Friday, August 30, 2019

TANGAZO LA NAFASI ZA AJIRATAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuujulisha Umma wa Watanzania kuwa, Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (United Nations Environment Programme-UNEP) imetangaza nafasi 5 za ajira zifuatazo:-
  1. Senior Administrative Officer;
  2. Senior Programme Management Officer;
  3. Chief of Section;
  4. Human Resource and Management;
  5. Deputy Chief Officer.


Wizara inawahimiza Watanzania wenye vigezo na sifa stahiki kuomba nafasi hizi. Kupata taarifa zaidi na taratibu za kuomba nafasi hizo tafadhali bofya HAPA


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika 

Mashariki

Dodoma, Tanzania.

30 Agosti 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MKUTANO KUHUSU KUIMARISHA AMANI NA UTULIVU BARANI AFRIKA – TICAD7 YOKOHAMA JAPAN


Tanzania imetoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa na Japan kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwenye changamoto mbalimbalii ambazo bado zinajitokeza kwenye baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo ugaidi wa kimataifa, uhalifu, mabadiliko ya tabianchi, ukame, njaa na magonjwa sambamba na kujitolea kuchangia na kuwekeza kwenye miradi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha mazingira yaliyoharibiwa kutokana na uwepo wa kambi za Wakimbizi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Rai hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu kuimarisha amani na usalama barani Afrika uliofanyika wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliomalizika leo tarehe 30 Agosti 2019 jijiji Yokohama, Japan.

Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa, miradi hiyo ambayo ni pamoja na kubadilishana teknolojia hususan kwenye maeneo ya mipakani na mifumo ya kutoa taarifa mapema kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza itasaidia kuboresha mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na wakimbizi na watu wanaotafuta makazi.

“Uwepo wa wakimbizi na watu wanaotafuta makazi kwa namna moja au nyingine huathiri mazingira, jamii usalama na uchumi wan chi inayowapokea. Hivyo ni ombi letu kwenu kushirikiana nasi kwenye miradi mbalimbali katika kuboresha mazingira” alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Aliongeza kusema kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imekuwa kimbilio kwa wakimbizi kutoka nchi jirani wanaokimbia nchi zao kutokana na migogoro ya kisisasa, kikabila na kuibuka kwa vikundi vya uasi. Alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 1 Agosti 2019, Tanzania inahifadhi wakimbizi wapatao 305,983.

Vilevile, Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, katika kuhakikisha amani inapatikana pote dunaiani, Tanzania ina mchango mkubwa katika amani, utulivu na utatuzi wa migogoro barani Afrika na kwamba ni miongoni mwa nchi zinazochangia misheni za ulinzi wa amani katika nchini mbalimbali Afrika na duniani. 


Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu amefanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Bw. Fillipo Grandi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika.

Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Waziri Mkuu na Bw. Grandi wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usalama kwenye makambi ya wakimbizi, kuimarisha mipaka pamoja na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na Wakimbizi.

Akizungumzia Mkutano wa Saba wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwa siku tatu jijini Yokohama, Japan. Mhe. Waziri Mkuu amesema Mkutano huo umemalizika kwa mafanikio huku Wakuu wa Nchi a Serikali wakikubaliana kuteleleza Azimio la Yokohama linalolenga kuleta mapinduzi barani Afrika kwa kuimarisha  masuala ya usalama, elimu, sayansi na teknolojia na kukuza sekta binafsi.

Amesema kuwa, Tanzania itajipanga kikamilifu kutekeleza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ambayo ni ya manufaa makubwa kwa nchi za Afrika.
Mhe. Waziri Mkuu alieleza kuwa, maazimio hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamegusa sekta zote muhimu zikiwemo afya, elimu, maendeleo ya miundombinu, sayansi na teknolojia na amani na usalama yanalenga kuzikwamua kiuchumi nchi za Afrika kupitia ushirikiano  na Serikali ya Japan.

“Tumemaliza kikao cha TICAD leo ambacho kimejadili mambo mengi yakiwemo ya usalama, maendeleo ya elimu, sayansi na teknolojia na namna nzuri ya kuendesha nchi zetu kupitia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu. Kikao hiki kwetu Tanzania ni chachu ya kuendeleza jitihada zetu za kufikia uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025”  alifafanua Waziri Mkuu. 

Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa, Japan imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika kupitia fursa ya mikopo na ufadhili. Aliongeza kuwa, Tanzania itajipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kuandaa maandiko mazuri ya miradi ya kipaumbele ili kupata fedha hizo.

Amesema kuwa, nchi za Afrika ambazo kwa kiasi kikubwa zimejaliwa kuwa na maliasili na malighafi za kutosha kwa ajili ya kujenga uchumi, zimesisitizwa kuimarisha mahusiano na sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa nchi hizo. 


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan
30 Agosti 2019

WAZIRI MKUU MHE MAJALIWA AKUTANA NA KAMISHNA MKUU WA UNHCR

  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa akiwa katika mzungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi. Mazungumzo hayo yamefanyika kando na mkutano wa TICAD7 Yokohoma,Japan.

  Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania yakiendelea. Yokohama, Japan.

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudiakifuatilia mazungumzo kati ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi(hayupo pichani) Yokohama, Japan.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mb) Mhe. Kassim M. Majaliwa akiagana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania. Mazungumzo hayo yamefanyika Yokohama, Japan

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudia kisalimiana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandimara baada ya kumaliza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.

   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (Mb) Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika mazungumzo ya Waziri Mkuu mhe. Kassim M. Majaliwa. Yokohama, Japan.

Thursday, August 29, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE, MHE. PROF. PALAMAGAMBA JOHN KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA MEYA WA JIJI LA NAGAI NCHINI JAPAN


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa kwenye mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan, Mhe. Shigeharu Uchiya. Mazungumzo yao yalihusu Jiji hilo kuwa kambi ya maandalizi ya wanamichezo watakaoshiriki Michezo ya Olyimpic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020 wakiwemo kutoka Tanzania. Mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Kabudi na Mhe. Uchiya yalifanyika tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika unaoendelea jijini hapo.
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Kabudi na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya (hawapo pichani). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi Amina Shaaban, akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Japan, Bw. John Kambona na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Bertha Makilagi
Meya wa Jiji la Nagai, Bw. Shigeharu Uchiya akimweleza jambo Mhe. Prof. Kabudi wakati wa mazungumzo kati yao
Ujumbe uliongozana na Meya wa jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya ukifuatilia mazungumzo.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo
Mhe. Prof. Kabudi akimwonesha Mhe. Uchiya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini
Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Mhe. Shigeharu Uchiya mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao
Mhe. Prof. Kabudi akisalimiana na mmoja wa raia wa Japan aliyewahi kufanya kazi za kujitoleak kwenye sekta ya afya nchini Tanzania miaka ya 1960.

=============================================================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi afanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuishirikisha Tanzania kikamilifu kwenye maandalizi ya Michezo ya Olympic inayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake kutoka Tanzania.

Mhe.Prof. Kabudi ametoa shukrani hizo wakati wa mkutano wake na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya uliofanyika leo tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika (TICAD 7).

Mhe. Prof. Kabudi alisema kuwa, anaishukuru Japan kwa kuwa imeonesha nia ya dhati ya kuifanya Tanzania ishiriki kwenye Michezo hiyo muhimu ya Olympic ambayo itafanyika nchini humo mwaka 2020 na kuzishirikisha nchi zote duniani. Mhe. Waziri alifafanua kuwa tayari Serikali hiyo imesaini Hati ya Makubaliano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwezi Julai 2019 kuhusu ushiriki wa Tanzania kwenye michezo hiyo pamoja na kufanikisha ziara ya Timu ya wanariadha kutoka nchini wakiongozwa na mkimbiaji wa mbio za marathon mstaafu, Bw. Juma Ikangaa iliyofanyika mwezi Oktoba 2018. Pia Japan imeahidi kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake yatakayotolewa jijini Nagai.

 “Ushikiano wa kirafiki kati ya Japan na Tanzania ni wa miaka mingi  hususan kwenye medani za siasa, uchumi na diplomasia. Umefika wakati sasa nchi hizi mbili zishirikiane katika masuala ya kijamii na utamaduni ili kuwaunganisha mtu mmoja mmoja na kwamba ushirikiano huo ndio muhimu kwa ukuaji wa Taifa lolote” alisema Prof. Kabudi.

Aidha, alieleza kufurahishwa na ahadi kuwa Japan itatoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake ili kuwajengea uwezo kwenye michezo mbalimbali ikiwemo ile ya Olympic itakayofanyika Tokyo mwaka 2020. “Tumepokea kwa furaha taarifa kwamba Nagai itatoa mafunzo kwa wanamichezo wetu wanawake. Hii itawajengea uwezo mkubwa wanamichezo hao wakati wakijiandaa na mashindano ya Olympic” alisisitiza Prof. Kabudi.

Kadhalika, Mhe. Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kumweleza Mhe. Uchiya kuwa Serikali ya Tanzania imehamishia shughuli zake jijini Dodoma ambako ni Makao Makuu ya nchi na kwamba ipo tayari kuanzisha ushirikiano wa kidada kati ya Jiji la Dodoma na Jiji la Nagai.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya alisema kwamba jiji hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania na tayari limeanzisha program ya kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya michezo ambapo Mtanzania, Bw. Bahati Rogers ni miongoni mwa vijana wanaoshiriki program hiyo jijini humo. Pia alisema kuwa aliongoza ujumbe wa watu ishirini kutembelea Tanzania mwaka 2017 kwa ajili ya kubadilisha uzoefu kuhusu michezo.

Serikali ya Japan ambayo imeanza maandalizi ya Michezo ya Kimataifa ya Olympic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020, imetenga Jiji la Nagai kuwa kituo cha Wanamichezo wote wa Tanzania kitakachotumika kuwaadaa kabla ya kuanza kushiriki michezo hiyo rasmi. Maandalizi hayo ni pamoja na kuwawezesha wanamichezo kuzoea hali ya hewa, tamaduni, chakula na masuala mengine muhimu kuhusu Japan kabla ya ushiriki wao rasmi wa michezo hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasil
iano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Yokohama, Japan
29 Agosti 2019

Wednesday, August 28, 2019

JAPAN YATOA DOLA BILIONI 20 KUSAIDIA MAENDELEO KWA NCHI ZA AFRIKA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAPAN YATOA DOLA BILIONI 20 KUSAIDIA MAENDELEO KWA NCHI ZA AFRIKA

Japan imetangaza kutenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa Nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha Nchi hizo kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi katika Bara la Afrika huku Tanzania ikikazia mkakati wake wa uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe ameyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo Internatinaol Conference on African Development TICAD7) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Pacifico jijini Yokohama na kuongeza kuwa Serikali ya Japan itaendelea kuchangia maendeleo ya Bara la Afrika kupitia program mbalimbali za ushirikiano kwa kuimarisha rasilimali watu, elimu ya awali kwa watoto na kuboresha huduma ya afya kwa wote.

Mhe. Abe amesema kuwa, kupitia Mpango wa TICAD, ushirikiano kati ya Japan na Afrika umeimarika na kwamba nchi hiyo itaendelea kuhakikisha inahamasisha Kampuni za Japan kuwekeza Afrika ambapo hadi sasa sekta binafsi ya Japan imewekeza dola za marekani bilioni 20 katika nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumzia program mbalimbali zinazotekelezwa na Japan katika kuchangia maendeleo ya Afrika ikiwemo ile ya ABE-African Businness Education Initiative, Waziri Mkuu huyo amesema kuwa tayari vijana zaidi ya 350 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanafanya mafunzo kwa vitendo kwenye Kampuni mbalimbali kupitia mpango huo na wengine 3000 ambao walishapitia mpango huo kama wawezeshaji.

Mhe. Abe amesema kuwa, Japan itaendelea kuchangia kwenye sekta ya afya hususan kwenye masuala ya dawa, lishe na kutoa mafunzo ya ujuzi kuhusu masuala hayo kwa nchi mbalimbali za Afrika. Pia Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Afrika kwenye ujenzi wa miundombinu kama barabara na bandari pamoja kutoa wataalam kwani nchi yake haijawahi kupungukiwa wataalam.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye anahudhuria mkutano huo akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi za Afrika zinazozalisha malighafi zinazosafirishwa nje kwa ajili ya kuongezewa thamani jambo linalofanya Bara la Afrika Tanzania ikiwemo kujikuta ikisafirisha ajira na kutengeneza soko la bidhaa kutoka katika mataifa mengine na kwamba sasa Tanzania imedhamiria kupitia viwanda kutumia malighafi zake kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wake lakini pia kuuza nje ya nchi na kuzalisha fedha za kigeni.
Ameongeza kuwa kupitia mkakati wa Japan kwa nchi za Afrika Tanzania ni mojawapo ya nchi zitakazonufaika na mkakati huo na kuongeza kuwa mojawapo ya maeneo ya kuboresha ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda ni kujenga miundo mbinu imara itakayoweka msingi wa kufikia malengo hayo kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa pamoja na malighafi zitakazotumika katika viwanda.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema tofauti na mikutano iliyotangulia Mkutano huu wa TICAD saba kwa mara ya kwanza umeweka fursa ya kuwa na mpango kazi wa Yokohama ambapo badala ya kuwa na maazimio pekee sasa kutakuwa na fursa ya kuweka malengo vilevile kupima utekelezaji wake na upatikanaji wa fedha.

Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah el-Sisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa TICAD 7, Mhe. El-Sisi amesema kuwa Afrika kwa sasa inahitaji mapinduzi katika teknolojia na uvumbuzi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinalolikabili Bara hilo ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na mabadiliko ya tabia. Aidha, ametoa rai kwa nchi zinalizoendelea kutekeleza ahadi zao pamoja na Mkataba wa Paris kuhusu kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mhe. Rais El-Sisi alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji kutoka Japan kuwekeza Afrika pamoja na kuzitaka taasisi za kifedha za kimataifa kutoa masharti nafuu ya mikopo ili kukuza na kuimarisha uwekezaji na biashara barani Afrika.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guteres ameipongeza Japan kwa ushirikiano wake na nchi za Afrika hususan katika kuunga mkono jitihada mbalimbali za kudumisha amani na usalama baranii humo. Pia amezipongeza nchi za Afrika kwa kuanzisha Mpango wa Eneo Huru la Biashara barani humo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya biashara na uwekezaji na kuchangia maendeleo ya nchi hizo. Mhe. Guteres amesisistiza kuwa nchi za Afrika kwa kushirikiana na Japan ziwekeze kwenye elimu bora kwa vijana hususan kwenye maeneo ya sayansi, hesabu na teknolojia kwani yana mchango mkubwa katika maendeleo. 

Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Guteres amesema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaziathiri nchi za Afrika. Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa ameitisha Mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika jijini New York, Marekani mwezi Septemba 2019 ili kwa pamoja nchi zijadili namna ya kuendelea kutatua changamoto hizo.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Moussa Faki Mahamat ambao hushirikiana na Japan kuandaa mikutano ya TICAD, amesema kuwa, Mkutano wa Saba umekuja na suluhisho kwa vijana kuhusu masuala ya teknolojia na uvumbuzi na kusisistiza kwamba suala hilo ni la kipaumbele kwa nchi za Afrika.

Mkutano wa Saba wa TICAD ambao umebeba kaulimbiu ya Kuiendeleza Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi, umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 4,000 pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 44 za Afrika.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan.
28 Agosti 2019

WAZIRI MKUU ASHIRIKI TICAD7- YOKOHOMA,JAPAN

Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb) akiwa kaaika Mkutano wa Kimataifa Tokyo kuhusu Maendeleo kwa Bara la Afrika. Nyuma yake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb). Mkutano huo unafanyika Yokohama,Japan.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akisaliqmiana na Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth walipokutana na kufanya mazungumzo katika Mji wa Yokohoma Japan.


Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akisikiliza jambo kutoka kwa Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth. Viongozi wote wawili walikutana na kufanya mazungumzo ya namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia baina ya Nchi hizo. wote wapo katika Mji wa Yokohoma,Japan kushiriki mkutano wa TICAD7.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akiwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth walipokutana na kufanya mazungumzo katika mji wa Yokohoma Japan. Kushoto kwa Mhe. Majaliwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi (Mb).

MHE. WAZIRI MKUU ATEMBELEA BANDA LA TANZANIA LA MAONESHO YA TICAD 7

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana akiangalia mojawapo ya bidhaa nchini Japan alipotembelea banda la maonesho ya vivutio vya utalii wa Tanzania jijini Yokohama, Japan tarehe 28 Agosti 2019.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Bi. Edda Magembe, Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Japan alipotembelea banda la maonesho ya vivutio vya utalii wa Tanzania jijini Yokohama, Japan tarehe 28 Agosti 2019. Mhe. Waziri Mkuu yupo nchini Japan akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Maonesho hayo yanaenda sambamba na mkutano huo ambao umetoa fursa kwa nchi za Afrika kujitangaza kwenye masuala ya vivutio vya utalii, uwekezaji na biashara.
Mhe. Waziri Mkuu akisalimiana na mmoja wa washiriki kwenye banda la maonesho la Tanzania. Maonesho hayo yanafanyika sambamba na Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7)

Mhe. Waziri Mkuu akiangalia moja ya kipeperushi kuhusu maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini alipotembelea banda la Tanzania kwenye Mkutano wa TICAD 7 unaofanyika jijini Yokohama, Japan
Mhe. Waziri Mkuu kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa maonesho kwenye banda la Tanzania yanayoendelea sambamba na Mkutano wa Saba wa TICAD

Tuesday, August 27, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA JAPAN AWAANDALIA HAFLA MAALUM MAWAZIRI WANAOSHIRIKI MKUTANO WA SABA WA TICAD

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe.  Kono Taro akimkaribisha  Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi alipowasili kwenye Hoteli ya Royal Palace iliyopo jijini Yokohama kwa ajili ya kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Taro kwa heshima ya Mawaziri wanaoshiriki Mkutano wa  Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) unaofanyika nchini humo kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.
Mhe. Taro akizungumza wakati wa hafla hiyo ambapo ameendelea kuwahakikishia  ushirikiano Mawaziri kutoka Afrika 
Mhe. Taro akizungumza huku Mawaziri wakimsikiliza
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika meza moja na Mhe. Taro na Mawaziri wengine kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa TICAD
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa na Waziri mwenzake wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan kwa heshima ya Mawaziri kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa TICAD
Picha ya pamoja ya Mhe. Taro na Mawaziri kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) utakaofanyika Yokohama, Japan kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisalimiana na Mawaziri wenzake akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor (kulia) mara baada ya kumalizika kwa hafla maalum iliyoandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Taro.