Friday, July 22, 2022

WAKUU WA NCHI ZA EAC WASISITIZA UMUHIMU WA SOKO LA PAMOJA KATIKA KUKUZA UCHUMI WA KIKANDA

 Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesisitiza umuhimu wa soko la pamoja katika kukuza uchumi wakati waliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Mkutano huo maalum wa ngazi ya Wakuu wa Nchi uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 na mkutano maalum wa ngazi ya Mawaziri uliofanyika tarehe 20 Julai 2022 jijini Arusha ni sehemu ya mikutano ya awali kuelekea Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.

 

Katika mkutano huo Wakuu wa Nchi walijadili na kuyawekea msisitizo masuala mbalimbali ya hali ya halisi ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na kuainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja katika kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo.

 

Akichangia mada wakati wa mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo, amesisitiza juu ya kukuza uzalishaji pamoja na  kuongeza thamani ya mazao na bidhaa  zinazozalishwa ndani ya jumuiya ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara kimataifa.

 

Aidha, aliongeza kufafanua kuwa katika kuyafikia malengo ya pamoja ni muhimu kwa nchi wanachama kuwekeza katika amani na utawala bora ili nchi ziweze kuongeza nguvu katika usimamizi wa rasilimali na uzalishaji badala ya kuwekeza katika migogoro.

 

Naye Mwenyekiti wa mkutano huo na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta amesisitiza umuhimu wa kuwa na mawasiliano kupitia ujenzi wa miundombinu ambao ndio msingi mkuu wa kuyafikia malengo ya soko la pamoja.

 

Vilevile akaeleza kwa sasa nchi wanachama zimeunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa na akatolea mfano ujenzi wa reli ya kisasa unaofanywa na Tanzania ambao utaziunganisha nchi wanachama na kwamba kwa upande mwingine Tanzania na Kenya zinaunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu uliofanywa mipakani katika eneo la Namanga na Taveta.

 

Maeneo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na fursa za kiuchumi zilizoongezeka kufuatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na jumuiya hiyo, umuhimu wa usimamizi wa rasilimali kama vile madini na umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuyafikia malengo yaliyowekwa.

 

Kadhalika, mkutano huo ulijadili mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya hiyo ikiwemo, uhuru wa kufanya biashara, mtangamano wa kijamii na fursa za kuvuka mipaka kupitia Hati ya kusafiria ya kielektroni ya Afrika Mashariki na kuondoleana visa miongozi mwa nchi wanachama.

 

Mkutano huo umehudhuriwa na Nchi zote saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni pamoja mwenyekiti wa mkutano huo Jamhuri ya Kenya; Mwenyeji wa mkutano huo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Jamhuri ya Uganda; Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Sudan Kusini, na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Pia ulihudhuriwa na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mkutano huo.


==========================================================



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwatambulisha viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Arusha tarehe 21 Julai 2022.
Mhe. Kenyatta yupo nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine aliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akimkaribisha Waziri anayeshughulikia masuala ya Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Barnaba Marial Benjamin mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha kushiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.
Mhe. Benjamin anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir katika mkutano huo pamoja na Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi wa EAC .



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba akifafanua kwa wananchi juu ya umuhimu wa soko la pamoja na fursa zake kwa taifa na wanachi wa Tanzania kwa ujumla kupitia kituo cha Luninga cha TBC1 .

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua juu ya fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wananchi kupitia kituo cha Luninga cha TBC1.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakifatilia majadiliano ya Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika.
Wapili kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akifuatilia Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 21 Julai 2022 jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.