Wednesday, July 20, 2022

WAZIRI MULAMULA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 24 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022. 

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwao ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Tathmini ya Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor amesema hali ya usalama katika kanda kwa ujumla inaridhisha na kwamba Nchi Wanachama wa SADC ziendelee kujitolea katika masuala ya ulinzi na usalama kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi hizo.

 

Kadhalika amesisitiza nchi wanachama kuendelea kupambana na ugaidi na vitendo vyote vya kigaidi katika Kanda huku akipongeza  Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya nchini humo ambapo wamefanikiwa kurejesha hali ya amani na usalama katika Jimbo la Cabo Delgado. 

 

Kuhusu utekelezaji wa maazimio yatokanayo na Mkutano wa 23 wa Kamati hiyo ya Mawaziri, Mhe. Dkt. Pandor amezipongeza Nchi Wanachama  na Sekretarieti ya SADC kwa kutekeleza maazimio hayo kwa takriban asilimia 81. 

 

“Utekelezaji huu bila shaka unadhihirisha dhamira ya dhati iliyopo miongoni mwetu ya kuhakikisha tunafikia lengo la kuimarisha amani na utulivu katika kanda”, alisema Mhe. Pandor.

 

Akizungumzia masuala ya demokrasia katika nchi wanachama, Mhe. Pandor amesisitiza nchi wanachama kuendelea kuendesha chaguzi zake kwa kufuata miongozo ya kidemokrasia ya SADC na ile ya nchi husika ili chaguzi hizo zikamilike kwa amani na utulivu.

 

“Katika kujenga amani na utulivu katika kanda, SADC itaendelea kuzingatia misingi ya demokrasia ili kuzuia migogogoro kwa maslahi mapana ya wananchi katika kanda. Kwa kuzingatia misingi hiyo SADC kama kanda itaendelea kuendesha chaguzi kwa kufuata misingi ya demokrasia, uwazi, amani na ukweli. Serikali za Angola na Lesotho zitakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Agosti na Oktoba mwaka huu mtawalia. Tunawatakia wanachama wenzetu uchaguzi wa amani” alisisitiza Mhe. Pandor.



Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi.

 

Pia alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Pandor kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia na kumwahidi ushirikiano.

 

Mbali na Mhe. Balozi Mulamula, Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawazirii wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 19 Julai 2022. Mkutano huo umemjumuisha pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Mhe. Lt. Jenerali Salum Othman na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi

 Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Dkt. Tax wakiwa wamesimama kwa heshima kutekeelza itifaki za ufunguzi wa mkutano ikiwemo kupigwa wimbo wa Taifa la Afrika Kusini na ule wa SADC
Mhe. Dkt. Tax akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab wakatib wa Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC
 

Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Mhe. Lt. Jenerali Salum Othman (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi kwenye Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC

Mkutano ukiendelea

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.