Wednesday, August 31, 2016

Mkurugenzi wa Idara ya Asia akutana na Mwakilishi masuala ya Uchumi Ubalozi wa China

Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki (kulia) akizungumza na  mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Jamhuri ya Watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw.Li Zhiyong ambaye alimtembelea katika Ofisi za Wizara tarehe 31 Agosti, 2016.
 Mazungumzo yao yalijikita katika kujadili maandalizi ya mkutano wa 5 wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano wa masuala ya Teknolojia  kati ya Tanzania na China unaotarajiwa kufanyika nchini   tarehe 13 Oktoba, 2016.
Maafisa wa Ubalozi wa China wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mbelwa na Bw. Zhiyong (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea

Monday, August 29, 2016

Waziri Mkuu atembelea Banda la Tanzania na nchi zingine maonesho ya TICAD VI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka kuhusu Michoro maarufu ya Tanzania ijulikanayoo kama Tingatinga alipotembelea Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan yaliyofanyika Jijini Nairobi wakati wa Mkutano wa TICAD VI. Wengine wanaoshuhudia ni Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Chirau Ali Mwakere (wa kwanza kushto),  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ya Kenya, Bi. Betty Maina na Kaimu Balozi wa Tanzania, Kenya, Bi. Talha Waziri.
Bw. Rutageruka akisisitiza jambo kuhusu michoro hiyo kuwa asili yake ni Tanzania na si sehemu nyingine yoyote
Mhe. Waziri Mkuu akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Cliford Tandari (kushoto) alipowasili kwenye Banda la maonesho la TIC.
Mhe. Waziri Mkuu akisaini kitabu cha wageni kwenye Banda la TIC huku Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho Bw. Tandari na Maafisa kutoka TIC wakishuhudia.
Mhe. Wazir Mkuu akimsikiliza Meneja wa Uwekezaji wa EPZA, Bw. Lameck Borega alipotembelea Banda lao la Maonesho.
Mhe. Waziri Mkuu akisalimiana na Bi. Alistidia Karaze, Afisa Utafiti Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) alipotembelea Banda la Maonesho la TTB.
Bi. Karaze akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kuhusu mikakati ya kutangaza Utalii inayofanywa na TTB.
Mhe. Waziri Mkuu nae akitoa maelekezo kuhusu namna bora ya kujipanga katika kutangaza utalii. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Sayansi, Prof. Makame Mbarawa ambaye naye alikuwa Jijini Nairobi kuhudhuria Mkutano wa TICAD VI
Mhe. Waziri Mkuu akipata maelezo kuhusu soko la Batiki kutoka kwa mmoja wa akina mama wa Kitanzania wanaoshiriki maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan Jijini Nairobi alipotembelea Banda lao. Kushoto ni Bw. Francis Mosongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan katika Ubalozi wa Tanzania, Japan.
Mhe. Waziri Mkuu akimsikiliza mshiriki mwingine kutoka Tanzania ambaye anajishughulisha na biashara ya bidhaa kutoka Tanzania kama vitege, khanga, na batiki

Mhe. Waziri Mkuu akiwa ametembelea Banda la Maonesho la Rwanda

Mhe. Waziri Mkuu akipata maelezo alipotembelea Banda la Maonesho la Kenya

Mhe. Waziri Mkuu akikaribishwa alipotembelea Banda la Maonesho la Uganda
Mhe. Waziri Mkuu akinsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Sumitomo ya Japan alipotembelea Bandani hapo. Kampuni ya Sumitomo ndiyo inajenga mitambo ya uzalishaji wa Umeme wa gesi asilia wa Megawati 240 iliyopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa Sumitomo akimwonesha Waziri Mkuu picha za Mitambo ya Umeme iliyopo Kinyerezi
Mhe. Waziri Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya waliofika Uwanja wa Ndege wa Jommo Kenya kwa ajili ya kumsindikiza kabla ya kuondoka kurejea nchini mara baada ya kuhudhuria Mkutano wa TICAD VI. Katika Picha ni Bi. Talha Waziri, Kaimu Balozi wa Tanzania, Kenya; Bw. Mkumbwa Ally (wa pili kushoto), Bw. Amos Mwakasege (kushoto) na Bw. Loshilaari Ole Kambainei (Kulia), Maafisa Waandamizi Ubalozini hapo.


Sunday, August 28, 2016

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi wa Gesi


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa kwenye Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan lililofanyika Nairobi, Kenya wakati wa Mkutano wa TICAD VI. Kongamano hilo pia lilifuatiwa na hafla ya baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuingia makubaliano na Makampuni na Mashirika ya Japan katika kuimarisha biashara na uwekezaji. Mhe. Majaliwa alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa TICAD VI uliofanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyeji na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa TICAD VI akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan. Kushoto ni Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe na kulia ni Naibu Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe nae akizungumza kwenye Kongamano hilo
Baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu na Makamu wa Rais wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Kongamano la Biashara la Afrika na Japan. Kushoto ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Viongozi akiwemo Mhe. Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Mjumbe kutoka Chiyoda kuashiria Makubaliano kati ya Tanzania na Shirika la Chiyoda ambalo litashirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo kwa Wahandisi kwenye masuala ya gesi na mafuta. Waliosimama kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe; Bw. Francis Mossongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Shirika la Chiyoda.
============================================

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameshiriki hafla iliyoashiria kusainiwa kwa makubaliano kati ya baadhi ya nchi za Afrika na Makampuni mbalimbali ya Japan iliyofanyika wakati wa Mkutano TICAD VI jijini Nairobi.

Hafla hiyo ambayo ilitanguliwa na Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan ilihusisha nchi 20 za Afrika ambazo zimeingia makubaliano ya kuimarisha uwekezaji na biashara na Makampuni makubwa 22 ya Japan.

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imeingia Makubaliano na Shirika la CHIYODA kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wahandisi wa Tanzania kwa kuwapitia mafunzo kwenye masuala ya teknolojia ya gesi na mafuta.

Akizungumza wakati wa Kongamano hilo Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta alisema kuwa Kongamano hilo ni jukwaa muafaka wakati Afrika ikiwa katika jitihada za mageuzi ya kiuchumi. Hivyo aliziomba nchi za Afrika kutumia ujuzi na uzoefu mkubwa wa Japan katika kuiimarisha Sekta Binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia maendeleo.

Aidha, aliongeza kuwa Kenya ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wenzake kuhakikisha kunakuwepo mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kutoka nje hususan Japan. Pia aliishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa Afrika na kukaribisha uwekazaji kutoka sekta binafsi ya Japan kwenye maeneo ya uzalishaji wa nishati ya umeme na maeneo mengine.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe alisema kuwa Japan itaendelea kushirkiana na Afrika katika kuhakikisha inapiga hatua zaidi ya maendeleo. Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Afrika  na Japan Kampuni 22 na Vyuo Vikuu vya Japan zimefuatana nae ili kukamilisha mikataba 73 na nchi za Afrika. 

Aidha,  alieleza kuwa Kampuni za Japan zimetumia fursa ya Mkutano wa TICAD  VI kutangaza Azimio la Biashara ikiwa ni katika kuelezea nia na madhumuni yao katika kuchangia maendeleo ya Afrika.

Mbali na Tanzania nchi zingine za Afrika zilizoingia Makubaliano na Kampuni na Mashrika kutoka Japan ni pamoja na Kenya, Angola, Cameroon, Congo, Cote d’ Ivoire, DRC, Ethiopia, Misri, Ghana, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Uganda na Zambia.

Wakati huohuo, Mkutano wa Sita wa Kilele wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) umemalizika   Jijini Nairobi leo huku Wakuu wa Nchi na Serikali wakipitisha kwa kauli moja Azimio la Nairobi na Mpango Kazi  wa utekelezaji wake.

Azimio la Nairobi pamoja na mambo mengine linalenga katika kutekeleza mambo makuu matatu  ambayo ni: Kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchumi ili kuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha uchumi huku mkazo ukiwekwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vitakavyozalisha ajira kwa wingi kwa vijana wa Afria; Kujenga mifumo ya Huduma za Afya ambazo ni endelevu kwa maisha bora ikiwemo kuboresha huduma za afya, kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa kama Ebola, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na jamii nzima; na Kukuza na kuimarisha Utulivu na Ustawi wa Jamii.

Mbali na Mkutano wa Kilele wa TICAD VI, shughuli zingine zilizoenda sambamba na mkutano huo ni Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan; Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan; na Mkutano wa Majadilino ya Kibiashara kati ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni Binafsi.

Mkutano wa TICAD VI ambao ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 30 kutoka Afrika, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda pia uliyashirikisha Makampuni zaidi ya 100 kutoka Serikali ya Japan, Sekta Binafsi na kuhudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 10,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

-Mwisho-Waziri Mkuu akutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Jijini Nairobi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan, Mhe. Luteni Jenerali Barki Hassan Salih walipokutana Jijini na Nairobi wakati wa Mkutano wa TICAD VI kwa mazungumzo ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mhe. Majaliwa akiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba(kushoto) na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bi. Talha Waziri (wa pili kulia) na Bi. Irene Bwire, Mwandishi wa Waziri Mkuu wakifuatilia mazungumzo  kati yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan, Mhe. Lt. Gen. Salih na ujumbe wake hawapo pichani)
Mhe. Salih (wa tatu kushoto) akiwa na ujmbe aliofuatana nao wakati wa mazungumzo yake na Mhe. Majaliwa (hayupo pichani)Saturday, August 27, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Naibu Waziri wa Marekani masuala ya Afrika

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Mhe. Linda Thomas-Greenfield walipokutana wakati wa Mkutano wa TICAD VI Jijini Nairobi na kuzugumzia masuala ya ushirikiano. Wakati wa mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Kolimba alimshukuru Mhe. Greenfield kwa ushiriano uliopo kati ya Tanzania na Marekani ambapo nchi hiyo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za afya na miradi mingine ya maendeleo.
Mhe. Naibu Waziri akizungumza na Mhe. Greenfield 
Mazungumzo yakiendelea kati ya Mhe. Dkt. Susan na Mhe. Greenfield (hayupo pichani). Wengine katika picha ni Bi. Talha Waziri (kushoto), Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Bi. Bertha Makilagi (kulia), Afisa Mambo ya Nje.
Mhe. Greenfield akiwa na ujumbe wake nae akichangia jambo wakati wa mazungumzo yake na Mhe. Dkt. Susan (hayupo pichani)
Mhe. Dkt. Susan aiagana na mgeni wake Mhe. Greenfield  mara baada ya mazungumzo huku Bi. Makilagi (katikati) akishuhudia
Mhe. Naibu Waziri (mwenye gauni la bluu) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bi Talha Waziri (wa pili kutoka kulia), Bw. Adam Isara, Msaidizi wa Naibu Waziri na Bi. Bertha Makilagi (kushoto), Afisa Mambo ya Nje.

Banda la Maonesho la Tanzania lang'ara kwenye mkutano wa TICAD VI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akipokelewa  na Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka mara baada ya kuwasili kwenye Banda la Maonesho la Tanzania yanayofanyika wakati wa Mkutano wa TICAD VI Jijini, Nairobi. Makampuni na Taasisi mbalimbali kutoka nchi za Afrika ikiwemo Tanzania na Japan yanashiriki maonesho hayo yanayolenga kuvutia wawekezaji na wafanyabishara.
Mhe. Naibu Waziri akipata maelezo kuhusu bidhaa mbalimbali zinazozalishwa Tanzania zilizokuwepo kwenye Banda hilo. Bidhaa hizo ni pamoja na Kahawa, Majani ya Chai na Viungo vya chakula
Banda la Tanzania kama linavyoonekana
Mhe. Waziri akipata maelezo ya namna watu wa makampuni mbalimbali walivyovutiwa na kahawa ya Tanzania
Mhe. Naibu Waziri akikaribishwa na Bi. Latifa Kigoda, Afisa Mwandamizi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) alipotembelea banda la Tanzania
Mhe. Naibu Waziri akisaini kitabu cha wageni bandani hapo
Mhe. Naibu Waziri akisikiliza maelezo kutoka kwa Bi. Kigoda kuhusu namna TIC ilivyojipanga kutangaza fursa za uwekezaji kwa wawekezaji mbalimbali wanaohudhuria mkutano wa TICAD VI
Bi. Kigoda akimpatia Jarida Maalum lililoandaliwa na TIC kwa ajili ya kuvutia wawekezaji waliohudhuria mkutano wa TICAD VI
Bi. Kigoda akimpatia maelezo Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Bi. Talha Waziri ambaye alikuwa amefuatana na Mhe. Naibu Waziri.
Mmoja wa wageni aliyetembelea bandani hapo akipata maelezo ya fursa za uwekezaji zilizopo nchini kutoka kwa Bi. Kigoda
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt.  Susan Kolimba akipata maelezo kutoka kwa Bw. Lameck Borega, Meneja wa Uwekezaji wa EPZA.
Mhe. Dkt. Kolimba akimpatia ushauri wa namna ya kuwashawishi wawekezaji kuja nchini kuwekeza kupitia EPZA
Mhe. Naibu Waziri akiwa amewasili kwenye Banda la Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kupatiwa maelezo na Bi. Alistidia Karaze, Afisa Utafiti Mkuu kwenye Bodi hiyo
Mhe. Naibu Waziri akimpatia ushauri Bi. Karaze wa namna ya kuboresha huduma za utalii nchini ikiwemo maonesho ili kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea nchini.

Friday, August 26, 2016

Mkutano wa Mawaziri wa TICAD wafanyika Jijini Nairobi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha Mawaziri wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI)  uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) tarehe 26 Agosti, 2016. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Khalid Salum Mohammed na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki.
Balozi Mbelwa akitoa ufafanuzi kwa Mhe. Naibu Waziri kuhusu masuala yatakayojadiliwa kwenye Mkutano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Amina Mohammed akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Fumio Kishida nae akizungumza wakati wa mkutano wa Mawaziri
Sehemu ya Wajumbe waliohudhuria mkutano huo
Sehemu nyingine ya wajumbe
Picha ya pamoja ya meza kuu.
=======================================

 MKUTANO WA MAWAZIRI WA TICAD WAFANYIKA JIJINI NAIROBI

Kikao cha Mawaziri kuandaa Mkutano wa Kilele wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) kimemalizika   Jijini Nairobi leo ambapo Mawaziri hao wameikubali kwa kauli moja Rasimu ya Azimio la Nairobi na Mpango Kazi  wake tayari kwa  kuwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa ajili ya kupitishwa.

Akihitimisha Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Amina Mohammed amewashukuru Mawaziri wenzake, waandaaji wa kikao hicho na washiriki wote kwa kikao chenye mafanikio na kueleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa agenda zilizojadiliwa zitapitishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye Mkutano wao.

Aidha, alisema kuwa Rasimu hiyo ya Azimio ambalo linazungumzia agenda muhimu tatu ambazo ni Kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uendelezaji wa viwanda; Kuboresha sekta ya Afya kwa maisha bora na Kusaidia jitihada za kudumisha amani na utulivu katika jamii linalenga kutatua changamoto mbalimbali na kuiwezesha Afrika kufikia maendeleo endelevu.

Pia, aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuiunga mkono Afrika katika kukamilisha malengo yake ya maendeleo na kwamba mkutano huu wa 6 utaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afrika na Japan.

“Mkutano huu una lengo kubwa moja la kuiwezesha Afrika kufikia maendeleo endelevu kwa kushirikiana na Japan. Hivyo nawapongeza waandaaji na washiriki wote kwa kufanikisha rasimu ya Azimio la Nairobi na ni imani yangu kuwa Azimio hili litapitishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao” alisema Mhe. Mohammed.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Fumio Kishida alisema kuwa Afrika imeendelea kuwa mdau muhimu katika ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake inaona fahari kuendeleza ushirikian huo ili kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo endelevu. Pia aliishukuru Serikali ya Kenya kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa TICAD VI na ana matarajio makubwa kuwa utakuwa na tija.

Pia aliongeza kuwa Mikutano ya TICAD ni jukwaa muhimu linaloziwezesha nchi za Afrika na Japan kuangalia vipaumbele mbalimbali katika ushirikiano ili hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuinua uchumi na kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya.

Naye Waziri wa Uchumi na Mipango wa Chad, Mhe. Mariam Mahamat Nour ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika alisema kuwa mkutano wa 6 wa TICAD utatoa mwanga kwa changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara la Afrika kupitia Azimio la Nairobi mara litakapotishwa na kuanza kutekelezwa.

Kwa upande wa Tanzania Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Dkt. Susan Kolimba aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa Mawaziri. Wajumbe wengine waliohudhuria ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unatarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016 ambapo moja ya agenda ni kupitisha Azimio la Nairobi. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo.

Mkutano wa Sita wa TICAD unalenga kuiwezesha Afrika katika sekta ya uchumi na uwekezaji ambapo utawashirikisha pia wadau kutoka sekta binafsi zikiwemo Kampuni binafsi zaidi ya 300 kutoka Japan ili kufikia lengo hilo.

-Mwisho-