Tuesday, May 4, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS UHURU KENYATTA AMUALIKA KUWA MGENI RASMI MIAKA 60 YA TANZANIA BARA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta alipowasili katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya tarehe 04 Mei, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako yupo katika ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wakielekea kwenye mazungumzo ya Pamoja na Ujumbe wa Tanzania na Kenya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta wakati nyimbo za Taifa za Tanzania na Kenya zilipopigwa mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya tarehe 04 Mei, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima liloandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya tarehe 04 Mei, 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wakielekea kwenye mazungumzo ya Pamoja na Ujumbe wa Tanzania na Kenya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta mara baada ya mazungumzo yao katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya na amemualiaka kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika tarehe 9 Disemba 2021.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yao Mhe. Rais Samia amesema wamekubaliana kukuza na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kidugu, kihistoria na wa kirafiki uliopo baina ya nchi mbili.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa wamekubaliana kutekeleza miradi ya pamoja ya kimkakati ikiwamo miradi ya usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa na kuangalia jinsi ya kupata nishati ya umeme na gesi kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es salaam hadi Mombasa na kusisitiza kuwa ni wakati wa kuitekeleza miradi hiyo kwa vitendo.

Mhe. Rais amesema kuwa wamekubaliana kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara, kuimarisha usafiri wa majini katika ziwa Victoria, reli na anga na kushughulikia uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kuagiza Tume ya pamoja ya Ushirikiano (JPC) kukutana kushughulikia vikwazo hivyo ili kuondoa mivutano na misuguano  inayokwamisha juhudi za kukuza uchumi kwa nchi hizo. 

Amesema Tanzania imejipanga kwa nguvu zote kuwekeza nchini Kenya ili kukuza ujazo wa biashara na kuongeza miradi ya uwekezaji kutoka kampuni 30 za watanzania zilizowekeza mtaji wenye thamani ya Shilingi bilioni 19.3 za Kenya ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 410.2 za Tanzania na kutoa ajira kwa wakenya 2640.

Amesema Kenya ni miongoni mwa nchi zilizowekeza nchini kwa kiwango kikubwa ambapo kampuni 513 za nchi hiyo zimewekeza nchini mtaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7  ambazo ni sawa na Shilingi trilioni 3,888 na kuzalisha ajira  51,000  kwa watanzania na amemuhakikishia mwenyeji wake kuwa atawashawishi wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kuwekeza kwa wingi nchini Kenya.

Awali, akizungumza katika mkutano huo Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta alimuhakikisha Rais Samia kuwa Kenya itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na Tanzania ili kutimiza lengo la kuziletea maendeleo nchi hizo na kuongeza kuwa Kenya itaendeleza juhudi za kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi mbili hizo ili kuinua uchumi kupitia sekta mbalimbali kama vile biashara, uwekezaji, madini, nishati, mifugo, usafirishaji, ulinzi na usalama kwa manufaa ya nchi zote mbili na watu wake.

Mhe. Kenyata amekubali mualiko wa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kuahidi kuungana na Watanzania wakati wa maadhimisho hayo yatakayofanyika nchini tarehe 9 Disemba, 2021.

Mhe. Rais Samia yuko katika ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya.

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.