Tanzania
na Afrika Kusini zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika
sekta za fedha na uchumi, kilimo, madini, maji, utalii, siasa na diplomasia,
mawasiliano na uchukuzi, teknolojia ya habari, uchumi, nishati, elimu, wiwanda,
biashara na uwekezaji, ujenzi, utalii, kilimo, uvuvi, afya, elimu na utamaduni.
Makubaliano
hayo yamefikiwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano (Bi-National Cooperation) kati ya Tanzania na Afrika Kusini
unaofanyika tarehe 13 – 16 Machi 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Mkutano
huu uliofunguliwa katika ngazi ya Maafisa Waandamizi unafanyika tarehe 13 na 14 Machi 2023 pia ni mkutano wa awali kwa
ajili ya kuandaa taarifa zitakazopitiwa na kujadiliwa na mkutano ngazi ya
Mawaziri utakaofanyika tarehe 15 Machi 2023.
Mkutano
wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini
unalenga kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika
masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa kwanza wa
BNC uliofanyika mwezi Mei 2017 jijini Dar es salaam.
Akihutubia
wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania
katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na
Afrika Kusini, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab ameeleza kuwa
mkutano huu unatoa nafasi ya kupitia hali halisi ya utekelezaji wa maeneo ya
ushirikiano yaliyokubaliwa katika kikao cha kwanza na kuweka mikakati imara ya
kusonga mbele kimaendeleo.
“Kikao hiki kitahusisha majadiliano
yatakayowezesha kufikiwa kwa makubaliano katika maeneo mbalimbali ya
ushirikiano ya kisekta yatakayo rasimishwa kwa ajili ya utekelezaji na kuruhusu
maeneo mapya ya ushirikiano” alisema Balozi Fatma.
Vilevile,
akaeleza kuwa mkutano huu ni muhimu kwakuwa ushirikiano wa nchi zetu umejengwa
katika misingi imara iliyopiganiwa kwa jasho na damu tangu enzi za ubaguzi wa
rangi na hivyo BNC hiyo ni chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa
kiuchumi na kijamii katika maeneo yatakayokubaliwa.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini na
Mwenyekiti mwenza za kikao hicho Bw. Zane Dangor, alieleza kuwa BNC inatoa
fursa ya kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya biashara na
uwekezaji.
“Jukumu
letu ni kuimarisha ushirikiano katika masuala yenye maslahi makubwa kwa mataifa
yetu na kufungua fursa ya maeneo mapya ya ushirikiano” alisema Bw. Dangor.
Matarajio
ya Wenyeviti wa Mkutano huu ngazi ya Maafisa Waandamizi ni kuhakikisha wajumbe
wanawasilisha michango yenye tija ya kisekta katika majadiliano ili kuifikia
hatua ya juu ya kimaendeleo kupitia ushirikiano uliopo.
Pia
viongozi hao wamesisitiza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinauchukulia kwa
upekee ushirikiano huo kwakuwa nchi hizo zina masuala mengi ya kushirikishana
kupita uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC
na kwa lengo la kujenga uchumi wa kanda hiyo na Afrika kwa ujumla.
Tanzania
na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential
Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini Tume ya
Ushirikiano wa Pamoja (Bi-National Commission) ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.