Saturday, March 11, 2023

TANZANIA NA NAMIBIA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

 

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri Namibia zimesaini Hati za Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya usalama, mishati na mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia. 

Hati za Makubaliano hayo zimesainiwa katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliomalizika jijini Windhoek, Namibia tarehe 10 Machi 2023 katika ngazi ya Mawaziri. 

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ambaye ameambatana na Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde(Mb.) na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.).

Kadhalika, ujumbe wa Jamhuri ya Namibia umeongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye ameambatana na Mawaziri wa kisekta na Makatibu Wakuu wa nchi hiyo.

Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia umejadili na kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi. Maeneo hayo ni pamoja na; Siasa na Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Uchumi, Nishati, Kilimo, Maendeleo na Miji, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Maliasili, Utalii na Mazingira, na Uvuvi, Afya, Elimu na Utamaduni.

Aidha, mkutano huu wa Mawaziri umewaagiza watendaji katika sekta za ushirikiano kukamilisha kwa wakati masuala yote yanayohitaji utekelezaji ndani ya muda ulioazimiwa na kikao hicho ili kuleta tija katika shughuli za wananchi na kuwainua kiuchumi.

Vilevile, wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Bara la Afrika kwa ujumla.

Wakihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Namibia Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah wamesisitiza umuhimu wa kukuza mawasiliano baina nchi hizo mbili ili kuweza kurithisha kizazi cha sasa juu ya historia ya mataifa hayo mawili na kufahamu ndoto kubwa waliyokuwa nayo waasisi wa matifa haya katika kuyafikia maendeleo ya watu wake.

Mkutano huu ulitanguliwa na mkutano wa awali wa ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 Machi 2023 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 9 Machi 2023.

Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia umeazimia kuwa mkutano ujao wa JCC utafanyika mwaka 2024 nchini Tanzania.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax  na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika masuala ya ulinzi, nishati na mashauriano ya kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia jijini Windhoek Namibia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax  na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa wakibadilishana Hati za Makubaliano baada ya kukamilisha zoezi la uwekaji saini wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia Jijini Windhoek.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax  na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa wakionesha Hati za Makubaliano zilizosainiwawakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia Jijini Windhoek..

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia jijini Windhoek. Katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa kufanyia kazi kwa wakati maazimio ya mkutano huo ili kuweza kujenga uchumi imara wa kisekta na kujenga mahusiano mazuri baina ya wananchi wa Tanzania na Namibia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa akihutubiwa wakati wa mkutano huo, ambapo pamoja na kuhimiza umuhimu wa kurithishwa historia ya ushirikiano wa Tanzania na Namibia amezitaka sekta zenye makubaliano ya ushiriano kufanyia kazi maeneo yote yanayohitaji utekelezaji ili Wizara za Mambo ya Nje ziweze kuratibu ushirikiano uliopo kwa tija na maslahi ya nchi hizo.

Kutoka kushoto, Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde(Mb.) na Naibu Waziri Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.)wakifatilia majadiliano katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Tanzania na Namibia uliofanyika jijini Windhoek, Namibia.

Ujumbe wa Tanzania, kushoto ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba akifatilia majadiliano katika mkutano huo.

Kutoka kushoto, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw. Ally Gugu, Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz na Afisa Mambo ya Nje, Bw. Makamba Makamba wakifatilia Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia uliofanyika jijini Windhoek, Namibia.

Ujumbe wa Tanzania

Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax  na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Naitwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Tanzania na Namibia, Makatibu Wakuu walioongoza ujumbe wa Tanzania na Namibia katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) ngazi ya Maafisa Waandamizi na Mabalozi wa Tanzania na Namibia.























 

 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.