Friday, March 24, 2023

TANZANIA – KOREA KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA KUKUZA BIASHARA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ameeleza kuwa Serikali na wadau inaendelea kuweka jitihada katika kuboresha mazingira ya biashara baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ili kuendelea kuinua kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili. 

Waziri Dkt. Tax ameeleza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo mapema leo tarehe 24 Machi 2023 jijini Dodoma. 

Dkt. Tax amemuhakikishia Balozi Kim kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Jamhuri ya Korea ili kuwezesha biashara baina ya pande hizo mbili inaendelea kushamiri zaidi tofauti na ilivyo sasa. Dkt. Tax ameeleza baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania ni pamoja na kuendelea kutekeleza na kubuni programu zinazolenga kuongeza mwingiliano wa watu (people to people exchange) kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea. 

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mwaka 2020, Korea iliagiza bidhaa zenye thamani ya shilingi za Tanzania bilioni 340.3 kutoka Tanzania, huku Tanzania ikiagiza bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 290.3 kutoka Jamhuri ya Korea.

Kwa upande wake Balozi Kim, Sun Pyo ameeleza kuwa Jamhuri ya Korea inaendelea kuwahamasisha watu wake kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini ikiwemo katika sekta ya kilimo, viwanda, ujenzi wa miundombinu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Utalii. 

Takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka saba (2015-2022), Korea imewekeza nchini dola za Kimarekani milioni 18.01 katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, ujenzi na usafirishaji na uchukuzi. Uwekezaji huo unakadiriwa kuzalisha fursa za ajira zipatazo 531. 

Mbali na hayo Waziri Tax ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha hali ya maisha ya watu ikiwemo elimu, afya, kuendeleza uchumi wa buluu, kilimo, Teknolojia ya Habari na ujenzi wa miundombinu. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo wakiwa katika picha ya pamoja walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma
 Mazungumzo yakiendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo yaliyofanyika jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo walipokuwa kwenye mazungumzo jijini Dodoma
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo wakiwa katika picha ya pamoja walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.