Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Wakala wa Kitaifa wa Kukuza Uwekezaji (ANAPI) cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekutana kujadili fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania na DRC.
Akiongea Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Mifumo ya Habari wa TIC, Bw. Mafutah Bunini amesema ANAPI imekuja Tanzania kuelezea fursa za uwekezaji na biashara zinazopatikana nchini Kongo DRC.
“Kama tunavyofahamu Serikali ya Awamu ya Sita imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hivyo ndugu zetu wa DRC wamekuja kuangalia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania ili waweze kuwekeza zaidi,” alisema Bw. Bunini.
Bw. Bunini ameongeza kuwa Tanzania imejipanga kushirikiana na DRC kuwekeza katika sekta za kilimo hususan uzalishaji wa mbegu za mafuta, mazao ya chakula kama mchele, mifugo, madini, utalii pamoja na usafirishaji.
Amesema DRC Kongo ina wawekezaji wake Tanzania na ndiyo maana ANAPI imekuja hapa kuhamasisha wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza zaidi nchini Kongo, hivyo uwekezaji na biashara ni wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ANAPI, Bw. Anthony Nkinzo Kamole amesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuna fursa nyingi za uwekezaji hususan katika sekta za madini, usafirishaji, utalii, nishati, afya na viwanda.
“Tuna makubaliano ya biashara kati yetu (Kongo) na Tanzania na ndiyo maana tumekuja hapa kuelezea fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zinazopatikana nchini kwetu ili kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania kuwekeza zaidi Kongo,” alisema Bw. Kamole
Pamoja na Mambo mengine, Mkurungenzi Mtendaji wa ANAPI aliongeza kuwa “mazingira ya biashara nchini Kongo ni mazuri na yakuridhisha, kwanza tuna sera ya kulinda uwekezaji, tumeboresha pia taratibu za kujisajili kampuni nchini Kongo, tumepunguza kodi kwa wawekezaji ili kuwawezesha kufanya biashara na uwekezaji katika mazingira mazuri na salama zaidi kuliko ilivyokuwa awali,”.
Septemba, 2022 Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zilikutana katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kukubaliana maeneo ya ushirikiano yenye tija ya moja kwa moja kwa nchi hizo na watu wake hasa biashara na uwekezaji.
DRC imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta za miundombinu, nishati, utalii, elimu, afya, huduma za kifedha, biashara, uwekezaji, kilimo, maliasili na ufugaji. Aidha, zinashirikiana na kuungana mkono kwenye masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Sehemu ya Wafanyabiashara na wawekezaji wakifuatilia Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na DRC. Kongamano hilo limefanyika Jijini Dar es Salaam. |
Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Mifumo ya Habari wa TIC, Bw. Mafutah Bunini akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara |
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.