Thursday, July 7, 2022

DKT. MWINYI AZISIHI NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI KUBUNI MBINU ZA KUENEZA KISWAHILI

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kubuni mbinu bora za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda huo na duniani kwa ujumla.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Kiswahili Duniani lililoanza jana na kuhitimishwa leo Zanzibar ambapo amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuhakikisha kuwa zinashirikiana na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa mafunzo ya Isimu na Fasishi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mikakati madhubuti ya kuendeleza lugha ya Kiswahili Duniani.

“Natoa wito pia kwa taasisi za elimu ya juu kushirikiana na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia lugha ya Kiswahili kama fursa kwa vijana wetu kwani lugha hii ni kama bidhaa,” amesema Dkt. Mwinyi.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwinyi ameihakikishia Kamisheni ya Kiswahili na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa zitaendelea kuunga mkono jitihada za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani kote.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kuanzisha mabaraza ya Kiswahili ikiwa ni njia moja wapo mahsusi ya kukuza na kuendeleza lugha hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amesema kuwa ni lugha ya Kiswahili ni lugha ya kwanza kutumika katika shughuli rasmi za Umoja wa Afrika, pia ni lugha ya kwanza Afrika na ya nane duniani kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa

“Kutumia lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kutasaidia kuongeza umoja baina ya wananchi wa ukanda huo kuliko ilivyokuwa awali na kuongeza maelewano na baina ya nchi na nchi” amesema balozi Sokoine

Balozi Sokoine ameongeza kuwa, lugha ya Kiswahili ikitumika vizuri itasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya kisiasa, biashara, uchumi, elimu utamaduni na ustawi wa jamii.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Sokoine amezisisi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Masahriki kuongeza kasi ya kutangaza na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki” 

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma amezisihi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa wanakuza na kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha mabaraza ya Kiswahili

Dkt. Mwanahija ameongeza kuwa njia nyingine ya kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ni pamoja na nchi wanachama kuungana pamoja na Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya tafiti za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani limehudhuriwa na nchi wanachama sita kutoka ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda na Jamhuri ya Sudani kusini.

Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. Vilevile, Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika Mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.

Aidha, Mwezi Septemba, 2022 Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa  ulianza kuitangaza na kuisamba lugha ya Kiswahili, nchini Ufaransa kwa kushirikiana na Chama cha Watanzania Ufaransa (CCWU), ambapo ulianza kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa mwaka wa masomo 2021/22, ambayo yaliendeshwa na Kituo cha Utamaduni na Lugha cha Kitanzania (CCLT).

Washiriki wa matembezi kutoka ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakionesha baadhi ya Bendera za nchi wananchama wa Jumuiya hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika leo Zanzibar




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipokelewa na viongozi mbalimbali alipowalisi kuhitimisha Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar

   
Washiriki wa Kongamano la Kiswahili Duniani wakifuatilia Hotuba ya Rais wa Zanzibaar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa kufunga kongamano hilo leo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwasilisha Hotuba yake wakati wa kuhitimisha Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililohitimishwa leo Zanzibar



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria Kongamano la Kiswahili Duniani leo Zanzibar




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.