Saturday, May 29, 2021

NAIBU WAZIRI MBAROUK; TANZANIA ITAENDELEA KUHESHIMU NA KUTAMBUA MCHANGO WA WALINDA AMANI KOTE DUNIANI.

Tanzania inaendelea kuheshimu na kuthamini mchango na kazi kubwa inayofanywa na Walinda Amani kote duniani. Haya yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo pia aliongoza zoezi la uwekaji mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa. “lengo kuu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchangia vikosi vyake kwenye Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika maeneo yenye migogoro na wananchi wa maeneo hayo wanarejea kwenye shughuli zao za kila siku” Naibu Waziri Mbarouk.

Tanzania inashikilia nafasi ya 13 kwa wingi wa idadi ya askari miongoni mwa nchi 122 zinazochangia vikosi kwenye Umoja wa Mataifa. Kutoka nchi za Afrika, Tanzania inashikilia nafasi ya 7 kati ya nchi 35 zinazochangia vikosi vya kulinda amani. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2021, Tanzania ilikuwa na jumla ya Askari 1,481 kwenye Misheni sita za ulinzi wa amani sehemu mbalimbali duniani. 

Aidha, Naibu Waziri Mbarouk ameeleza furaha kuona Umoja wa Mataifa (UN) umetambua mchango na umuhimu wa vijana ambao ndio hutoa mchango mkubwa katika misheni za kulinda amani. “Nafurahi kuona UN wanatambua mchango wa vijana kupitia maazimio ya Baraza la Usalama Na. 2250 (la mwaka 2015) kuhusu vijana, amani na usalama; Azimio Na. 2419 (la mwaka 2018) kuhusu kuwajumuisha vijana kwenye majadiliano na utekelezaji wa makubaliano ya amani; na Azimio Na. 2535 (la mwaka 2020) ambalo hutaja hatua za utekelezaji za ajenda ya vijana, amani na usalama kwenye maeneo ya operesheni za amani”. ameeleza Naibu Waziri Mbarouk 

Licha ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hushiriki pia katika jitihada za kuimarisha amani kwa nchi zinazotuzunguka kuupitia mitangamano ya kikanda kama vile, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akihutubia hadhira iliyojitokeza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akikagua gwaride kwenye maadhimisho ya siku ya walinda amani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) akiweka mashada kama ishara ya kuwakumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakati wa harakati za kudumisha amani kwenye operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.