Tuesday, April 28, 2020

TANZANIA NA KUWAIT ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Faleh Alsehaijan alipomtembelea katika ofisi za wizara Jijini Dodoma tarehe 28 Aprili 2020.

Mazungumzo yao yalijikita katika kujadili namna bora ya kuuenzi na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia iliopo baina ya mataifa yao ili uweze kuleta tija na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Kuwait.

Vilevile wawili hao walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya utekelezezaji katika sekta ya afya, na utawala ambapo kwa pamoja wamekubaliana kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mambo yaliyokubaliwa kwa nyakati tofauti katika sekta hizo yanakamilika kwa wakati.

Tanzania na Kuwait zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya kilimo, afya, biashara, maji, pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshe katika sekta hizo kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi unafikiwa kwa wakati. 

Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Faleh Alsehaijan akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Ndumbaro ambapo pamoja na mambo mengine walipata nafasi ya kushirikishana hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mataifa yao katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona unaoikabili dunia kwa sasa.

Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ayoub Mndeme na Msaidizi wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Charles Faini wakifatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.


Thursday, April 23, 2020

MUONGOZO WA USAFIRISHAJI BIDHAA KATIKA NCHI ZA SADC

 MWONGOZO WA USAFIRISHAJI WA BIDHAA MUHIMU NA HUDUMA KATIKA NCHI ZA SADC KWA KIPINDI HIKI CHA JANGA LA VIRUSI  VYA CORONA (COVID – 19)

23 APRILI, 2020, DODOMA

Tarehe 6 Aprili, 2020 ulifanyika Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo ulijadili janga la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona. Mkutano huo ulihusisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Fedha,Viwanda,Biashara, Utalii, Mambo ya Ndani na Uchukuzi, kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ambazo ni Angola, Botswana, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Ushelisheli, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.

Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri lilitoa mwongozo kuhusu Usafirishaji wa Bidhaa Muhimu na Huduma Katika Nchi za SADC katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Corona. Mwongozo huu utatumika katika kipindi hiki unalenga kupunguza safari zisizo za lazima na usafirishaji wa bidhaa ambazo ni za muhimu tu na unazitaka Nchi Wanachama kuzingatia na kutekeleza sera na miongozo mbalimbali iliyotolewa na inayoendelea kutolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Forodha Duniani (WCO), Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Usafiri wa Maji Duniani (IMO).

Kwa mujibu wa Muongozo huo Malori na magari yatakayoruhusiwa kusafirisha mizigo ni yale yatakayobeba bidhaa za Vyakula; Vifaa tiba na Dawa, vifaa binafsi vya kujikinga; Mafuta na makaa ya mawe; Pembejeo za kilimo; vifungashio, vipuri vya magari na mashine. 

Raia wanaorejea katika nchi zao wanatakiwa kuzingatia sheria za nchi zilizowekwa za kupimwa na ikiwa atagundulika mgonjwa mwenye Virusi vya Corona, atatakiwa kutengwa kwa kuwekwa kizuizini kwa muda uliowekwa; Kupunguza idadi ya wasafiri katika mabasi na vyombo vingine vya usafiri; Kutumia miongozo ya WHO ya usafi katika vyombo vya usafiri, vituo vya mabasi na maeneo mengine ambayo mabasi yatasimama; Madereva/waendeshaji kutoa taarifa mbalimbali kuhusu njia za kupambana na COVID-19 kwa wasafiri katika lugha za wasafiri na; Kujaza fomu zinazohoji maeneo waliopita wasafiri na kuhakikisha fomu hizo zinawasilishwa kwa kituo cha maafisa afya.

Vyama vya wasafirishaji vinatakiwa Kushirikiana na maafisa afya kuandaa na kutekeleza programu ya uhamasishaji kwa wasafirishaji magari na waajiri wake;Kuwaelekeza madereva wa malori kujaza fomu maalum zinazoonyesha maeneo ambayo watapita, maeneo watakayosimama wakati wa safari na kituo cha mwisho cha safari ambazo zitawekwa katika ofisi za maafisa afya zilizopo mipakani ili kuweza kuwasiliana na kufuatilia madereva kwa uchunguzi;

Wasafirishaji magari wanatakiwa kushirikiana na Serikali kuangalia jinsi taarifa za gari zinavyoweza kutumika wakati wa kuifuatilia; Kuhakikisha madereva wanaovuka mipaka wanabeba sabuni na maji ya kunawa; Kuwaelekeza madereva kutobeba watu wasiohusika katika magari yao; Kuelekeza madereva wa malori kuzingatia umbali wa mita moja kati yao wakati wa safari; na; Kugawa vifaa maalum kwa wafanyakazi na waajiriwa ambao wapo katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi. 

Madereva wa malori watalazimika kuweka bayana kituo cha mwisho cha safari yao na wanaaswa kusimama katika vituo maalum vilivyopangwa na endapo dereva au wahudumu wa chombo husika wataonesha dalili za kuugua COVID-19 lori hilo litalazimika kupitia hatua za usafishaji kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari, watoa huduma wa chombo hicho watengwa katika eneo maalum (Quarantine) au kupelekwa kituo cha matibabu kwa gharama zao; Mmiliki wa lori atalazimika kuandaa dereva na watoa huduma wengine ili kuwezesha bidhaa kufika mahali zilipokusudiwa.

Dereva na wasaidizi wake wakishusha mzigo watapaswa kukaa watengwa katika eneo maalum ( Quarantine) kwa siku 14 na kutofanya safari nyingine ya nje katika kipindi hicho na wataalamu wa afya waliopo mpakani mwa nchi husika watalazimika kuwasiliana kwa kina na wataalamu wa afya wa nchi mwenyeji wa lori husika ili kupata taarifa zitakazo saidia kuchukua hatua ya kuwatenga katika eneo maalum dereva na wasaidizi wake wakati wa kushusha au kupakia mzigo.

Vyombo vya usafiri wa majini kutoka nchi ambazo zipo hatarini zaidi katika maambukizi au zenye wasaidizi au abiria waliopo kwenye hali hatarishi zaidi ya maambukizi watalazimika kutengwa katika eneo maalum kwa siku 14 kwa gharama zao kabla ya kuruhusiwa kutoka eneo ambalo chombo hicho kilitia nanga na chombo kilichobeba abiria na wasaidizi walioathirika na COVID-19 hakitaruhusiwa kutia nanga. 

Ndege zinazofanya safari katika maeneo mbalimbali zitalazimika kufuata hatua zote za usafishaji kwa kupuliziwa dawa na hatua zingine za kujikinga ambazo kila ndege iliyobeba abiria walioathirika au washukiwa wa COVID 19 inapaswa kuzipitia.

SADC ilikubaliana kuwa hakutakuwa na zuio dhidi ya wasafirishaji wa nje waliosajiliwa la kuingia nchi mwanachama endapo wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sera za usalama za nchi husika. 


Imetolewa na:

 Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali 
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 


Wednesday, April 8, 2020

TAARIFA KWA UMMASADC YAAZIMIA USAFIRISHAJI WA BIDHAA MUHIMU KUDHIBITI COVID - 19


Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), ambaye pia  ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Prof. Palamagamba John Kabudi Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu maazimio ya Mkutano wa dharura wa Jumuiya hiyo kuhusu Covid-19 kwa Nchi za SADC uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania
Mwenyekiti wa Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa  Jumuiya ya Nchi za Kusini  Mwa Afrika(SADC)  ambaye pia  ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Kanali.Wilbert Ibuge.


MAAZIMIO YA MKUTANO WA DHARURA KUHUSU COVID - 19 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), limeridhia usafirishaji wa bidhaa muhimu katika ukanda  huo wakati wa janga la homa ya mapafu (Covid-19) ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa nchi wanachama.


Akizungumza katika Mkutano wa dharura wa SADC, kuhusu Covid-19,  uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Prof.Palamagamba John  kabudi amesema Baraza limepitisha mapendekezo ya Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya uliofanyika Machi 9, 2020, Dar es Salaam, Tanzania.

“Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya wa tarehe 9, Machi 2020, ulitoa mapendekezo ambayo yamefanyiwa kazi na Mkutano wa Baraza la Mawaziri yakiwa ni   ufuatiliaji na utekelezaji masuala ya afya kuhusu mlipuko wa Covid-19, kujadili namna ya kujiandaa na kukabiliana na virusi vya Covid -19,kubaini wagonjwa na kufuatilia waliokutana nao na huduma za tiba katika ukanda wetu” Alisema Prof. Kabudi.

Ameongeza kuwa masuala mengine ni uchunguzi na upimaji wa kimaabara, uzuiaji na udhibiti wa maambukizi, uelimishaji wa madhara na ushirikishwaji wa jamii, uratibu wa kikanda wa kukabiliana na Covid-19, uwezeshaji na usafirishaji wa bidhaa muhimu katika ukanda huo wa SADC wakati huu wa Covid-19.

Mengine yaliyopitishwa ni Covid-19 na uwezeshaji wa biashara, Covid-19 na masuala ya udhibiti biashara na usimamizi wa majanga hatarishi katika ukanda huo wa Nchi za Kusini mwa Afrika, mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba  Covid-19 imeendelea kusambaa  duniani kwa hiyo Jumuiya imeona iweke mikakati madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo.

“Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri SADC uliitishwa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi na vifo katika baadhi ya nchi Duniani, kwa mujibu wa taarifa namba 76 ya Shirika la Afya Duniani(WHO), ya April 5, 2020 inaeleza kuwa takribani watu 1,133,759 wameambukizwa ugonjwa huo na kati ya hao matukio mapya ni 82,061 na vifo 62,784 huku Afrika kwa nchi 51 kuna wagonjwa 9,198 na vifo viko chini ya watu 500, lakini kwa ukanda wetu wa SADC kuna matukio 2,127 katika nchi 14 huku vifo vikiwa 38” Alisema Prof.Kabudi.

Aidha, Prof. Kabudi ameeleza kuwa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri uliofanyika sambamba na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa SADC ulilenga katika kupokea taarifa ya wataalamu pamoja na muongozo wa urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma katika nchi za SADC wakati huu wa mlipuko wa Covid-19.

Bidhaa zilizopitishwa kwenye muongozo ni pamoja na usafirishaji wa vyakula, vifaa tiba, Dawa na vifaa vya kujinga na Corona, mafuta na mkaa wa mawe, pembejeo za kilimo na madawa, vifungashio, bidhaa zote zinazotumika katika utengenezaji, uchakataji na uhifadhi wa vyakula na vifaa ambavyo vinahusu usalama na dharura kwenye majanga mbalimbali.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa SADC wamefanya hivyo ili kuzuia kuenea kwa Covid-19  na kuwezesha utekelezaji  mikakati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa huo na kuwezesha upatikana wa bidhaa muhimu ili kuzuia usafirishaji usio wa lazima kwa abiria katika ukanda huo wa Afrika .

MKUTAO WA DHARURA WA SADC KUHUSU COVID - 19 WAFANYIKA DAR ES SALAAM KWA NJIA YA MTANDAO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali. Wilbert Ibuge akiendesha Mkutano wa dharura kwa njia ya video ambao unawahusisha Maafisa Waandamizi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhusu mwenendo ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19), mkutano ambao umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania. Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa dharura kwa njia ya video ambao unawahusisha Maafisa Waandamizi Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhusu mwenendo ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19), mkutano ambao umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali. Wilbert Ibuge akiendesha Mkutano wa dharura kwa njia ya video ambao unawahusisha Maafisa Waandamizi Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhusu mwenendo ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19), mkutano ambao umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania, wengine ni Makatibu Wakuu na Maafisa kutoka Wizara mbalimbali.


Mkutano wa dharura kwa njia ya video ambao unawahusisha Maafisa Waandamizi Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhusu mwenendo ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19), ukiendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Tanzania

Wednesday, April 1, 2020

KAMPUNI YA JAPAN YASAIDIA TAASISI YA MIFUPA (MOI) MSAADA WA VIFAA TIBA VYA MILIONI 80.9


Kampuni ya EAA Co. Ltd ya nchini Japan bandia imetoa msaada wa viungo bandia vyenye thamani ya Shilingi milioni 80.9 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) leo Jijini Dar es Salaam.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi wa Tiba (MOI) Dkt. Samwel Swai amesema kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa matibabu ya wagonjwa wenye ulemavu wa miguu naa mikono. 

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya EAA Co. Ltd, Josiah Benedict amesema wameguswa na changamoto zinazowakabili watanzania ndiyo maana wameamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Msaada huo unatokana na juhudi za Ubalozi wa Tanzania Japan kwa kushirikiana na Watanzania waishio nchini Japan.


Mkurugenzi wa Tiba (MOI) Dkt. Samwel Swai (kulia) akipokea baadhi ya vifaa kutoka kwa Meneja wa Kampuni ya EAA, Josiah Benedict leo katika viwanja vya (MOI) jijini Dar es Salaam  

Mkurugenzi wa Tiba (MOI) Dkt. Samwel Swai (kulia) akipokea baadhi ya vifaa kutoka kwa Meneja wa Kampuni ya EAA Josiah Benedict leo katika viwanja vya (MOI) jijini Dar es Salaam  

Mkurugenzi wa Tiba (MOI) Dkt. Samwel Swai akiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Kampuni ya EAA, Josiah Benedict pamoja na baadhi ya wafanyakazi wengine waliohudhuria warsha ya makabidhiano leo katika viwanja vya (MOI) jijini Dar es Salaam