Thursday, November 30, 2017

Naibu Waziri afanya Mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Suzan Kolimba(Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini Mhe. Balozi Mohammed M. Almalik alipomtembelea wizarani tarehe 30/11/2017. Lengo la Mazungumzo hayo ni kuzungumzia mahusiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia, Mhe.Balozi alisema hadi sasa Saudi Arabia wana jumla ya miradi  6 katika eneo la maji na afya, kati ya hiyo 3 iko Tanzania bara na 3 Zanzibar.

 
Mhe. Naibu Waziri Dkt Kolimba na Mhe. Balozi Almalik wakiendelea na mazungumzo, wanaofuatilia mazungumzo hayo ni Bw. Charles Faini Msaidizi wa Naibu Waziri(kulia) na anayefuata ni Bw. Odilo Fidelis, Afisa Mambo ya Nje.

Monday, November 27, 2017

Waziri Mahiga akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akizungumza na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Roberto Mengoni alipomtembea katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Novemba 2017.

Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Italia. Pia wamejadili mikakati ya kuboresha ushirikiano katika sekta ya elimu hususan elimu ya ufundi, miundombinu, utalii, biashara na uwekezaji.
Mazungumzo ya Kiendelea.



Saturday, November 25, 2017

Katibu Mkuu ashiriki Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na China

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  Prof.Adolf Mkenda (kulia) akizungumza katika  wa Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na China

Katibu Mkuu Prof.Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Serikali ya Tanzania na wa Serikali ya Watu wa Jamhuri ya China mara baada ya kuhitimisha Mkutano na Benki ya Uwekezaji ya Asia.

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika Mkutano wa Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Uwanja wa ndege wa Hanan (Hanan Airport Special Economic Zone) uliofanyika nchini China.

Wajumbe wakifuatilia Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na China

Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza kwenye Mkutano wa  Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na China

Friday, November 24, 2017

Wizara kuongeza wigo wa matumizi ya kiswahili Afrika Mashariki

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba leo  akiongea na Wanachama wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) amesema Wizara inaendelea na jitihada za kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo hadi sasa tayari baadhi ya nchi wanachama zimeshaweka lugha ya Kiswahili katika mitaala ya Elimu katika shule za Msingi na Sekondari  hatua ambayo itawezesha kuongeza wigo wa matumizi ya lugha hii katika Jumuiya yetu.

Mhe. Dkt Kolimba akizungumza katika kongamano hilo amewapongeza Viongozi na Wanachama wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki kwa kuwahusisha baadhi ya Ofisi za Balozi zilipo nchini katika hatua za kufanikisha Kongamono hilo. Kwa namna ya pekee alitumia fursa hiyo kumpongeza  Balozi wa Kuwait nchini Mhe.Jaseem Al Najem na Watumishi wa Ubalozi huo kwa kukubamwaliko wa kushiriki Kongamano na kwa mchango waliotoa kufanikisha Kongamano hilo.

Tokea mwaka 2004 hadi sasa Kiswahili kimekuwa lugha ya kwanza ya Afrika kutumika katika vikao vya Ngazi ya Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika, hii ni kufuatia jitihada na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Jitihada hizo ilikuwa ni pamoja na kugharamia wakalimani kwa fedha za ndani, na mwaka 2008 Wizara iliishawishi Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuchukua jukumu hilo.

Aidha Mhe. Dkt. Kolimba amewahakikishia Viongozi na Wanachama wa CHAKAMA kuwa nia ya Serikali ya kufungua vituo vya kufundishia lugha ya  kiswahili  sehemu mbalimbali nje ya mipaka ya Tanzania bado iko palepale, "tayari tulishafungua kituo kimoja mwaka 2012 katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia" amesema Mhe. Dkt. Kolimba.

CHAKAMA imehitimisha Kongamano lake leo lililofanyika kwa muda wa siku mbili mjini Dodoma ,likiwa na kauli  mbiu ya "Kiswahili na Maendeleo ya Afrika Mashariki" chama hiki kinaundwa na nchi Wanchama za Jumuiya ya Afrika pia kinahusisha wanachama kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Ghana na Zimbabwe.


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akihutubia washiriki wa kongamano la Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki lililofanyika katika Hoteli ya African Dream mjini Dodoma

Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba akimkabithi cheti cha ushiriki mmoja wa wajumbe wa Kongamo la CHAKAMA

Naibu Waziri Mhe.Dkt. Kolimba  akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kongamano



Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa akutana na Msajili wa UN-MICT

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Celestine Mushy akizungumza na Msajili wa Mfumo wa Kimataifa wa kumalizia mashauri masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (MICT), Dkt. Olufemi Elias alipotembelea katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Novemba 2017.

Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Chipeta na Maafisa mambo ya nje wakifuatilia mazungumzo.

Maafisa walioambatana na Msajili wa UN-MICT wakifuatilia mazungumzo.

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje ziarani China kushiriki Mkutano wa FOCAC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akifungua Mkutano wa kuvutia wawekezaji uliofanyika Ubalozi wa Tanzania nchini China na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Makampuni 100 yenye nia ya kuwekeza Barani Afrika. Prof. Mkenda yupo nchini China kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 12 wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC unaofanyika kwa ngazi ya Watendaji.
Prof. Mkenda akizungumza na Kiongozi wa Benki ya AIIB iliyoanzishwa kwa lengo  la kutoa mikopo kwa miradi ya miundombinu kwa nchi wanachama wa Belt and Road. Benki hiyo imeikaribisha Tanzania kujiunga nayo ili iweze kufaidika na fursa za mikopo nafuu. Vilevile, Prof. Mkendaamekutana na uongozi wa Kampuni ya Hainan Group inayomiliki mashirika mbalimbali ya ndege na Hoteli zaidi ya 1000 ulimwenguni. Katika mazungumzo hayo Prof. Mkenda amewashawishi wawekeze kwenye ujenzi wa Hoteli katika maeneo ya Utalii Zanzibar na Tanzania Bara.
Ujumbe ukifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Kiongozi wa Benki ya AIIB (hawapo pichani).  Kutoka kushoto ni Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Lu Yongqing, aliyekuwa Balozi wa China nchini Tanzania na Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini China.
Ujumbe kutoka Benki ya AIIB
Prof. Mkenda akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua Mkutano wa Kuvutia Wawekezaji uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini China.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Chen Xiaodong akifungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika unaofanyika tarehe 24 Novemba, 2017 Beijing, China. Baada ya ufunguzi kiongozi huyo amefanya mazungumzo ya kukuza ushirikiano na nchi nne Tanzania ikiwa ya kwanza kukutana nayo. Katika mazungumzo kati ya Prof. Mkenda na Mhe. Xiaodong, China imeahidi kuendeleza ushirikiano katika nyanja  za uchumi hususan kwenye ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa Eneo Maalum la Uwekezaji Bagamoyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. CHEN Xiaodong mara baada ya kukamilisha mazungumzo ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.

Wednesday, November 22, 2017

Naibu Waziri afanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Korea chini Tanzania Mhe. Song, Geum-Young walipokutana  na kufanya mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mhe. Dkt. Kolimba katika mazungumzo hayo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuchangia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo eneo la afya, elimu na teknolojia. Aidha amemuhakikishia Mhe. Balozi Young kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla wataendelea kuboresha uhusiano mzuri wa Kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea

Naibu Waziri Mhe.Dkt. Kolimba akimsiliza Balozi wa Jamhuri ya Korea Mhe. Young, kulia ni Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo

Mhe. Dkt. Kolimba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo

Naibu Waziri Mhe. Dkt. Kolimba akipokea machapisho yenye ujumbe mbalimbali kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe.Young mara baada ya mazungumzo 

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP nchini


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf  Mkenda akifanunua jambo kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bibi Natalie BOUCLY walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu Prof. Mkenda amemuhakikishia ushirikiano Mkurugenzi Mkazi wa UNDP katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Katibu Mkuu Prof. Mkenda akimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) nchini Bibi Natalie BOUCLY

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) nchini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Mazungumzo. Wengine ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa  Wizarani Balozi Celisitine J Mushy (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Mradi kutoka UNDP Bw. Amon Manyama (wa kwanza kushoto)

Monday, November 20, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Shelisheli awasilisha Hati za Utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Shelisheli mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Mhe. Danny Faure. Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 14 Novemba 2017, katika Ikulu ya nchi hiyo.
Mhe. Balozi Chana  akizungumza na Mhe. Rais Faure ambapo Serikali ya Jamhuri ya Shelisheli imemuhakikishia kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mhe. Balozi Chana akiwasili katika Ikulu ya Jamhuri ya Shelisheli.

Sunday, November 19, 2017

UFAFANUZI KUHUSU UINGIZWAJI WA MIFUGO NCHINI TANZANIA


TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU UINGIZWAJI WA MIFUGO NCHINI TANZANIA

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari na kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuishutumu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia hatua ya kukamata na kupiga mnada mifugo iliyoingizwa nchini bila kufuata sheria. Aidha, taarifa hizo zinajenga sintofahamu kuhusiana na suala la vifaranga vya kuku vilivyoteketezwa kufuatia kuingizwa nchini bila kufuata sheria. Baadhi ya taarifa hizo zimeenda mbali zaidi na kudai kuwa hatua hizi zinaweza kudhoofisha mahusiano yetu na nchi jirani. 

Kadhalika, kufuatia suala hilo la kupigwa mnada kwa ng’ombe walioingia nchini kinyume cha sheria, na wenye ng’ombe hao kukaidi kuondoa mifugo yao hata baada ya kupewa muda kufanya hivyo, na kufuatia kuteketezwa kwa vifaranga vilivyoingia nchini kinyume cha sheria na kanuni, Serikali ya Kenya ilimwita Balozi wetu aliyeko Nairobi kutaka maelezo. Balozi wetu alisikiliza maelezo ya Serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea masuala haya kwa Serikali ya Kenya. Vile vile Serikali imepokea barua kutoka Serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na Serikali itaijibu barua hiyo kutoa ufafanuzi.

Serikali inapenda kuufahamisha umma kwa ujumla kuwa uingizwaji wa mifugo na bidhaa zake nchini Tanzania huongozwa na sheria za nchi, makubaliano ya kikanda na kimataifa.


Sheria na taratibu hizi ni pamoja na:
(i)    Sheria ya Magonjwa ya Wanyama (Animal Disease Act) Na. 17 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2007 na 2010, ambazo zinatumika kudhibiti na kukagua uingizaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege;
(ii)   Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama (Grazing-land and Animal Feed Resources Act) Na. 13 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia nyanda za malisho na ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo;
(iii)   Zuio (quarantine)  la uingizaji ndege na mazao yake nchini la mwaka 2006, kutokana na uwepo wa ugonjwa hatari wa Homa ya Mafua Makali ya Ndege katika nchi mbalimbali duniani. Ugonjwa huo umejitokeza kwenye nchi jirani ya Uganda mwanzoni mwa mwaka 2017 na hivyo kuiweka nchi yetu katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu iwapo zuio hili litakiukwa. Zuio hilo halijaondolewa hadi leo.
(iv)  Ukweli kwamba katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mifugo na bidhaa za mifugo zinavuka mipaka kwa utaratibu maalum kupitia kwenye vituo vya mipakani ambapo maofisa mifugo kutoka pande zote za mipaka hufanya shughuli ya udhibiti.
Utekelezaji wa sheria na makubaliano haya hufanyika bila ubaguzi wa uraia wa mwingizaji wa mifugo au nchi inakotoka mifugo hiyo. Nchi zote duniani, zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinadhibiti uingizwaji wa mifugo na mimea katika nchi zao. Udhibiti huu hufanyika katika viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mipakani. Kwa mfano, katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani cha Namanga, wapo maofisa wa mifugo na kilimo kutoka Kenya na Tanzania wanaodhibiti uingizwaji wa mifugo na mimea kwenye nchi zao.

Katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hii, ilibainika kuwa idadi kubwa ya mifugo kutoka nchi za jirani imeingizwa nchini pasipo kufuata sheria na taratibu zilizopo. Serikali iliagiza mifugo hiyo irudishwe kwenye nchi ilikotoka kwani ilikuwa inahatarisha mazingira na kuongeza uwezekano wa kusambaa magonjwa ya mifugo. Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa wamiliki wa mifugo hiyo kuiondoa nchini. Tahadhari ilitolewa kwamba muda uliotengwa ukifikia ukomo, mifugo hiyo itakamatwa na kushugulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Pamoja na agizo hilo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilituma Waraka wa Kidiplomasia  kwa Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, ikizihimiza kuwataka raia wao walioingiza mifugo nchini isivyo halali waiondoe. Wamiliki wengi walitii agizo hilo la Serikali ya Tanzania na kuondoa mifugo yao nchini.

Hata hivyo, wapo wamiliki wachache kutoka nchi za jirani waliokaidi agizo hilo na hivyo ng’ombe wapatao 1113 walikamatwa katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kupigwa mnada baada ya wamiliki wake kushindwa kujitokeza. Katika mkoa huo wa Kilimanjaro wapo ng’ombe 74 ambao wamiliki wake walijitokeza, wakalipa faini kwa amri ya mahakama na kuondoka na ng’ombe wao. Katika Mkoa wa Kigoma ng’ombe 324 ambao wamiliki wake hawajajitokeza wamekamatwa na hatua stahiki zinachukuliwa. Aidha, katika mkoa huo wa Kigoma ng’ombe 728 walikamatwa na wamiliki wao walijitokeza na kulipa faini kutokana na maamuzi ya Mahakama. Katika mkoa wa Kagera jumla ng’ombe 1,536 ambao wamiliki wake bado hawajulikani wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama na sheria itachukua mkondo wake.

Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba zoezi hili halijalenga nchi yeyote, kwa sababu sio nchi moja tu imeathirika. Zoezi hili limelenga kutekeleza sheria na kanuni za nchi yetu ili kulinda mazingira na kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ya mifugo. Hili suala halipaswi kusababisha mgogoro wa kidiplomasia na nchi yeyote, labda tu mtu aamue kwa makusudi yasiyo mema kupotosha na kuchochea mgogoro.

Aidha, tarehe 24 Oktoba, 2017 jumla ya vifaranga vya kuku wa mayai 6,400 vilikamatwa katika Mkoa wa Arusha kwa kuingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni. Vifaranga hivyo vilikuwa kwenye maboksi 60 vikiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 285 BAY. Mmiliki wa vifaranga hivi alidai kwamba ameviingiza nchini kutokea Kenya. Vifaranga hivi viliteketezwa kutokana na msafirishaji wa vifaranga hivi kutokuwa na kibali cha aina yoyote kutoka mamlaka husika ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo hapa nchini ambayo ni Idara ya Huduma za Afya Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Pia, mmiliki huyu alishindwa hata kuonesha kibali cha Serikali ya Kenya kumruhusu kusafirisha vifaranga hivyo kutoka Kenya kuvileta Tanzania pamoja na kwamba mmiliki huyu alidai kwamba vifaranga hivyo amevitoa Kenya. Ni muhimu ikafahamika kwamba nchi zote duniani, ikiwemo Kenya, hufuata miongozo ya WTO na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kwa kutoa vibali (export permit) kwa mtu yeyote anayetaka kusafirisha mifugo nje ya nchi. Kosa jingine kubwa ni kwamba vifaranga hivi havikupitishiwa kwenye vituo rasmi vya Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake mipakani (zoosanitary border posts) kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.

Pamoja na yote haya, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania alimpigia simu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (Director of Veterinary Services) wa Kenya kutaka kujua kama Mamlaka za Kenya zina habari kuhusu vifaranga waliokamatwa na kama Kenya itakubali kuruhusu vifaranga hivyo virudishwe Kenya. Mkurugenzi huyu wa Kenya alisema hana taarifa kuhusu vifaranga hivyo na kwamba Kenya haiko tayari kuruhusu vifaranga hivyo kurudishwa nchini mwao kwa sababu havina nyaraka kulingana na miongozo ya kimataifa.

Ni vizuri umma ukajua kwamba hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuteketeza vifaranga vilivyoingizwa nchini bila kufuata sheria kanuni na taratibu. Vipo vifaranga vingi tu vimeteketezwa kwa namna hiyo hiyo baada ya kukamatwa kwenye viwanja vyetu vya ndege na sehemu nyingine. Kadhalika vifaranga ambavyo vimekuwa vikiteketezwa havitokei nchi moja tu. Vifaranga vyote vinavyoingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni zinazotulinda dhidi ya uwezekano wa magonjwa vinateketezwa mara moja bila kujali vinatoka nchi gani. Hatua hizi tumekuwa tukizitekeleza tangu tuweke zuio mwaka 2006, na hazijaathiri kwa namna yeyote ile mahusiano yetu na nchi yeyote. Hatua yeyote ya kujaribu kufanya jambo hili kuwa ni la mgogoro wa kidiplomasia dhidi ya nchi yeyote ile ni hatua isiyo sahihi.

Serikali inawaasa wananchi na raia wa kigeni wazingatie sheria, kanuni na taratibu pale wanapotaka kuingiza nchini  au kusafirisha nje ya nchi mifugo na mazao yake. Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu za nchi, kikanda na kimataifa zinazohusu utoaji na uingizaji wa mifugo na mazao yake nchini. Tunapenda kuuhakikishia umma kwamba, usimamizi wa sheria hizi hauwezi na hautakiwi kwa namna yoyote ile kuathiri mahusiano yetu na nchi nyingine kwa sababu nchi zote duniani zinasimamia sheria kama hizi.
Mojawapo ya misingi ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kujenga na kuimarisha mahusiano na nchi nyingine pamoja na kudumisha ujirani mwema. Hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa inalinda mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu kati yake na nchi nyingine duniani. Kadhalika, Serikali itaendelea kutumia fursa mbali mbali, kama vile vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikao vya pande mbili kati yetu na jirani zetu, na pia vikao vya ujirani mwema mipakani, kutatua changamoto zozote za kimahusiano zitakazo jitokeza kwa nia ya kuendelea kuimarisha ujirani mwema.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

19 Novemba, 2017

Tuesday, November 14, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Korea awasilisha hati za utambulisho

Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Matilda Masuka (kushoto) akitoa salam ya heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in wakati wa hafla ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Taifa hilo.

Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Matilda Masuka (kushoto) akiwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in

Balozi Mhe.Masuka na Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe.Moon Jae-in wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya zoezi la kuwasilisha hati za utambulisho

Monday, November 13, 2017

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje afanya mazungumzo na Balozi China nchini


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa China nchini Mhe. WANG Ke wakifuarahia jambo walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Mjini Dodoma.Naibu Waziri amemuhakikishia Mhe.Balozi WANG Ke kuwa Wizara na Serikali wataendelea kudumisha uhusiano wa kahistoria uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China. Pia Mhe. Dkt. Kolimba alitumia fursa hiyo  kuishukuru Serikali ya China kwa kufadhili miradi mbalimbali hapa nchini
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa China nchini Mhe. WANG Ke wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa nchi wa Falme za Kiarabu nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi wa Umoja wa nchi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mhe. Balozi Abdulla Ibrahim Alsuwaidi walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalikita katika kujadili masuala mbalimbali ya namna ya kudumisha na kukuza uhusiano baina ya pande mbili. (Tanzania na Umoja wa Nchi wa Falme za Kiarabu)  
Waziri Mhe.Balozi Dkt.Mahiga na Mhe. Balozi Alsuwaidi wakifurahia jambo wakati walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazunguzo
Waziri Mhe. Mahiga akimsikiliza Balozi wa Nchi wa Falme za Kiarabu nchini Mhe.Abdulla Ibrahim Alsuwaidi walipokutana kwa Mazungumzo Jijini Dar es Salaam

2018 SADC SECONDARY SCHOOL ESSAY COMPETITION





N:B All applicants are requested to send their applications to the following address:
    
         Permanent Secretary
         Ministry of Education,  Science and Technology
         Block 10,
         College of Business Studies and Law,
         University of Dodoma,
         P.O.Box 10
         DODOMA



















Friday, November 10, 2017

Kaimu Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa akutana na Ujumbe wa EU nchini

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Jestas Nyamanga akizungumza na Kaimu Kiongozi  wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Bw. Charlie Stuart alipofika Wizarani tarehe 10 Novemba, 2017 kwa ajaili ya kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu Umoja huo na masuala mengine ya Kimataifa.
Sehemu ya Ujumbe uliofuatana na Bw. Stuart wakifuatilia mazungumzo
Sehemu nyingine ya ujumbe kutoka EU na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Thursday, November 9, 2017

Katibu Mkuu afanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Pro.Adolf Mkenda akiwa katika mzungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) inchini Bibi Abla Beuhammouche,Wizarani Jijini Dar es Salaam. Pamoja na masuala mengine mazungumzo hayo yalijikita katika kujadili njia bora zaidi za kutekeleza miradi ya kilimo na uhifadhi wa mazingira. IFAD inatekeleza miradi ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda akimsiliza Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini Tanzania  Bibi Abla Beuhammouche walipokutana kwa mazungumzo Wizarani Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda na Mkurugenzi Mkazi wa IFAD nchini Tanzania  Bibi Abla Beuhammouche wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo