Friday, March 31, 2023

MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI AMALIZA ZIARA YA KIHISTORIA NCHINI


Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ameondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Kamala ameagwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ambaye aliongozana na Mhe. Mama Mbonimpa Mpango na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.

Mhe. Kamala ambaye kwenye ziara hii alifuatana na mwenza wake, Mhe. Douglas Emhoff pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani, pamoja na mambo mengine alikutana na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt Samia tarehe 30 Machi 2023 kwa mazungumzo rasmi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kwa pamoja walizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.

Kupitia ziara hii, Serikali ya Marekani na Tanzania zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, usalama wa mitandao, TEHAMA, Afya, usalama wa chakula, usafirishaji huku pia Marekani ikitangaza kutoa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Benki ya Exim ili kuwezesha upatikanaji wa kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.

Kadhalika Serikali ya Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.

Ziara ya Mhe. Kamala nchini ni matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, ililenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira, TEHAMA, usafirishaji, bandari na masuala ya utawala bora na demorasia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakati akimuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu nchini
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kwenye hafla ya kumuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku tatu nchini. 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Elsie Kanza kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakimuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango akiwa ameongozana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam  muda mfupi kabla ya kuondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake ya kihistoria ya siku tatu
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris  akisalimiana na Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol - CP) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Yusuph Mndolwa kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasiga kwenye hafla ya kumuaga Makamu huyo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff  wakiwapungia Watanzania walijiotekeza kumuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Thursday, March 30, 2023

TANZANIA NA MAREKANI ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani hususan kwenye sekta zinazochangia kuboresha maisha ya watanzania kama afya, elimu, kilimo, miundombinu, usalama wa chakula, demokrasia na utawala bora.

Mhe. Dkt. Rais Samia ameyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kumalizika kwa mazunguzo rasmi kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Amesema kupitia ushirikiano na Marekani, magonjwa kama Kifua Kikuu na UKIMWI sio tishio tena hapa nchini kwani kupitia program mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) maambukizi ya magonjwa haya kwa wananchi yamepungua kutoka asilimia 7.2 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017.

Kuhusu vifo vitokanavyo na Malaria, Mhe. Dkt. Rais Samia amesema vimepungua kutoka milioni 7.7 mwaka 2015 hadi kufikia vifo milioni 3.5 mwaka 2021.

“Lengo letu ni kutokomeza malaria kabisa katika jamii yetu ya Tanzania. Pia tunakaribisha wawekezaji wenye tija kutoka Marekani kuwekeza kwenye viwanda vya utengenezaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ili zitengenezwe hapa nchini kwetu", amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Mhe. Rais Dkt. Samia pia amesema anaikaribisha Marekani katika maeneo mapya ya ushirikiano hususan kwenye uvuvi katika bahari kuu, utafiti wa gesi na uchumi wa buluu.

Pia Mhe. Rais Samia ameiomba Marekani kupitia upya suala la utoaji visa ili kuwawezesha watanzania kupata visa za muda mrefu kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Kwa upande wake, Mhe. Kamala amesema Serikali ya Marekani inao Mpango mpya wa kushirikiana na Tanzania katika kusaidia miradi ya Teknolojia ya kidijiti, Usafirishaji na Nishati.

Amesema Serikali hiyo kupitia Benki ya Exim watasaini Hati ya Makubaliano na Tanzania ambayo itawezesha upatikanaji wa Dola za Marekani milioni 500 kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.

Vilevile amempongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha demokrasia nchini hususan kwenye masuala ya maridhiano na vyama vya siasa pamoja na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Amesema Marekani chini ya uongozi wa Mhe. Rais Joe Biden inaunga mkono agenda za kuimarisha Demokrasi anchini na itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano kama vile usalama wa chakula, afya, kuwasaidia wanawake na vijana Demokrasia na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile amesema katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania, Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.

Mhe. Kamala ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuchangia ulinzi wa amani duniani na kwamba nchi hiyo inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Tanzania katika kuhakikisha Kanda ya Maziwa Makuu inakuwa na amani na utulivu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakifurahia jambo alipowasili Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris alipowasili Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris akisaini kitabu cha wageni alipowasili Ikulu ya Dar es Salaam.
Mhe.Rais Dkt. Samia (kulia) akiongoza kikao kati yake na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris (kushoto) 


Wednesday, March 29, 2023

KAMALA AWASILI NCHINI

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris amewasili nchini tarehe 29 Machi, 2023 kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi, 2023.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijiji Dar es Salaam Mhe. Kamala amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Mhe. Kamala atapokelewa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao.

Vilevile, akiwa nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998. 

Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.

Katika ziara hii Mhe. Kamala amefuatana na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani.

Mapokezi ya Mhe. Kamala yameongozwa na Mhe. Dkt. Mpango na kumshirikisha Mama Mbonipa Mpango pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, Waziri wan chi, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya na Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla.
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akifurahia jambo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff wakiwasalimia Watanzania waliojitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwalaki walipowasili nchini usiku wa tarehe 30 Machi, 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipowasili nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakifurahia shamrashamra za mapokezi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akiwasalimia washereheshaji waliojitokeza kumpokea wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris wakibadilishana mawazo alipowasili  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Michael Battle
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Elsie Sia Kanza 
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  

Tuesday, March 28, 2023

TANZANIA, CUBA KUANZISHA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO


Tanzania na Cuba zimeaahidi kuaanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika nyanja za afya (chanjo), biashara na uwekezaji, uzalishaji wa mbolea na kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa katika kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Tax amesema kuwa kuanzishwa kwa maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kutasaidia kuimarisha ushirikiano uliodumu kwa takribani miaka 60 pamoja na kunufaisha wananchi wa mataifa yote mawili kiuchumi.

“Tunaamini kuwa kuanzishwa kwa maeneo mapya ya ushirikiano kutawanufaisha wananchi wa mataifa yote mawili kiuchumi, Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na Cuba kidiplomasi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Alisema Dkt. Tax

Mbali na maeneo mapya ya ushirikiano, Tanzania imekuwa ikishirikiana na Cuba katika sekta za afya, elimu, utalii, ulinzi na viwanda.

Kwa upande wake Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na imara baina yake na Serikali ya Cuba. 

“Tanzania imekuwa ikishirikiana na Cuba kwa muda mrefu na uhusiano huo umekuwa imara tangu ulipooasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo Hayati Fidel Castor na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” Alisema Balozi Vera. 

Cuba inaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha misingi ya kidiplomasia kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. “Ni wakati muafaka sasa Cuba na Tanzania kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha unakuwa na mafanikio ya kiuchumi kwa manufaa ya mataifa yote mawili,” aliongeza Balozi Vera. 

Tanzania ilianzisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Cuba mwezi Aprili 1963.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Mhe. Yordenis Despaigne Vera yaliyofanyika jijini Dar es Salaam walipokutana kwa mazungumzo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt.Stergomena Tax akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Mhe. Yordenis Despaigne Vera yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akifafanua jambo wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Mhe. Yordenis Despaigne Vera yaliyofanyika jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Jamhuri ya Cuba nchini Mhe. Yordenis Despaigne Vera wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara na Ubalozi mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Monday, March 27, 2023

DKT. TAX: ZIARA YA MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI NCHINI NI MATOKEO YA KUIMARIKA KWA DIPLOMASIA YA TANZANIA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris inayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na matokeo ya kuimarika kwa Diplomasia ya Tanzania.

 

Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Machi, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu umuhimu wa ziara ya Mhe. Kamala nchini na matarajio ya Tanzania.

 

Amesema ziara ya Mhe. Kamala nchini ambayo ni matokeo  ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, inalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira.

 

Pia amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ambao ulianza mwaka 1961 unaimarishwa na Program mbalimbali za ushirikiano  kati ya Tanzania na nchi hiyo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi.

 

Amefafanua kuwa Tanzania na Marekani zinashirikiana kupitia program mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupamana na Malaria (PMI) na Feed the Future.

 

Dkt. Tax ameeleza kuwa, Marekani kupitia Program ya PEPFAR imetangaza Bajeti ya miaka miwili ya kiasi cha Dola za 827,801,250 kwa Tanzania kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2024 hadi Septemba 2026. Utekelezaji wa program hiyo hapa nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na kuwezesha asilimia 88 ya watu wanaoishi na virusi kujua hali zao, na asilimia 95 kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.


Kuhusu uwekezaji wa Marekani nchini, Mhe. Tax amesema nchi hiyo kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imesajili jumla ya miradi 266 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 4,778.6 na kutengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania.

 

Akizungumzia ratiba ya Mhe. Kamala nchini, Mhe. Dkt. Tax amesema kuwa mara atakapowasili tarehe 29 Machi, 2023, Kiongozi huyo atapokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango.


Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Mhe. Kamala Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao.

 

Vilevile,  akiwa nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998. Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.

 

Mhe. Kamala na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe 31 Machi, 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza na kushoto ni Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo, Bw. Gerald Mbwafu wakifuatilia mkutao kati ya Mhe. Dkt. Tax na Wahariri
Mkutano ukiendelea


BALOZI MBAROUK AWATAKA VIONGOZI VIJANA KUSIMAMIA AGENDA YA KUONDOA UMASKINI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) – CCM Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amewaasa viongozi vijana kusimamia na kutekeleza agenda na mikakati ya kuondoa umaskini kwa vitendo. 

Balozi Mbarouk ametoa wito huo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana kutoka vyama vya Chama cha Mapinduzi (CCM), ANC- Afrika Kusini, SWAPO-Namibia, ZANU-PF – Zimbabwe, AMPLA – Angola, FRELIMO – Msumbiji, yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kibaha, Pwani. 

Balozi Mbarouk amewahimiza viongozi hao kutumia ujuzi na elimu watakayoipata katika mafunzo hayo ili kuleta mageuzi ya maendeleo kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii. 

“Vyama hivi rafiki vimefanya kazi nzuri ya kuleta ukombozi wa kisiasa, hivyo ni wakati muafaka sasa kwa viongozi vijana kutoka vyama hivi vikongwe barani Afrika kujikita katika kuondoa umaskini. Suala hili la kuondoa umasikini linapaswa kufanyika kwa vitendo, uadilifu na umoja kama ilivyofanyika katika kipindi cha kutafuta ukombozi,” alisema Balozi Mbarouk.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Marselina Mvula Chijoriga alisema mafunzo hayo pamoja na masuala mengine, ni jukwaa muhimu katika kuwaunganisha viongozi hao vijana, kubadilishana mikakati na uzoefu wa namna bora ya kuongoza jamii. 

Pamoja na mambo menhine, Balozi Mbarouk ambaye pia ni Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) – CCM amekipongeza chama rafiki cha Kikomunisti cha China (Chinese Communist Party) kwa kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na vyama hivyo na kufadhili baadhi ya mafunzo yanayotolewa katika Chuo hicho. 

Mafunzo hayo ya siku 14 (27 Machi hadi 7 Aprili 2023) yanajumuisha jumla ya washiriki 100, ambapo 26 kati yao wanatoka Tanzania.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) – CCM Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha, Pwani. 
Meza Kuu wakifurahia jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha, Pwani. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) – CCM Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akifungua mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha, Pwani. 
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM na watoa mada kwenye mafunzo ya uongozi kwa viongozi vijana yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha, Pwani. 
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya uongozi kwa ya viongozi vijana yanayotolewa katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha, Pwani.

Sunday, March 26, 2023

SAUDI ARABIA YAANZA RASMI SAFARI ZA NDEGE MOJA KWA MOJA HADI TANZANIA

Shirika la Ndege la Saudi Arabia limeanza rasmi safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudia Arabia hadi Tanzania. 

Akiongea katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kutoka Saudia hadi Tanzania ni moja ya matunda ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Saudi Arabia Mwezi, Juni 2022. 

“Kuanzishwa kwa safari hizi, kutachangia kuimarisha mazingira ya kibiashara na uwekezaji yatakayopelekea uhitaji wa usafiri wa anga wa moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Saudi Arabia,” Alisema Prof. Mbarawa

Prof. Mbarawa aliongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) za mwaka 2022, idadi ya abiria wa kimataifa nchini imeongezeka kwa asilimia 55 kutoka abiria 1,694,085 katika mwaka 2021 hadi kufikia abiria 2,618,119 mwaka 2022. 

“Awali abiria walilazimika kupitia mataifa mengine ili kufika Saudi Arabia, uzoefu unaonyesha kuwa walitumia takribani saa kumi ili kukamilisha safari zao. Hivyo, kwa kutumia Shirika hili, abiria wataweza kusafiri kwenda Jeddah moja kwa moja na watatumia saa Nne na dakika arobaini,” aliongeza Prof. Mbarawa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alisema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kutoka Saudia Arabia hadi Tanzania ni matokea ya uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya mataaifa hayo.

“Tunategemea kupitia safari hizi tutakuza na kuimarisha biashara, uwekezaji, viwanda na utalii nchini……..kwa sasa Urari wa biashara kati ya Tanzania na Saudia Arabia umefikia Dola za Kimarekani 18,000,0000,” alisema Balozi Mbarouk. Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa mbalimbali nchini Saudi Arabia hususan nyama, matunda na maua.

Naye Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bw. Fahad Alharbi alisema Saudi Arabia imefurahi kuanzishwa kwa safari hiyo ya kihistoria na yote hiyo imewezekana kutokana na uhusiano mzuri ilionao na Serikali ya Tanzania.

“leo tumeshuhudia uzinduzi rasmi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania. Ni Imani yangu kuwa safari hizi zitachangia kuimarisha biashara na uwekezaji, utalii pamoja na usafirishaji kwa kiasi kikubwa," alisema Bw.  Alharbi. Shirika la Ndege la Saudi Arabia litafanya safari zake kuja nchini mara nne kwa wiki. 

Februari, 2023 Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini na Meneja Mkuu wa Masoko, Kanda ya Kati wa Shirika la Ndege la Saudi Arabia Bw. Abdulrahman Alabdulwahab walikutana na kujadili maandalizi ya uzinduzi wa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Saudi Arabia.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia walijadili mikakati ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania ili kuongeza idadi ya watalii na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za Tanzania hususan nyama na matunda.

Hafla ya uzinduzi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania zilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini, Balozi wa Comoro Nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Ndege ya Shirika la Ndege la Saudi Arabia ikiwasili rasmi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania

Wageni wakipokelewa baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam

Picha ya pamoja 


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,akiwasilisha salamu za Wizara katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam
Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bw. Fahad Alharbi akitoa salamu za Saudi Arabia katika hafla ya mapokezi ya Ndege ya Shirika la Ndege la Saudia Jijini Dar es Salaam