Meya wa Jiji la Nagai, Bw. Shigeharu Uchiya akimweleza jambo Mhe. Prof. Kabudi wakati wa mazungumzo kati yao |
Ujumbe uliongozana na Meya wa jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya ukifuatilia mazungumzo. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mazungumzo |
Mhe. Prof. Kabudi akimwonesha Mhe. Uchiya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini |
Mhe. Prof. Kabudi akiagana na Mhe. Shigeharu Uchiya mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Prof. Kabudi afanya
mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya Japan kwa
kuishirikisha Tanzania kikamilifu kwenye maandalizi ya Michezo ya Olympic
inayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kutoa
mafunzo kwa wanamichezo wanawake kutoka Tanzania.
Mhe.Prof. Kabudi ametoa shukrani hizo wakati wa
mkutano wake na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya uliofanyika leo
tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa
Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika (TICAD 7).
Mhe. Prof. Kabudi alisema kuwa, anaishukuru Japan kwa
kuwa imeonesha nia ya dhati ya kuifanya Tanzania ishiriki kwenye Michezo hiyo
muhimu ya Olympic ambayo itafanyika nchini humo mwaka 2020 na kuzishirikisha nchi zote duniani. Mhe. Waziri alifafanua kuwa tayari Serikali hiyo imesaini Hati
ya Makubaliano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwezi Julai 2019
kuhusu ushiriki wa Tanzania kwenye michezo hiyo pamoja na kufanikisha ziara ya Timu
ya wanariadha kutoka nchini wakiongozwa na mkimbiaji wa mbio za marathon
mstaafu, Bw. Juma Ikangaa iliyofanyika mwezi Oktoba 2018. Pia Japan imeahidi
kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake yatakayotolewa jijini Nagai.
“Ushikiano wa
kirafiki kati ya Japan na Tanzania ni wa miaka mingi hususan kwenye medani za siasa, uchumi na diplomasia.
Umefika wakati sasa nchi hizi mbili zishirikiane katika masuala ya kijamii na utamaduni
ili kuwaunganisha mtu mmoja mmoja na kwamba ushirikiano huo ndio muhimu kwa
ukuaji wa Taifa lolote” alisema Prof. Kabudi.
Aidha, alieleza
kufurahishwa na ahadi kuwa Japan itatoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake ili
kuwajengea uwezo kwenye michezo mbalimbali ikiwemo ile ya Olympic
itakayofanyika Tokyo mwaka 2020. “Tumepokea kwa furaha taarifa kwamba Nagai
itatoa mafunzo kwa wanamichezo wetu wanawake. Hii itawajengea uwezo mkubwa
wanamichezo hao wakati wakijiandaa na mashindano ya Olympic” alisisitiza Prof.
Kabudi.
Kadhalika, Mhe. Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kumweleza
Mhe. Uchiya kuwa Serikali ya Tanzania imehamishia shughuli zake jijini Dodoma
ambako ni Makao Makuu ya nchi na kwamba ipo tayari kuanzisha ushirikiano wa
kidada kati ya Jiji la Dodoma na Jiji la Nagai.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu
Uchiya alisema kwamba jiji hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania
na tayari limeanzisha program ya kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya michezo
ambapo Mtanzania, Bw. Bahati Rogers ni miongoni mwa vijana wanaoshiriki program
hiyo jijini humo. Pia alisema kuwa aliongoza ujumbe wa watu ishirini kutembelea
Tanzania mwaka 2017 kwa ajili ya kubadilisha uzoefu kuhusu michezo.
Serikali ya Japan ambayo imeanza maandalizi ya Michezo
ya Kimataifa ya Olympic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020, imetenga Jiji
la Nagai kuwa kituo cha Wanamichezo wote wa Tanzania kitakachotumika kuwaadaa
kabla ya kuanza kushiriki michezo hiyo rasmi. Maandalizi hayo ni pamoja na
kuwawezesha wanamichezo kuzoea hali ya hewa, tamaduni, chakula na masuala
mengine muhimu kuhusu Japan kabla ya ushiriki wao rasmi wa michezo hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasil
iano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Yokohama,
Japan
29 Agosti 2019
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.