFRIKA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitambua Lugha ya Kiswahili kama lugha itakayosaidia kukuza utangamano Barani Afrika wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yenye kaulimbiu “Lugha Bila Mipaka” iliyofanyika jijini Paris, Ufaransa hivi karibuni.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa kushirikiana na UNESCO uliandaa mjadala kuhusu "Fursa na Changamoto za Kukitambua Kiswahili kama Lugha rasmi ya Bara la Afrika kwa ajili ya kukuza Utangamano".

Akizungumza wakati wa Mjadala huo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Mhe. Samwel Shelukindo pamoja na mambo mengine, alieleza hatua iliyochukuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha zitakazotumika katika Jumuiya hiyo.

Aidha, Mhe. Balozi Shelukindo alizipongeza nchi za Afrika  Kusini na Namibia kwa kuwa nchi za kwanza Kusini mwa Afrika  zilizoamua kuanzisha ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika shule mbalimbali. Mjadala huo uliwashirikisha Wataalam mbalimbali akiwemo Prof. Aldin Mutembei kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,

Kufanyika kwa mjadala huo katika UNESCO ni moja ya juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa za kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha zitakazotumika katika UNESCO. 


Friday, February 21, 2020

Rais wa Zanzibar afungua Kikao cha Mawaziri wa SADC

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema “Kufanyika kwa Mkutano wa SADC ni hatua muhimu katika kujenga matumaini mapya ya wananchi kuhusiana na maafa, tukizingatia kwamba katika miaka ya hivi karibuni  kumekuwa na ongezeko kubwa la  maafa pamoja na viashiria  vyake  katika nchi wanachama wa SADC.”Ameyasema hayo wakati akifungua  Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu  Mhe. Jenista Mhagama amesisitiza “Ushiriki wa kisekta katika kukabiliana na maafa ni njia pekee ya kupunguza madhara ya  maafa kwa Nchi wanachama wa SADC”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia maafa na kusisitiza kuwa  “Majanga hayana urasimu kitu muhimu kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana nayo pindi yanapotokea nchini”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.  
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC wakiwemo Mawaziri, Washauri wa Rais na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na Usalama wakisikiliza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na Maafa Zanzibar, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wenye dhamana ya Menejementi ya maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC baada ya kufungua Mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.


Na. OWM, ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema maeneo ya visiwa yapo katika hatari  kubwa  zaidi ya kukumbwa na maafa ukilinginisha na maeneo mengine duniani, hivyo alitoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuja na mikakati imara itakayoainisha mbinu za kutambua na kuwahi viashiria vya maafa kabla madhara hayajatokea.

“Tuna jukumu la kuendelea kushirikiana kati ya Serikali zetu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa, Taasisi za Utafiti, Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini, Taasisi za Fedha na  Mashirika yasiyo ya Serikali, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari katika suala hili. Tukifanya hivyo, itakuwa tumeitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mkutano huu isemayo:  “Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.” 

Rais Shein amesema hayo leo tarehe 21, Februari, 2020 Zanzibar alipokuwa anafungua kikao cha Mawaziri wa nchi za SADC wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa.

Rais Shein ameeleza kuwa maafa yana madhara makubwa katika nchi, endapo hakutakuwa na mipango thabiti ya kukabiliana nayo na kutolea mfano namna vimbunga vya Idai, Kenneth na vinginevyo vilivyosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbawe, Msumbiji na Comoro.

Rais Shein amefafanua kuwa maafa yanabadilisha agenda za maendeleo ya nchi mbali mbali duniani kwa sababu fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinabadilishwa matumizi kukidhi dharura za maafa kwa gharama kubwa zaidi.

Akitoa mfano wa mpango wa Sendai wa kukabiliana na maafa ambao unaonesha kati ya mwaka 2015 hadi 2018 nchi za Afrika zimekubwa na matukio 160 ya maafa ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Ameeleza kuwa mpango huo unaonesha kuwa zinahitajika Dola za Marekani bilioni 3700 ili nchi zilizoathirika ziweze kurejesha hali yake ya kawaida. “Kiasi kikubwa hiki cha fedha kinatumika kujenga upya miundombinu iliyoharibika badala ya kujenga miundombinu mipya”, Rais Shein alisema.

Rais wa Zanzibar amewambia wajumbe wa mkutano huo hatua zilizo fanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha uhimili wa kukabiliana na maafa, kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni miongoni mwa visiwa ambavyo hupata madhara ya maafa.

Hatua hizo ni pamoja na kuandaa Sera ya kukabiliana na maafa ya mwaka 2011 na sheria yake ya mwaka 2015, kuanzisha Kamisheni inayoshughulikia masuala ya maafa na mpango wa mawasiliano wakati wa maafa. 

Aidha, amebainisha hatua nyingine kuwa ni pamoja na mpango wa elimu ya kujikinga na maafa kwa wanianchi, kuimarisha vyombo vya usafiri wa baharini ikiwemo ununuzi wa meli mbili kubwa za MV. Mapinduzi II ya abiria na MV. Ukombozi II kwa ajili ya kubeba mafuta, ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufuatilia usafiri wa majini ikwemo ndege zisizokuwa na rubani na boat za uokoaji na kuzimia moto.

Dkt. Shein amesema ili kukabiliana na maafa ya mafuriko ambayo huwa yanakikumba kisiwa hicho kutokana na mvua za mwezi Oktoba hadi Desemba na mwezi Machi hadi Juni, nchi hiyo kwa msaada wa Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) imejenga kituo cha kuhifadhi watu wanaoathirika na mafuriko ambacho kina nyumba 30 zenye miundombinu yote kwa ajili ya maisha ya mwanadamu.

Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua mkopo wa Dola za Marekani milioni 93 kwa ajili ya ujenzi wa mitaro inayopeleka maji baharini wakati wa mafuriko. Ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho utakapokamilika, Dkt. Shein aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa, Zanzibar itaweza kuepuka mafuriko au Kupunguza kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Muhagama (Mb)ameeleza kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Kamati ya Mawaziri wenye Dhamana ya Maafa likiwemo lengo la kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC namna ya kupunguza madhara ya maafa. Alisema maafa yaliyosababishwa na majanga ya vimbunga vya Idai na Kenneth katika nchi za SADC, ukame na mafuriko ambayo hayana mipaka yamedhihirisha umuhimu wa nchi hizo kuwa na mpango wa ushirikiano wa kukabiliana na maafa.

Alieleza ili kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo wake wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote. 

Amebainisha hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Madhara ya Maafa; kuandaa Wasifu wa Janga la Mafuriko na Ukame; kuandaa Mpango wa Dhamira ya Taifa wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi; kuandaa Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji wa Taarifa za Gesi Joto;  Kuandaa Mipango ya Kukabiliana na Dharura za Afya ya Binadamu, Mifugo na Wanyama; kuandaa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna.

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa majanga hayataki urasimu yanapotokea, yanahitaji hatua za haraka na zinazoeleweka ili kuyakabili ipasavyo kabla hayajasababisha madhara makubwa.

Dkt. Tax alifafanua kuwa mkutano huo kufanyika Zanzibar ni fursa nzuri kwa nchi za SADC kujua vizuri muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka mingi sasa. Aidha, alisema itakuwa fursa nzuri kwa nchi hizo kujionea vivutio vya kipekee vya kisiwa cha Zanzibar ambacho kina umaarufu mkubwa duniani kote.

Serikali ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika baada ya Tanzania kuchukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, mwaka huu (2020).  Hatua hii inatokana na utaratibu wa kawaida wa mzunguko wa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
MWISHO.