Friday, July 29, 2022

TANZANIA, URUSI KUONGEZA MAENEO YA USHIRIKIANO

Serikali ya Tanzania na Urusi zimekubaliana kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji,utalii pamoja na utamaduni.

Makubaliano hayo yamefikiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mbarouk amesema kuwa Tanzania na Urusi zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kihistoria ambao uliasisiwa na Waasisi wa Mataifa hayo mawili…….“ kutokana na uhusiano mzuri tulionao umechangia kuimarisha sekta ya utalii, elimu pamoja na afya,” alisema Balozi Mbarouk

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Tanzania na Urusi zitaendelea kujikita zaidi kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii na masuala mengine ya kiuchumi kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.

Kwa upande wake Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia tangu aliwasili na kuongeza kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya mataifa mawili.

“Naamini kuwa mimi ni kiungo cha kuimarisha na kuendeleza uhusiano baina ya Urusi na Tanzania…..tumekuwa tukishirikiana katia sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu na afya utalii na utamaduni naahidi kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Balozi Avetsyan

Balozi Avetsyan ameongeza kuwa katika mwaka huu Serikali ya Urusi imepanga kutoa fursa za masomo kwa wanafunzi wa kitanzania takribani 70.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan


TANZANIA, USWISI KUENDELEZA USHIRIKIANO


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uswisi zimeahidi kuendeleza zaidi ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo teknolojia ya habari na mawasiliano, elimu, afya, ujenzi wa miundombinu, utawala bora na haki za binandamu, uhuru wa vyombo vya habari, kilimo na utalii kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. 

Ahadi hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uswisi iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2022. 


Waziri Mulamula alisema Tanzania na Uswisi zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na zimeendelea kushirikiana katika nyanja za teknolojia ya habari na mwasiliano, elimu, afya, ujenzi wa miundombinu, utawala bora na haki za binandamu, uhuru wa vyombo vya habari, kilimo na utalii. 

“Uswisi imekuwa mdau mkubwa katika masuala ya uchumi na kijamii ambapo kampuni mbalimbali kutoka Uswisi zimewekeza hapa nchini na zimekuwa zikichangia kutoa ajira kwa watanzania na kuongeza pato la taifa,” alisema Waziri Mulamula 

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot alisema Uswis imefurahishwa na ushirikiano mzuri inaoupata kutoka Serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa itaendelea kudumisha uhusiano huo kwa maslahi ya mataifa yote mawili

Balozi Chassota aliongeza kuwa Uswiss itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuunga mkono juhudi mbalimbali za kukuza maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania.

Hafla hiyo ilihudhuriwa Mabalozi mbalimbali na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, asasi za kiraia, na wafanyabiashara. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akitoa hotuba yake katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uswisi iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2022
Balozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot akitoa hotuba yake katika hafla ya kuandimisha Siku ya Taifa ya Uswisi iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2022
Hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uswisi iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2022 ikiendelea. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na alozi wa Uswisi nchini Mhe. Didier Chassot wakifurahia jambo kwenye hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uswisi iliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2022

Thursday, July 28, 2022

WAZIRI MULAMULA AMUAGA BALOZI WA PAKISTAN NCHINI TANZANIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemuaga Balozi wa Pakistan hapa nchini Mhe. Mohammad Saleem anayemaliza kipindi chake cha kuhudumu. 

Katika tukio hilo ambalo limefanyika kwenye Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam Waziri Mulamula amemshukuru Balozi Saleem kwa utumishi uliotuka na kumpongeza kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika utendaji wake ambayo yataacha alama na kumbukumbu ya kudumu kwenye historia ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Pakistan.

“Wazara na Serikali kwa ujumla tunajivunia utendaji wako, katika kipindi chako ulichohudumu hapa nchini licha ya kudumisha na kukuza uhusiano baina yetu na Pakistan umefanya kazi nzuri sana ya kuibua fursa na mikakati mbalimbali ambayo imeleta manufaa kwa wananchi wetu, kama vile fursa za nafasi za masomo, kuendeleza shughuli za uvuvi nchini na kukuza biashara baina ya Tanzania na Pakistan” Alisema Waziri Mulamula

Balozi Saleem kwa upande wake ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mzuri iliompa katika kipindi chote alichokuwa nchini kuteleza majukumu yake. Aidha ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini usimamizi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya ya kuleta maendeleo nchini. 

Waziri Mulamula amemuhakikishi Balozi Saleem kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Pakistan kwa manufaa ya maslahi mapana ya pande zote mbili.

Wakati huo huo Waziri Mulamula amempokea na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Mohamed Gaber katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. Wawili hao wamejadili musaula mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili ikiwemo uwekezaji, biashara, elimu na mafunzo, ushirikiano katika sekta ya utamaduni na michezo na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayotekelezwa na Kampuni za Misri hapa nchini.

Aidha wamekubaliana kuendelea kufuatilia utelezaji wa makubaliano na mikataba mbalimbali liyosainiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Misri mwezi Novemba 2021. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimsikiliza Balozi wa Pakistan anayemaliza kipindi chake cha kuhudumu nchini Mhe. Mohammad Saleem alipokuwa akimuaga katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam
Mazungumo baina Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula Balozi wa Pakistan anayemaliza kipindi chake cha kuhudumu nchini Mhe. Mohammad Saleem yakiendelea katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Mohamed Gaber wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Ubalozi na Wizara
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Mohamed Gaber wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Mohamed Gaber wakiwa katika picha ya pamoja

WAZIRI MULAMULA ASHIRIKI MKUTANO WA BARAZA LA AMANI NA USALAMA LA UMOJA WA AFRIKA KUJADILI HALI YA AMANI NA USALAMA NCHINI SOMALIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia hoja kwenye mkutano wa 1094 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Julai 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki Mkutano wa 1094 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Julai 2022. 

Mkutano huo ulilenga kupokea na kujadili taarifa ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu hali ya amani na usalama ya nchini Somalia na shughuli za Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (The African Union Transition Mission in Somalia –ATMIS).

Taarifa hiyo ambayo iliyowasilishwa na Mhe. Mahmoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Djibouti ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Julai 2022, pamoja na mambo mengine iliangazia masuala yafuatayo; Hali ya kisiasa ya nchini Somalia na kukamilika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu (political Development and update on National Elections), Hali ya Usalama na Maendeleo ya Shughuli za Pamoja katika Kusaidia Mpango wa Mpito wa Somalia na Usanifu wa Usalama wa Kitaifa.

Masuala mengine ni kuangazia hali ya Maendeleo katika utekelezaji wa Pendekezo la Pamoja na Dhana ya Uendeshaji, Masuala yanayohusiana na kuimarisha Hali ya Kibinadamu nchini Somalia na Ufadhili endelevu wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini SomaliaAkichangia katika mkutano huo Waziri Mulamula alianza kwa kumpongeza Mhe. Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Shirikisho la Somalia. Vilevile alitumia nafasi hiyo kuelezea matumaini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi hiyo baada ya kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi sasa kunawapa fursa na hali mpya ya kuweka nguvu katika kutekeleza mambo muhimu kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Mpito wa Somalia, kama vile kujenga taasisi za serikali, na kuongeza nguvu katika maandalizi ya makabidhiano ya serikali kwa amani na usalama. 

Aidha, Waziri Mulamula alitoa wito kwa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), Umoja wa Mataifa na Serikali ya Shirikisho la Somalia kufanya kazi kwa pamoja katika kushughulikia masuala muhimu yatakayo leta amani ya kudumu sambamba na kutazama suala la vikwazo vya silaha dhidi vilivyowekwa dhidi ya Somalia.

Mkutano huo umetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuzingatia kwa haraka maombi ya Serikali ya Shirikisho la Somalia kuhusu kuondolewa vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya nchi yao, ili kuiongezea nchi hiyo uwezo wa kutosha wa kukabiliana vilivyo na tishio la usalama linaloletwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Vilevile mkutano uliipongeza Serikali ya Shirikisho la Somalia kwa kumchagua Naibu Spika mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo. Pia ulisisitizo kuhusu umuhimu wa Serikali ya Somalia kuendelea kutambua nafasi ya wanawake, vijana, mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari katika mchakato wa mpito ambao utaifanya Somalia kufikia lengo la asilimia 30 kama ilivyokubaliwa katika Makubaliano ya Uchaguzi wa tarehe 17 Septemba 2020 na 27 Mei 2021. 

Tanzania ni miongoni mwa wajumbe 15 wa Baraza hilo. Wajumbe wengine ni Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Gambia, Ghana, Morocco, Namibia, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.
Mkutano wa 1094 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Julai 2022 ukiwa unaendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia jambo kwenye mkutano wa 1094 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Julai 2022

Wednesday, July 27, 2022

BALOZI MULAMULA AFUNGUA MAFUNZO YA UANDISHI WA HABARI ZA KIDIPLOMASIA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi Patrick Tsere alipowasili katika ufunguzi wa mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akifungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga na kushoto ni Kaimu Mkuu wa  Chuo cha Diplomasia Dkt. Anita Lugimbana


Balozi Peter Kalaghe akiwaeleza waandishi wa habari jinsi ya kuandika taarifa za kidiplomasia wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam

Watoa mada katika mafunzo ya waandishi wa habari nchini wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo uliofamywa na Waziri Mulamula hayupo pichani

Balozi Patrick Tsere (kushoto) akiwa na Balozi Mindi Masiga (kulia) wakimfuatilia Balozi Peter Kalaghe (hayupo pichani) akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo ya waandishi wa habari ya kuandika habari za kidiplomasia yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikianio wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam

Baadhi ya washiriki mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini wakimfuatilia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akifungua mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari ya kuandika habari za kidiplomasia yaliyoandaliwa na Wizara na kufanyika katika Chuo cha Diplomasia cha Dar es Salaam

Balozi Patrick Tsere akiongea na waandishi wa habari juu ya kuandika habari kwa kuzingatia uzalendo katika kulinda taswira ya Tanzania wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini yanayofanyika katika Chuo cha diplomasia jijini Dar es Salaam

Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango , Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Justine Kisoka akizungumza katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na wizara na kufanyika katika chuo cha diplomasia jijini Dar es salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (aliyekaa katikati) katika picha ya pamoja na waandishi wa habari nchini baada ya kufungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amefungua mafunzo ya uandishi wa habari za kidiplomasia kwa waandishi wa habari nchini.

Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam, Balozi Mulamula amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha wanaimarisha mahusiano kati ya wizara na vyombo vya habari.

'Tuwe pamoja siku zote tuendelee kushirikiana, vyombo vya habari ni wadau muhimu, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya nchi yetu,' alisema.

Amesema waandishi wa habari wanajukumu la kuilinda na kuitetea taswira ya Tanzania kupitia kazi zao na kuwataka waandishi wa habari nchini kuzingatia taswira ya nchi wakati wanatekeleza majukumu yao.
"Wanahabari, tuko hapa kuelimishana juu ya kuandika habari za kidiplomasia, niwaombe kwanza mhakikishe mnailinda taswira ya nchi, hii ni nchi yetu wote, ikiharibika taswira yake hata wewe uliyeandika pia utakutana na athari zake, hata uende wapi utajulikana kama Mtanzania. Mnapoandika mzingatie uzalendo na miiko ya taaluma ya uandishi wa habari," alisema Balozi Mulamula.

Pia aliongeza kusema mafunzo haya ambayo yatakuwa endelevu yanalenga pamoja na mambo mengine kutoa uelewa kuhusu masuala ya diplomasia ikiwemo Itifaki, Diplomasia ya Umma, Uzalendo na Mawasiliano ya kimkakati baina ya Tanzania na nchi zingine.

Kadhalika, aliwashukuru waandishi wa habari kote nchini kwa ushirikiano uliopo kati yao na wizara na kuwataka kuzingatia mafunzo yatakayotolewa kwao.


"Nawashukuru kwa ushirikiano na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Wizara na Sera ya Mambo ya Nje inayosisitiza katika Diplomasia ya Uchumi. Nawaomba mzingatie mafunzo haya kwani yatakuwa na tija kubwa kwenu," alisisitiza Balozi Mulamula.

Awali akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga alieleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini katika eneo la kuandika habari za kidiplomasia.

Amesema mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwani kufanya hivyo kutasaidia kuboresha uandishi na kuwa daraja kati ya Wizara na waandishi wa habari na hivyo kuwafikia wananchi wengi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yamewashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini.

 

 

 

 

WAZIRI MULAMULA ATOA WITO KWA AFRIKA KUTHAMINI MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA KUJENGA UCHUMI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa wito kwa Jumuya ya Afrika kutambua na kuthamini mchango wa Wanawake kwenye maendeleo ya uchumi. 

Waziri Mulamula ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Uchumi wa Wanawake Afrika (Pan-African Women Economic Summit 2022) uliofanyika tarehe 26 Julai 2022 jijini Dar es Salaam. Waziri Mulamula ameeleza kuwa pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na wanawake kwenye maendeleo, bado katika maeneo mengi barani Afrika hawatambui na kuthamini ipasavyo mchango huo hivyo kufifisha jitihaza za kundi hilo muhimu na lenye idadi kubwa barani katika kujenga uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mulamula aliendelea kubainisha kuwa endapo mchango wa wanawake ungetambuliwaingewapa motisha zaidi ya kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo kwenye jamii na kajikwamua dhidi ya umaskini uliokithiri na hali ngumu ya maisha. 

Pamoja na hayo Waziri Mulamula akifafanua zaidi hoja yake alieleza kuwa kutambua mchango wa wanawake kwenye uchumi ni muhimu kwa mamlaka mbalimbali kuanza kufikiria namna ya kuwavutia wanawake kuendesha shughuli zao katika sekta rasmi. 

"Wanawake wa Kiafrika ni wajasiriamali wa hali ya juu, wanamiliki theluthi moja ya biashara zote barani Afrika, Hata hivyo wajasiriamali wanawake wana uwezekano mkubwa wa kuendesha biashara ndogo ndogo katika sekta isiyo rasmi, wakijihusisha na shughuli za ongezeko la thamani la chini ambazo huvuna faida ndogo. Wanaelekea kuwa wajasiriamali wa lazima, badala ya fursa, wakiongozwa na biashara ndogo na ukosefu wa njia mbadala” Alisema Waziri Mulamula.

Kwa upande Mkurugenzi wa Tanzania Women CEO’s Roundtable Bi. Emma Kawawa akizungumza kwenye hafla ufunguzi wa mkutano huo, alieleza kuwa lengo la mkutano huo ni pamoja na kuwahamasisha wanawake kushiri katika shughuli rasmi za uzalishaji mali. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akipokelewa na Waandaaji wa Mkutano wa Uchumi wa Wanawake Afrika alipowasili katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam. Tarehe 26 Julai 2022
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Uchumi wa Wanawake Afrika wakifualia mjadala ulikokuwa ukiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja waandaaji na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Uchumi wa Wanawake Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisisitiza jambo wakati wa akifungua Mkutano wa Uchumi wa Wanawake Afrika (Pan-African Women Economic Summit 2022) uliofanyika jijini Dar es Salaam

Tuesday, July 26, 2022

BALOZI FATMA RAJAB AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA SERIKALI YA OMAN

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya Oman leo tarehe 26 Julai 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Oman kwakuwa nchi hizo  zinashirikiana katika sekta za biashara, kilimo, uwekezaji, utalii, afya, elimu, ujenzi wa miundombinu,madini na uvuvi.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya siku 6 na unaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi ambaye ameambana na viongozi wengine wa Serikali ya Oman.

Pamoja na Balozi Fatma Rajab, ujumbe huo pia umefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka pamoja na uongozi wa jiji la Dodoma ambapo, ulipata wasaa wa kutembelea kiwanja kilichotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujenga ofisi za Ubalozi wa Oman.

Aidha, tarehe 24 Julai 2022 ujumbe huo ulikutana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo ulifanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein  Ali Mwinyi. 

Ziara ya ujumbe huu ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Oman.

Hivyo, ujumbe huu upo nchini kufanya ufuatiliaji wa masuala ya utekelezaji katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa wakati wa ziara hiyo na kuangalia namna ya kuhuisha mikutano ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

=====================================

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akizungumza na Katibu Mkuu Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi leo tarehe 26 Julai 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima, mjumbe kutoka Serikali ya Oman na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mashariki ya Kati, Bw. Leonce Bilauri wakifuatilia mazungumzo.

Ujumbe uliombatana na Mhe. Wahaibi ukifuatilia mazungumzo.

Picha ya pamoja.

Balozi Fatma Rajab akimkaribisha Mhe. Wahaibi na ujumbe wake.


VACANCY ANNOUNCEMENT


 

WAZIRI MULAMULA AWAKUMBUSHA WASHIRIKA WA MAENDELEO KUTO ELEKEZA MIRADI UPANDE MMOJA WA NCHI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa washirika wa maendeleo nchini kuelekeza miradi na programu zao katika sehemu mbalimbali za nchi kulingana na mahitaji ya walengwa na vipaumbele vya taifa.

Waziri Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akifanya mazungumzo ya Balozi wa Austria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellner mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula ameeleza kuwa mara nyingi programu na miradi kutoka kwa washirikia wa maendeleo zinazolenga kuwawezesha wananchi katika shughuli za uzalishaji mali zimekuwa zikielekezwa upande mmoja wa nchi na kusahau maeneo mengine. 

"Tanzania ni nchi kubwa na kila sehemu ya nchi ni muhimu na inamchango wake katika maendeleo ya Taifa letu kulingana na mazingira yanayowazunguka, hiyo ni vyema miradi na programu zinazoandaliwa na washirika wetu wa maendeleo zilenge kuwawezesha wananchi wa pande zote za nchi badala ya kuelekeza nguvu upande mmoja. Alipendekeza michango hiyo ielekezwe kupitia Serikali Kuu" Alisema Waziri Mulamula

Sambamba na hayo Waziri Mulamula amemshukuru Balozi Fellner kwa msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali ya Austria wenye thamani ya Euro 50,000 uliokabidhiwa nchini jana tarehe 25 Julai 2022 na kupongeza mchango wa Serikali hiyo katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia programu mbalimbali wanazozifanya hapa nchini ikiwemo katika sekta ya afya, elimu, utalii, kilimo, usafirishaji na teknolojia. 

Vilevile Waziri Mulamula amemweleza Balozi Fellner kuhusu utayari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuendelea kushirikiana na Austria na hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kufungua na kuongeza maeneo ya ushirikiano na Dunia. Aliongeza kusema kuwa bado kuna fursa ya kuongeza maeneo ushirikiano hasa katika biashara, uwekezaji na utalii baina ya Tanzania na Austria.

Kwa upande wake Balozi wa Austria nchini Mhe. Christian Fellner ameeleza kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania sambamba na kuongeza nguvu zaidi katika kusaidia sekta ya elimu, ikiwemo kuanzisha na kuendesha programu za kuwajengea uwezo Wanafunzi na Taasisi za Elimu wa kufanya utafiti wa masuala mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.
================================

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimsikiliza Balozi wa Autria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellner mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (wa tatu kushoto) Balozi wa Autria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellner (wa pili kushoto) Balozi Swaiba Mndeme Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Wizarani na Ubalozi wa Autria.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Autria nchini Tanzania Mhe. Christian Fellnermwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Monday, July 25, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAWANOA WANAHABARI JUU YA MIKAKATI, MALENGO YA SADC

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuielimisha jamii juu ya mikakati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili waweze kutumia  fursa mbalimbali za kiuchumi kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola alipofungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine.

Balozi Kayola amesema waandishi wa habari wana mchango mkubwa katika kuhakikisha watanzania wengi hasa vijana wanafahamu umuhimu wa SADC na kutumia vizuri fursa zinazopatikana katika jumuiya hiyo.

"Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,"amesema Balozi Kayola.

Balozi Kayola ameongeza kuwa Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi na kuwasihi waandishi hao wa habarinkuhakikisha wanatumia lugha ya Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zao.

“Tanzania itaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu," ameongeza Balozi Kayola.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Kayola ameeleza mikakati mbalimbali ya Serikali ya Tanzania katika SADC ikiwemo kuwaenzi viongozi waanzilishi akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. 

Amesema wanahabari wana jukumu la kuifanya jamii ya Watanzania inafahamu majukumu, malengo na fursa zinazopatikana katika nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC.

Awali Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga aliwasihi waandishi wa habari pamoja na Maafisa Habari walioshiriki katika warsha hiyo kuhakikisha uelewa wanaoupata katika mafunzo hayo wanaielimisha jamii ya watanzania ili kuelewa mikakati na fursa za kiuchumi zinazopatika katika ukanda wa SADC.

“Vyombo vya Habari ni mhimili wa nne katika Serikali, hivyo nawasihi tujitahidi kuielimisha jamii yetu ili iweze kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika ukanda huo,” alisema Balozi Mindi.

Mafunzo ya waandishi wa habari nchini  yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola akifungua mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongea na washiriki wa mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani

Balozi mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Omar akiwasilisha mada katika mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mafunzo  ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani


Mwezeshaji wa masuala yanayohusu SADC, Bw. Chibamba Kanyama akizungumza na waandishi wa habari walioshiriki mafunzo mjini Bagamoyo Mkoani Pwani


Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mafunzo mjini Bagamoyo Mkoani Pwani

Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo Mkoani Pwani