Wakuu
wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesisitiza umuhimu wa kujenga
miundombinu bora na ya kisasa ili kuweza kuyafikia malengo ya pamoja ya
maendeleo ya kiuchumi katika jumuiya.
Hayo
yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika mashariki aliyemaliza muda wake,
Mhe. Uhuru Kenyatta wakati wa hafla ya ufunguzi wa barabara ya kikanda ya Arusha
Bypass uliofanyika leo tarehe 22 Julai jijini Arusha na kuhudhuriwa na nchi zote
wanachana pamoja na mgeni mwalikwa Serikali ya Shirikisho la Somalia.
Pia
akafafanua kuwa barabara hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kupunguza
msongamano wa magari, itaongeza mawasiliano na muingiliano wa kijamii, itakuza
biashara, itarahisisha usafiri wa mizigo na kupunguza umasikini kwa nchi
wanachama na kujiletea heshima duniani.
Naye
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyeji wa mkutano huo, Mhe. Samia
Suluhu Hassan katika hotuba yake ameeleza kuwa barabara iliyozinduliwa ina urefu
wa kilomita 42.4 na imegharimu kiasi cha shilingi Billioni 197.4 na kwamba imejengwa kwa
ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.
Vilevile,
ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Japan (JICA) na Washirika wa Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki “East Africa Trademark” kwa kuendelea kutoa uwezeshaji wa kifedha kukamilisha kwa awamu ya kwanza ya mradi huo na kukubali kuendelea kuwezesha awamu ya pili
ya mradi wa barabara inayoanzia Arusha, Horiri, Taveta, Voi yenye urefu wa
kilomita 117.
Kadhalika,
Mhe. Rais Samia ametoa rai kwa wananchi kutumia fursa za miundombinu katika
kukuza sekta za utalii, biashara, uwekezaji, usafirishaji wa mizigo na
akawataka wananchi kutunza miundombinu iliyopo kuiwezesha serikali kuendelea na
ujenzi wa miundombinu katika maeneo mengine kama vile uimarishaji wa miundombinu ya
reli, bandari na usafiri wa anga.
Maboresho
hayo ya miundombinu yatawezesha kuiunganisha Afrika Mashariki na nchi nyingine
za Afrika na kulitumia vema soko la eneo huru la biashara la Afrika.
========================================
Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya EAC Arusha Bypass uliofanyika eneo la Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha tarehe 22 Julai 2022. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.