Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa ziara ya Makamu wa Rais wa
Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris inayotarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia
tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na
Marekani na matokeo ya kuimarika kwa Diplomasia ya Tanzania.
Dkt. Tax ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Machi, 2023
Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu
umuhimu wa ziara ya Mhe. Kamala nchini na matarajio ya Tanzania.
Amesema ziara ya Mhe. Kamala nchini ambayo ni
matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha
ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, inalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha
ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile
biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira.
Pia amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya
Tanzania na Marekani ambao ulianza mwaka 1961 unaimarishwa na Program
mbalimbali za ushirikiano kati ya
Tanzania na nchi hiyo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia juhudi za Serikali
za kuboresha maisha ya wananchi.
Amefafanua kuwa Tanzania na Marekani zinashirikiana
kupitia program mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana
na UKIMWI (PEPFAR), Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupamana na Malaria (PMI) na Feed the Future.
Dkt. Tax ameeleza kuwa, Marekani kupitia Program ya
PEPFAR imetangaza Bajeti ya miaka miwili ya kiasi cha Dola za 827,801,250 kwa
Tanzania kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2024 hadi Septemba 2026. Utekelezaji wa
program hiyo hapa nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuenea kwa
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na kuwezesha asilimia 88 ya watu
wanaoishi na virusi kujua hali zao, na asilimia 95 kutumia dawa za kupunguza
makali ya ugonjwa huo.
Kuhusu uwekezaji wa Marekani nchini, Mhe. Tax amesema
nchi hiyo kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imesajili
jumla ya miradi 266 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 4,778.6 na
kutengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania.
Akizungumzia ratiba ya Mhe. Kamala nchini, Mhe. Dkt.
Tax amesema kuwa mara atakapowasili tarehe 29 Machi, 2023, Kiongozi huyo atapokelewa
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Mhe. Kamala Ikulu jijini Dar es Salaam
tarehe 30 Machi 2023 ambapo mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo ya
kuimarisha ushirikiano wa pande mbili baina ya viongozi hao.
Vilevile, akiwa
nchini, Mhe. Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar
es Salaam kama ishara ya kuwakumbuka wahanga wa mabamu yaliyolipuliwa kwenye
Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998. Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana pamoja nakushiriki
Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Rais Samia.
Mhe. Kamala na ujumbe wake wataondoka nchini tarehe
31 Machi, 2023
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023 |
Mkutano ukiendelea |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.