Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa anaingia katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Tokyo,Japan. August 26,2019. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika moja ya Maktaba ya vitabu iliyopo katika Ubalozi wa Tanzania - Tokyo,Japan. August 26,2019. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akikagua aina ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Ubalozi wa Tanzania Nchini Japan. August,26,2019. |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika ofisi ya Balozi wa Tanzania Nchini Japan. August 26,2019. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO WA SABA WA TOKYO KUHUSU
MAENDELEO YA AFRIKA (TICAD 7)
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John
Kabudi amewasili jijini Yokohama, Japan tarehe 26 Agosti kwa ajili ya kushiriki
Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International
Conference on African Development-TICAD 7) utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi
30 Agosti 2019.
Mkutano
huu wa Saba utatanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Makatibu
Wakuu na Mabalozi tarehe 25 na 26 Agosti 2019 ukifuatiwa na kikao cha Mawaziri
tarehe 27 Agosti, 2019 na utahitimiswa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali
tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019. Kauli mbiu ya Mkutano huu ni “Kuendeleza
Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi”.
Mkutano
wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano
na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi
cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.
Agenda
za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha
mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na
ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha
amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na
agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa
Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu
Mabadiliko ya Hali ya Hewa.
Kutokana
na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, Mkutano
wa TICAD 7 umeandaa ratiba maalum itakayozishirikisha taasisi binafsi na za umma
kwenye majadiliano ya kibiashara yatakayofanyika tarehe 29 Agosti 2019. Lengo
la majadiliano hayo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa
Serikali wamiliki wa Kampuni, wafanyabiashara na wawekezaji ili kujadili kwa
pamoja masuala mbalimbali ya kukuza baishara, uwekezaji na utalii kati ya Japan
na Afrika.
Kadhalika wakati wa mkutano wa saba nchi zote za Afrika zimepatiwa nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa lengo la
kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na vivutio vya utalii za nchi husika. Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB) imejipanga kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini wakati wa mkutano huo.
Mkutano
wa Saba wa TICAD utahitimishwa kwa Wakuu wa Nchi kupitisha Azimio la Yokohama
na Mpango Kazi wa utekelezaji wa Azimio hilo. Serikali ya Japan ilianzisha jukwaa
la majadiliano kati yake na nchi za Afrika mwaka 1993 kwa ajili ya kujadili
maendeleo na nchi hizo.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ataongoza
ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama,
Japan.
26 Agosti 2019
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.