Saturday, July 16, 2022

MAKATIBU WAKUU WA SADC WAANZA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 24 WA KAMATI YA MAWAZIRI

Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utafanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai, 2022. 

 

Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika tarehe 16 na 17 Julai 2022 ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kamati hii unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab ambaye anamwakilisha Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine. 

 

Mkutano wa 24 unalenga pamoja na mambo mengine kupokea na kujadili agenda mbalimbali zikiwemo mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 23 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya kanda; na tathmini ya hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda pamoja na Tathmini ya athari zitokanazo na mgogoro unaoendelea katika bara la Ulaya.

 

Viongozi wengine kutoka Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu ni pamoja na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Lt. Jenerali Salum Othman, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.

 

Ujumbe wa Tanzania kwa ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kuongozwa na Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ataambatana na Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu unaofanyika kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC MCO) utakaofanyika jijini Pritoria, Afrika Kusini kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai 2022.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu (kulia) na Mjumbe kutoka Sekretarieti ya SADC  wakati wa ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 16 na 17 Julai 2022 kwa ajili ya kuandaa Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.

Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Angola ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Sehemu ya Ujumbe wa Serikali ya Botswana ukishiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Wakati huohuo Mhe. Balozi Fatma ameongoza kikao kati yake na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu. Pichani Balozi Fatma akizungumza na ujumbe huo (hawapo pichani) kuhusu namna ya kushiriki kikamilifu kama Tanzania kwenye Mkutano wa 24 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.

Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa,  Kamishna wa Polisi Salum  Hamduni (kushoto) wakimsikiliza kiongozi wa ujumbe wa Tanzania, Balozi Fatma (hayupo pichani) wakati wa kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu

Viongozi wengine akiwemo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala (kushoto) wakati wa kikao cha maandalizi

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Shija akifuatilia kikao cha maandalizi cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Makatibu Wakuu

Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akishiriki kikao cha maandalizi kilichohusisha ujumbe wa Tanzania.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.