Akizungumza katika Mkutano wa dharura wa SADC, kuhusu Covid-19, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Prof.Palamagamba John kabudi amesema Baraza limepitisha mapendekezo ya Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya uliofanyika Machi 9, 2020, Dar es Salaam, Tanzania.
“Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya wa tarehe 9, Machi 2020, ulitoa mapendekezo ambayo yamefanyiwa kazi na Mkutano wa Baraza la Mawaziri yakiwa ni ufuatiliaji na utekelezaji masuala ya afya kuhusu mlipuko wa Covid-19, kujadili namna ya kujiandaa na kukabiliana na virusi vya Covid -19,kubaini wagonjwa na kufuatilia waliokutana nao na huduma za tiba katika ukanda wetu” Alisema Prof. Kabudi.
Ameongeza kuwa masuala mengine ni uchunguzi na upimaji wa kimaabara, uzuiaji na udhibiti wa maambukizi, uelimishaji wa madhara na ushirikishwaji wa jamii, uratibu wa kikanda wa kukabiliana na Covid-19, uwezeshaji na usafirishaji wa bidhaa muhimu katika ukanda huo wa SADC wakati huu wa Covid-19.
Mengine yaliyopitishwa ni Covid-19 na uwezeshaji wa biashara, Covid-19 na masuala ya udhibiti biashara na usimamizi wa majanga hatarishi katika ukanda huo wa Nchi za Kusini mwa Afrika, mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba Covid-19 imeendelea kusambaa duniani kwa hiyo Jumuiya imeona iweke mikakati madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo.
“Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri SADC uliitishwa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi na vifo katika baadhi ya nchi Duniani, kwa mujibu wa taarifa namba 76 ya Shirika la Afya Duniani(WHO), ya April 5, 2020 inaeleza kuwa takribani watu 1,133,759 wameambukizwa ugonjwa huo na kati ya hao matukio mapya ni 82,061 na vifo 62,784 huku Afrika kwa nchi 51 kuna wagonjwa 9,198 na vifo viko chini ya watu 500, lakini kwa ukanda wetu wa SADC kuna matukio 2,127 katika nchi 14 huku vifo vikiwa 38” Alisema Prof.Kabudi.
Aidha, Prof. Kabudi ameeleza kuwa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri uliofanyika sambamba na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa SADC ulilenga katika kupokea taarifa ya wataalamu pamoja na muongozo wa urazinishaji (harmonization) na uwezeshaji usafirishaji wa bidhaa muhimu na huduma katika nchi za SADC wakati huu wa mlipuko wa Covid-19.
Bidhaa zilizopitishwa kwenye muongozo ni pamoja na usafirishaji wa vyakula, vifaa tiba, Dawa na vifaa vya kujinga na Corona, mafuta na mkaa wa mawe, pembejeo za kilimo na madawa, vifungashio, bidhaa zote zinazotumika katika utengenezaji, uchakataji na uhifadhi wa vyakula na vifaa ambavyo vinahusu usalama na dharura kwenye majanga mbalimbali.
Prof. Kabudi aliongeza kuwa SADC wamefanya hivyo ili kuzuia kuenea kwa Covid-19 na kuwezesha utekelezaji mikakati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa huo na kuwezesha upatikana wa bidhaa muhimu ili kuzuia usafirishaji usio wa lazima kwa abiria katika ukanda huo wa Afrika .
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.