Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya
mazungumzo na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
katika ofisi ndogo za Wizara leo tarehe 6 Julai 2022 jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Waziri
Mulamula amewahakikishia Wawakilishi hao kuwa Serikali inaendelea kuimarisha
ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza sekta za uzalishaji kwa maslahi mapana
ya Taifa.
‘’ Wizara kupitia Balozi zetu
nje imeendelea kuhakikisha fursa mbalimbali zinazopatikana nchini zinatangazwa katika
maeneo ya uwakilishi ili kuzihakikishia sekta hizo mageuzi makubwa ya kiuchumi” alisema Balozi Mulamula.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
TPSF, Bi. Angelina Ngalula pamoja na wajumbe alioambatana nao wameipongeza na
kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuweka mkazo wa kuinua sekta binafsi.
Akifafanua Bi. Ngalula ameeleza
juu ya uwepo wa mafanikio katika sekta za biashara, Utalii, uwekezaji, kilimo, madini,
huduma, uchukuzi na usafirishaji na ujenzi.
“Sisi sekta binafsi tunaishukuru
Serikali yetu kwa kuboresha mazingira ya biashara, sasa tunashuhudia mipaka
inafunguka sambamba na ongezeko la watalii kupitia jitihada za makusudi
zinazofanyika katika kuitangaza filamu ya “Tanzania the Royal Tour” alisema Bi.
Ngalula
Aidha, akafafanua matokeo
yaliyopatikana kupitia ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan, kwamba kupitia ziara hizo mikutano na makongamano ya
biashara yalifanyika katika nchi mbalimbali na yamesaidia kupatikana kwa washirika
wa kibiashara kutoka mataifa hayo.
Kupitia mazungumzo hayo Waziri
Mulamula na Wawakilishi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi, wamekubaliana
kuanzisha timu maalum ya uratibu na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya
kimkakati kitaifa, kwa lengo la kuimarisha na kukuza diplomasia ya uchumi
nchini.
Kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Balozi Mindi Kasiga akifafanua jambo katika mazungumzo hayo. |
Balozi Mulamula akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Bi. Ngalula vitabu vya Diplomasia ya Uchumi. |
Picha ya Pamoja. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.