Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezisihi nchi wanachama 22 zinazoshiriki Warsha ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini Hali ya Mazingira ya Bahari kuhakikisha kuwa wanalinda mazingira ya bahari, kuongeza uelewa pamoja na kujenga uwezo juu ya utawala wa bahari.
Rai hiyo imetolewa na Dkt. Mpango leo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano hilo la siku tisa lililozikutanisha nchi 22 na washiriki zaidi ya 50 kwa lengo la kujadili usimamizi na utunzaji wa bahari.
Dkt. Mpango ameongeza kuwa vitendo vya kisayansi na teknolojia vinahitajika zaidi katika kusaidia kulinda mazingira ya bahari pamoja na ushirikishwaji wa wadau wote ikiwemo vijana na wanawake katika mijadala mbalimbali ya utunzaji wa mazingira ya bahari kwa kuwa wao ni sehemu ya suluhisho.
“Endapo tutasimamia bahari na mazingira yake itasaidia kuongeza wigo wa ajira na kusaidia mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini. Kuna hitaji la kuongeza hatua zaidi kulinda mazingira ya bahari na rasilimali zinazohusiana. Tunapaswa kufanya mabadiliko ya kuboresha usimamizi na utunzaji wa bahari,” alisema Dkt. Mpango.
Nawapongeza wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto zinazokabili mazingira ya bahari na pia kutekeleza lengo namba 14 la Maendeleo Endelevu SDGs ikiwa ni pamoja na ufadhili wa lengo hilo kwani utunzaji wa Bahari na mazingira yake ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ni matumaini yangu kuwa kupitia warsha hii, mtaimarisha ujuzi, uwezo wa kisheria na kisayansi katika nyanja ya masuala ya bahari ili kufikia Ajenda ya mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu katika muktadha wa masuala ya bahari.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema dunia inajielekeza kuangalia ni jinsi gani bahari kwa ujumla wake inaweza kuwa nyenzo ya kujenga uchumi na masuala mbalimbali ya kijamii hivyo warsha hiyo itajadili taarifa mbalimbali za mwenendo wa kiuchumi na kijamii kuhusiana na bahari.
“Kongamano hili litasaidia katika majadiliano ili kubadilishana uzoefu wa masuala ya bahari, kujengeana uwezo kwa watafiti mbalimbali na kujionea jinsi gani mataifa mengine yanatumia fursa za bahari kujenga uchumi na kuondoa umasikini kwa wananchi wake,” alisema Dkt. Jafo
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar, Dkt. Aboud Jumbe amesema kuwa mkutano huo unasaidia kuwakutanisha wataalam mbalimbali kutoka nchi wanachama kujadili fursa za kiuchumi na kijamii za bahari.
“Tunahitaji taarifa sahihi za kisayansi, kimazingira, kiuchumi lakini pia taarifa ambazo ni rahisi kumfikia mwananchi na kufahamu hali halisi ya mazingira yake lakini pia taarifa hizo ziweze kusaidia hususan wavuvi, usafiri wa baharini hivyo ni muhimu kuwa na taarifa hizo,” alisema Dkt. Jumbe
Kongamano hilo la masuala ya bahari limeratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Warsha ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini Hali ya Mazingira ya Bahari Jijini Dar es Salaam |
Washiriki wa warsha ya Umoja wa Mataifa ya kutathmini Hali ya Mazingira ya Bahari wakifuatilia warsha |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.