Sunday, August 28, 2016

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi wa Gesi


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa kwenye Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan lililofanyika Nairobi, Kenya wakati wa Mkutano wa TICAD VI. Kongamano hilo pia lilifuatiwa na hafla ya baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuingia makubaliano na Makampuni na Mashirika ya Japan katika kuimarisha biashara na uwekezaji. Mhe. Majaliwa alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa TICAD VI uliofanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyeji na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa TICAD VI akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan. Kushoto ni Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe na kulia ni Naibu Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto
Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe nae akizungumza kwenye Kongamano hilo
Baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu na Makamu wa Rais wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Kongamano la Biashara la Afrika na Japan. Kushoto ni Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Viongozi akiwemo Mhe. Majaliwa wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Mjumbe kutoka Chiyoda kuashiria Makubaliano kati ya Tanzania na Shirika la Chiyoda ambalo litashirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo kwa Wahandisi kwenye masuala ya gesi na mafuta. Waliosimama kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe; Bw. Francis Mossongo, Afisa Mwandamizi wa Dawati la Japan, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Shirika la Chiyoda.
============================================

Tanzania kushirikiana na Japan katika mafunzo kwa Wahandisi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameshiriki hafla iliyoashiria kusainiwa kwa makubaliano kati ya baadhi ya nchi za Afrika na Makampuni mbalimbali ya Japan iliyofanyika wakati wa Mkutano TICAD VI jijini Nairobi.

Hafla hiyo ambayo ilitanguliwa na Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan ilihusisha nchi 20 za Afrika ambazo zimeingia makubaliano ya kuimarisha uwekezaji na biashara na Makampuni makubwa 22 ya Japan.

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imeingia Makubaliano na Shirika la CHIYODA kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wahandisi wa Tanzania kwa kuwapitia mafunzo kwenye masuala ya teknolojia ya gesi na mafuta.

Akizungumza wakati wa Kongamano hilo Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta alisema kuwa Kongamano hilo ni jukwaa muafaka wakati Afrika ikiwa katika jitihada za mageuzi ya kiuchumi. Hivyo aliziomba nchi za Afrika kutumia ujuzi na uzoefu mkubwa wa Japan katika kuiimarisha Sekta Binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia maendeleo.

Aidha, aliongeza kuwa Kenya ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wenzake kuhakikisha kunakuwepo mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji kutoka nje hususan Japan. Pia aliishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa Afrika na kukaribisha uwekazaji kutoka sekta binafsi ya Japan kwenye maeneo ya uzalishaji wa nishati ya umeme na maeneo mengine.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe alisema kuwa Japan itaendelea kushirkiana na Afrika katika kuhakikisha inapiga hatua zaidi ya maendeleo. Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Afrika  na Japan Kampuni 22 na Vyuo Vikuu vya Japan zimefuatana nae ili kukamilisha mikataba 73 na nchi za Afrika. 

Aidha,  alieleza kuwa Kampuni za Japan zimetumia fursa ya Mkutano wa TICAD  VI kutangaza Azimio la Biashara ikiwa ni katika kuelezea nia na madhumuni yao katika kuchangia maendeleo ya Afrika.

Mbali na Tanzania nchi zingine za Afrika zilizoingia Makubaliano na Kampuni na Mashrika kutoka Japan ni pamoja na Kenya, Angola, Cameroon, Congo, Cote d’ Ivoire, DRC, Ethiopia, Misri, Ghana, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Seychelles, Afrika Kusini, Uganda na Zambia.

Wakati huohuo, Mkutano wa Sita wa Kilele wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) umemalizika   Jijini Nairobi leo huku Wakuu wa Nchi na Serikali wakipitisha kwa kauli moja Azimio la Nairobi na Mpango Kazi  wa utekelezaji wake.

Azimio la Nairobi pamoja na mambo mengine linalenga katika kutekeleza mambo makuu matatu  ambayo ni: Kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchumi ili kuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha uchumi huku mkazo ukiwekwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vitakavyozalisha ajira kwa wingi kwa vijana wa Afria; Kujenga mifumo ya Huduma za Afya ambazo ni endelevu kwa maisha bora ikiwemo kuboresha huduma za afya, kuweka mikakati ya kukabiliana na magonjwa kama Ebola, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na jamii nzima; na Kukuza na kuimarisha Utulivu na Ustawi wa Jamii.

Mbali na Mkutano wa Kilele wa TICAD VI, shughuli zingine zilizoenda sambamba na mkutano huo ni Kongamano la Biashara kati ya Afrika na Japan; Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan; na Mkutano wa Majadilino ya Kibiashara kati ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni Binafsi.

Mkutano wa TICAD VI ambao ulihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 30 kutoka Afrika, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda pia uliyashirikisha Makampuni zaidi ya 100 kutoka Serikali ya Japan, Sekta Binafsi na kuhudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 10,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

-Mwisho-



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.