Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris ameondoka nchini baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya siku tatu iliyofanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi 2023 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mhe. Kamala ameagwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ambaye aliongozana na Mhe. Mama Mbonimpa Mpango na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax.
Mhe. Kamala ambaye kwenye ziara hii alifuatana na mwenza wake, Mhe. Douglas Emhoff pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Marekani, pamoja na mambo mengine alikutana na mwenyeji wake Mhe. Rais Dkt Samia tarehe 30 Machi 2023 kwa mazungumzo rasmi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kwa pamoja walizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano waliyofikia kwenye mazungumzo yao.
Kupitia ziara hii, Serikali ya Marekani na Tanzania zimeahidi kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, usalama wa mitandao, TEHAMA, Afya, usalama wa chakula, usafirishaji huku pia Marekani ikitangaza kutoa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Benki ya Exim ili kuwezesha upatikanaji wa kugharamia upelekeaji wa huduma na bidhaa katika sekta za miundombinu, usalama wa mitandao, usafirishaji, teknolojia ya kidigiti, nishati na miradi ya nishati jadidifu.
Kadhalika Serikali ya Marekani ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya nikeli yanayotumika kutengeneza betri za umeme wa magari ifikapo mwaka 2026.
Ziara ya Mhe. Kamala nchini ni matokeo ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, ililenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira, TEHAMA, usafirishaji, bandari na masuala ya utawala bora na demorasia.
Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakimuaga Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris alipokuwa akiondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake |
Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Harris na mwenza wake Mhe. Doug Emhoff wakiwapungia Watanzania walijiotekeza kumuaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.