Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeratibu msauala ya UVIKO-19,
Dkt. Ted Chaibans jijini Dar Es Salaam tarehe 5 Julai 2022.
Katika kikao hicho, Balozi
Mulamula alielezea hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania za kudhibiti
ugonjwa wa UVIKO-19 na kusisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea
kushirikiana na Tanzania kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Balozi Mulamula alisema
licha ya changamoto za uhaba wa miundombinu na ukubwa wa nchi, Serikali
imejitahidi kupambana na ugonjwa huo, hususan kwa kuhamasisha wananchi
wajitokeze kupata chanjo za UVIKO-19.
Balozi Mulamula
alihitimisha mazungumzo hayo kwa kukumbushia wito wa Serikali kuhusu kupata
msaada wa Jumuiya ya Kimataifa ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza azma
yake ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za Uviko-19 na magonjwa mengine.
Kwa upande wake, Dkt.
Chaibans alikiri kuwa licha ya Tanzania kuchelewa kuanza matumizi ya chanjo za
UVIKO-19 lakini imepiga hatua kubwa kuliko baadhi ya nchi zilizoanza mapema
kampeni za kuhamasisha chanjo. Alisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea
kuhamasisha watu kwa kubuni mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatumia
viongozi wa dini. Aliendelea kwa kutoa wito kwa Serikali ya Tanzania,
ihakikishe kuwa makundi ya kipaumbele kama Wazee, wenye maradhi ya kudumu,
watumishi wa sekta za afya, elimu na utalii wanahamasishwa ili wapate chanjo za
UVIKO-19.
Wakati huo huo, Balozi Mulamula amekutana na wajumbe wa Kamati ya Afrika ya Hydrogen inayojihusisha na uwekezaji katika nishati jadidifu (renewable energy). Wajumbe wa Kamati hiyo walimweleza Mhe. Waziri Mulamula utajiri wa vyanzo mbalimbali vya nishati ilivyonavyo Tanzania ambavyo vina fursa nyingi za kibiashara, endapo vitatumiwa vizuri. Kamati hiyo imeelezea utayari wa kufanya kazi na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa rasimali hizo zinatumika vizuri ili ziweze kuleta maendeleo endelevu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Kamati ya Afrika ya Hydrogen ambayo inajishughulisha na masuala ya kutoa ushauri na uwekezaji katika Nishati jadidifu (renewable energy).
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.