Saturday, May 29, 2021

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI TANZANIA JENERALI VENANCE MABEYO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA- PRETORIA

 Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, ametembelea Ubalozi wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini.


Jenerali Mabeyo yupo Nchini Afrika Kusini kuhudhuria sherehe za kumuaga Mkuu Majeshi wa Afrika Kusini Jenerali SZ Shoki zilizofanyika kitaifa Jana Mjini Pretoria. Kuhudhuria sherehe hizi,ni utaratibu uliowekwa  na nchi wanachama wa Jumuiya za SADC ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha  mashirikiano  hususan katika nyanja ya Diplomasia ya Ulinzi (Defence Diplomacy) na Amani katika eneo Ia nchi za SADC.

 

Jenerali Mabeyo, alikaribishwa Ubalozini na Mhe. Balozi Mej. Jen. Gaudence Milanzi (Mst) na watumishi wa Ubalozi Mhe. Balozi Milanzi alitoa taarifa fupi ya eneo la uwakilishi ya Afrika Kusini, Botswana na Falme ya Lesotho.

 

Mhe. Balozi alieeza kuwa hali ya uwakilishi inaridhisha kiulinzi na kiusalama, Ubalozi umeendelea kukuza mashirikiano na nchiza eneo la uwakilishi ikiwa ni pamoja na SADC. Kwa kufuata miongozo ya sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kuendeleza Diplomasia ya kisiasa na kutekeleza Diplomasia ya uchumi.

 

Upande wake Jenerali Mabeyo alielezea ziara yake kwa ujumla nchini Afrika Kusini imekuwa ni ya mafanikio, na pia kuna mambo kama ambayo kama Mkuu  wa Majeshi ameona yanafaa kuigwa ili kuboresha utendaji wa Jeshi la Tanzania.

 

Jenerali Mabeyo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya  Muungano  wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan, amelenga kuendeleza maendeleo ndani na nje ya nchi mfano katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania na mwelekeo  unaelekeza kuimarisha  Diplomasia kwa  kujenga mahusiano na nchi duniani kwa   kuimarisha Diplomasia ya siasa na Diplomasia ya uchumi.

 

Jenerali Mabeyo alimsihi Balozi na watumishi wa Ubalozi kuhakikisha kuwa wanaielewa na kuisimamia dira ya Diplomasia kama ilivyoainishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuweza kutelekeza majukumu yao kwa wepesi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi wakati alipotembelea ubalozi huo Jijini Pretoria


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akiwa kwenye kikao na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na watumishi wa Ubalozi wakati alipotembelea ubalozi huo Jijini Pretoria


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi pamoja na watumishi wa Ubalozi  



MAWAZIRI SEKTA YA BIASHARA EAC WAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VISIVYO VYA KIBIASHARA

Na mwandishi wetu, Arusha

Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki lakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kuimarisha biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo.

Awali akifungua mkutano Jijini Arusha Ijumaa, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawawezesha mawaziri kupitia na kujadili miongozo ambayo itasaidia kuboresha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara.  

Aidha, Mhandisi Mlote ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kanuni na sheria ya Afrika Mashariki, vikwazo visivyo vya kibiasha baina ya nchi na nchi vimekuwa vikizuia ukuaji wa biashara hivyo ni muhimu kupitia mkutano wa baraza la mawaziri kuangalia namna ya kuviondoa ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndani ya jumuiya.

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana mambo mengi ya msingi ikiwemo kuendelea kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi.

“Tumezungumza pia kuhusu ushiriki wetu katika kufanya biashara na Uingereza kwa kuzingatia kuwa Uingereza siyo sehemu Jumuiya ya Ulaya, lakini pia tumezungumzia suala la EAC kujiunga na jumuiya ya biashara ya Afrika ambayo sisi Tanzania tupo katika hatua kadhaa na kuona kuwa na sisi tunajiunga na jumuiya hiyo mwaka huu,” Amesema Prof. Mkumbo

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amesema kuwa mawaziri wamekubaliana kutoa msukumo wa biashara katika jumuiya ya afrika mashariki lizingatiwe na kupea kipaombele na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara katika nchi mbalimbali.

“Pamoja na mambo mengine, pi tumekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru (Non-tarrif barriers) viondolewe kwani vimekuwa vikikwamisha biashara bila sababu za msingi, na kuangalia jinsi ya kuwekeza kwenye eneo la uwekezaji ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvutia wawekezaji” amesema Mhe. Mwambe    

Miongoni mwa maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na maamuzi ya ripoti ya mawaziri wa fedha, ripoti ya kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati ya uwekezaji.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya Mhe. Betty Maina, Waziri wa Viwanda na Biashara, - Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.

Wengine ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Mhe. Beata Habyarimana, Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Mhe. Grace Choda, pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Balozi Jeremie Banigwaninzigo.

Mkutano huu ni maelekezo ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini Kenya tarehe 04 hadi 05 Mei, 2021.

Waziri wa Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo akifafanua jambo katika mkutano wa Baraza la kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki leo jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe. Kulia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban. Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya, Mhe. Betty Maina akiwasilisha hoja kwenye mkutano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI). Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote

Ujumbe wa Uganda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)

Ujumbe wa Rwanda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)

Ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)




  

NAIBU WAZIRI MBAROUK; TANZANIA ITAENDELEA KUHESHIMU NA KUTAMBUA MCHANGO WA WALINDA AMANI KOTE DUNIANI.

Tanzania inaendelea kuheshimu na kuthamini mchango na kazi kubwa inayofanywa na Walinda Amani kote duniani. Haya yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo pia aliongoza zoezi la uwekaji mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa. “lengo kuu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchangia vikosi vyake kwenye Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika maeneo yenye migogoro na wananchi wa maeneo hayo wanarejea kwenye shughuli zao za kila siku” Naibu Waziri Mbarouk.

Tanzania inashikilia nafasi ya 13 kwa wingi wa idadi ya askari miongoni mwa nchi 122 zinazochangia vikosi kwenye Umoja wa Mataifa. Kutoka nchi za Afrika, Tanzania inashikilia nafasi ya 7 kati ya nchi 35 zinazochangia vikosi vya kulinda amani. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2021, Tanzania ilikuwa na jumla ya Askari 1,481 kwenye Misheni sita za ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani. 

Aidha, Naibu Waziri Mbarouk ameeleza furaha kuona Umoja wa Mataifa (UN) umetambua mchango na umuhimu wa vijana ambao ndio hutoa mchango mkubwa katika misheni za kulinda amani. “Nafurahi kuona UN wanatambua mchango wa vijana kupitia maazimio ya Baraza la Usalama Na. 2250 (la mwaka 2015) kuhusu vijana, amani na usalama; Azimio Na. 2419 (la mwaka 2018) kuhusu kuwajumuisha vijana kwenye majadiliano na utekelezaji wa makubaliano ya amani; na Azimio Na. 2535 (la mwaka 2020) ambalo hutaja hatua za utekelezaji za ajenda ya vijana, amani na usalama kwenye maeneo ya operesheni za amani”. ameeleza Naibu Waziri Mbarouk 

Licha ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hushiriki pia katika jitihada za kuimarisha amani kwa nchi zinazotuzunguka kuupitia mitangamano ya kikanda kama vile, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akihutubia hadhira iliyojitokeza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akikagua gwaride kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiweka mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.

Friday, May 28, 2021

WAZIRI MULAMULA AHIMIZA KASI NA WELEDI KATIKA UTENDAJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mkutano na watumishi wa Wizara jijini Dodoma. Pamoja na mambo mengine mkutano huu ulilenga kutoa maelekezo kwa watumishi wa Wizara ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, pia kusikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa Watumishi ili kuzipa suluhisho la kudumu.  

Waziri Mulamula ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwahimiza watumishi wa Wizara kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kujituma ili kukidhi matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita na Watanzania kwa ujumla. “Watanzania wanamatarajio makubwa na Wizara yetu, tunajukumu kubwa la kuhakikisha tunatimiza matarajio yao hivyo ni lazima tufanye kazi kwa kujituma na weledi zaidi, pia kuacha kufanya kazi kwa mazoea” Waziri Mulamula. 

Aidha, Waziri Mulamula ameeleza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa Wizara inatafuta fursa mbalimbali za masomo ya muda mfupi na mrefu ili kuwaongezea ujuzi watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao. Sambamba na hilo, Waziri mulamula ameleza kuwa Wizara inadhamira ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili kuwaogezea hali katika utendaji. “Natambua kuwa ufanisi katika Wizara hii hauwezi kupatikana iwapo mazingira ya ufanyaji kazi sio mazuri. Kupitia kwa Katibu Mkuu, tuna dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuhakikisha upandishwaji wa vyeo unakamilika na kuhakikisha kuwa watumishi wanapata stahili zao ipasavyo na kwa wakati” Waziri Mulamula

Kwa upande wake Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara amewasisitiza Watumishi kufanya kazi kwa ubunifu na kwa umoja ili kuendelea kukuza mahusiano ya kiuchumi na mataifa, jumuiya za kikanda na taasisi nyingine za kimataifa. Balozi Sokoine ameongezea kusema ni vyema watumishi wa Wizara kuendelea kuungana na kushirikiana vyema katika kulinda uchumi na masilahi mapana ya Taifa. Vilevile kuhakikisha kuwa balozi zetu zinakuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji na upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zetu.

Waziri Mulamula na Balozi Sokoine wamekutana na Watumishi wa Wizara kwa mara ya kwanza tokea walipoteuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nyadhifa zao. Mkutano huu pia ulihusisha Ofisi za Balozi zinazoiwalikilisha Tanzania sehemu mbalimbali duniani ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao. 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Wizara. Wengine walioketi, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine (kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Alex B.D.J Mfungo (kulia)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea baina yake na Watumishi wa Wizara uliofanyika jijini Dodoma

Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia Mkutano uliokuwa ukiendelea Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula na Watumishi wa Wizara


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano
Balozi Joseph Edward Sokoine Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wakati wa Mkutano wa Waziri Mulamula na Watumishi wa Wizara

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara.

Thursday, May 27, 2021

MAWAZIRI BIASHARA, VIWANDA, FEDHA NA UWEKEZAJI KUKUTANA KESHO JIJINI ARUSHA

 Na Mwandishi wetu, Arusha

Baraza la Mawaziri la kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili wanategemea kukutana kesho tarehe 28 Mei 2021 Jijini Arusha kujadili masuala mbalimbali ya kukuza biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo. 

Mkutano huo wa Mawaziri umetanguliwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa sekta ya Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) wa Jumuiya hiyo uliofanyika leo jijini Arusha ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamepokea na kujadili ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti za baraza la kisekta la mawaziri wa fedha, ripoti ya kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati ya uwekezaji.

Mkutano wa Makatibu Wakuu wa leo tarehe 27 Mei 2021 utafuatiwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa kisekta tarehe 28 Mei 2021 jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) ngazi ya Makatibu Wakuu, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Afrika Mashariki kutoka Kenya, Dkt. Kevit Desai akiongea na wajumbe wa mkutano ulifanyanyika leo Jijini Arusha


Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Bw. Doto James akifafanua jambo katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha. Kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Prof. Godius Kahyarara na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban. 


Ujumbe wa Burundi ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha


Ujumbe wa Kenya ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) ulifanyanyika leo Jijini Arusha 


Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sekta ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji (SCTIFI) leo Jijini Arusha

Wajumbe wakifuatilia mkutano 



Wednesday, May 26, 2021

KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA SADC LAFANYIKA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amezitaka taasisi na wadau mbalimbali wanaoshughulikia maendeleo ya Lugha ya Kiswahili nchini kuchambua kwa kina na kutoa mapendekezo ya namna ambavyo Tanzania inaweza kunufaika na Lugha ya Kiswahili kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Mhe. Abdullah ametoa agizo hilo leo tarehe 26 Mei 2021 wakati akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na kuwashirikisha wanafunzi na wadau kutoka sekta mbalimbali.

 

Mhe. Abdullah amesema kuwa, Lugha ya Kiswahili ambayo ilipitishwa kuwa miongoni mwa Lugha nne rasmi  zinazotumika SADC ni rasilimali mojawapo inayoweza kuchangia uchumi wa nchi endapo Serikali, Taasisi, Mashirika na Wadau mbalimbali watashirikiana  kikamilifu ili kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa inayouzika katika nchi za SADC.

 

“Kwa kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha mama, lugha ya taifa na rasmi kwenye Taifa letu ni vizuri Kongamano hili likachambua kwa kina jinsi ambavyo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla inaweza kunufaika na Lugha hii kupitia Jumuiya. Pia tuchekeche kwa undani na kupendekeza kile ambacho Serikali inaweza kufanya kwa kushirikiana na wadau husika ili kuona Kiswahili kinakuwa ni bidhaa inayouzika kwa nchi za SADC” alisema Mhe. Abdullah

 

Aliongeza kusema kuwa kwa sasa wapo vijana wengi wahitimu wa ngazi mbalimbali wa mafunzo ya ualimu wa Kiswahili na hawana ajira, hivyo alisema vijana hao wanaweza kutumia fursa hiyo na kwenda kufundisha Kiswahili kama lugha ya pili katika nchi za SADC.

 

Kadhalika Mhe. Abdulah alitumia fursa hiyo kulikumbusha Baraza la Kiswahili la Zanzibar kuzingatia maelekezo yaliyotolewa kwao wakati wa Kongamano la Kiswahili lililofanyika mwaka 2020 ya kujiimarisha ili kuona Kiswahili kinastawi na kuuzika nje ya nchi kwa faida ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

 

Mbali na Lugha ya Kiswahili, Mhe. Abdullah aliwataka washiriki wa Kongamano hilo pia kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kunufaika na Sekta ya Uchumi wa Bluu ambayo ni miongoni mwa sekta za kipaumbele za Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar.

 

“Napenda kuwakumbusha kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya uchumi wa bluu inayoelekeza matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali Bahari ili kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini. Hivyo basi ni muhimu kuonesha namna ambavyo Zanzibar inaweza kutekeleza kipaumbele hicho na kuimarisha sekta ya uchumi wa bluu kupitia SADC” alisisitiza Mhe. Abdullah.

 

Pia alisisiza umuhimu wa kutumia maadhimisho hayo kuuelewesha umma wa Watanzania kuhusu Jumuiya hiyo katika ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye SADC.

 

Awali akizungumza wakati wa Kongamano hilo ambalo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na SUZA, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said alisema kuwa kuwa upo umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano katika sekta ya elimu na nchi za SADC ili wananchi wa Tanzania wanufaike na fursa za elimu ikiwemo vyuo vya elimu ya juu vinavyopatikana kwenye nchi hizo.

 

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar alisema kuwa Jumuiya ya SADC inazo fursa nyingi za kitaaluma na kitaalam ambazo zitasaidia Chuo hicho kujenga mashirikiano na vyuo ambavyo vipo katika nchi wanachama kwa manufaa ya watanzania.

 

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ni Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar, Bw. Masoud Abdallah Balozi aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano hilo na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Wizara ili kwa pamoja waweze kunufaika na Jumuiya ya SADC.

 

Wakati wa Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo “Historia ya SADC” iliyowasilishwa na Waziri Wa Fedha Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa mada isemayo          “Fursa zilizopo SADC kwa Zanzibar” ambayo iliwasilishwa na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga na mada kuhusu “Mafanikio na Changamoto katika SADC iliyowasilishwa na Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA, Dkt. Abdallah Rashid Mkumbukwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) limefanyika katika Ukumbi wa Shule ya Utalii ya Chuo hicho uliopo eneo la Maruhubi, Zanzibar tarehe 26 Mei 2021. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni "Miaka 40 ya kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha maendeleo na Ustahmilivu wa Changamoto zinazoikabili Dunia".

Mhe. Abdullah akihutubia Kongamano

Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said akizungumza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Zakia Mohammed Abubakar naye akizungumza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ni Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar, Bw. Masoud Abdallah Balozi akitoa salamu za Wizara wakati wa Kongamano hilo

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa akizungumza wakati wa Kongamano hilo

Mabalozi Wadogo na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa waliopo Zanzibar wakiwa kwenye Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC

Sehemu ya Wanafunzi wakifuatilia matukio

Wadau wengine walioshiriki Kongamano

Kongamano likiendelea

Waziri wa Fedha Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakati wa Kongamano hilo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga akiwasilisha mada kuhusu "Fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa Zanzibar"

Balozi Mtaafu, Mhe. Mohammed Haji Hamza akiongoza majadiliano wakati wa Kongamano hilo

Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUZA, Dkt. Abdallah Rashid Mkumbukwa akiwasilisha mada kuhusu " Mafanikio na Changamoto miongoni mwa Nchi Wanachama wa SADC"

Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA naye akiwasilisha mada

Picha ya pamoja

Wadau mbalimbali wakichangia wakati wa majadiliano

Mmoja wa washiriki akichangia jambo

Mwanafunzi wa SUZA akichangia jambo

Mdau akichangia