Monday, July 25, 2022

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAWANOA WANAHABARI JUU YA MIKAKATI, MALENGO YA SADC

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuielimisha jamii juu ya mikakati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili waweze kutumia  fursa mbalimbali za kiuchumi kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola alipofungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine.

Balozi Kayola amesema waandishi wa habari wana mchango mkubwa katika kuhakikisha watanzania wengi hasa vijana wanafahamu umuhimu wa SADC na kutumia vizuri fursa zinazopatikana katika jumuiya hiyo.

"Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,"amesema Balozi Kayola.

Balozi Kayola ameongeza kuwa Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi na kuwasihi waandishi hao wa habarinkuhakikisha wanatumia lugha ya Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zao.

“Tanzania itaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu," ameongeza Balozi Kayola.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Kayola ameeleza mikakati mbalimbali ya Serikali ya Tanzania katika SADC ikiwemo kuwaenzi viongozi waanzilishi akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. 

Amesema wanahabari wana jukumu la kuifanya jamii ya Watanzania inafahamu majukumu, malengo na fursa zinazopatikana katika nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC.

Awali Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga aliwasihi waandishi wa habari pamoja na Maafisa Habari walioshiriki katika warsha hiyo kuhakikisha uelewa wanaoupata katika mafunzo hayo wanaielimisha jamii ya watanzania ili kuelewa mikakati na fursa za kiuchumi zinazopatika katika ukanda wa SADC.

“Vyombo vya Habari ni mhimili wa nne katika Serikali, hivyo nawasihi tujitahidi kuielimisha jamii yetu ili iweze kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika ukanda huo,” alisema Balozi Mindi.

Mafunzo ya waandishi wa habari nchini  yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola akifungua mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiongea na washiriki wa mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani

Balozi mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Omar akiwasilisha mada katika mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola pamoja na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga wakifuatilia mafunzo  ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani


Mwezeshaji wa masuala yanayohusu SADC, Bw. Chibamba Kanyama akizungumza na waandishi wa habari walioshiriki mafunzo mjini Bagamoyo Mkoani Pwani


Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mafunzo mjini Bagamoyo Mkoani Pwani

Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya waandishi wa habari mjini Bagamoyo Mkoani Pwani



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.