Friday, September 30, 2022

WAZIRI KIJAJI AFUNGUA JUKWAA LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo tayari Mswada kuhusu mapendekezo ya Sheria mpya ya Uwekezaji umesomwa bungeni hivi karibuni.

 

Mhe. Kijaji ametoa kauli hiyo leo tarehe 30 Septemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.

 

Mhe. Dkt. Kijaji ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Jukwaa hilo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji kutoka nje kunufaika na fursa lukuki za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.

 

Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni mapendekezo ya Sheria Mpya ya Uwekezaji ambayo tayari imesomwa Bungeni  hivi karibuni. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.

 

Mhe. Dkt. Kijaji alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo ambayo tayari ipo wazi kwa umma wa watanzania kwa ajili ya kutoa maoni yao.

 

“Watanzania wenzangu, tunapokutana kwenye jukwaa hili la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, Serikali yetu ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji na tayari tumeileta kwa wananchi. Sheria hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine inapendekeza kushushwa kwa kiwango cha mwekezaji mzawa kutoka mtaji wa Dola za Marekani 100,000 hadi 50,000.  Hivyo niwaombe watanzania wa kada zote, wawekezaji, sekta binafsi ni wakati wetu sasa wa kutoa maoni yetu kuhusu sheria hiyo” alisema Dkt. Kijaji.

 

Mhe. Kijaji ametaja maboresho mengine yanayofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Biashara na uwekezaji kuwa ni pamoja na kuanzishwa mifumo ya kiteknolojia inayomrahisishia mwekezaji namna ya kuanza biashara, kupata namba ya mlipa kodi, leseni, viza na vibali vya kazi na ukaazi. Kadhalika serikali inakamilisha kuandaa mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo bandarini.

 

Akizungumzia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, amesema unaendelea vizuri ambapo hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 111 kutoka Italia yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 274.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa uwekezaji kutoka nje hapa nchini.

 

Pia amezitaka taasisi za Serikali na Binafsi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji hapa nchini kukutana na kuandaa taarifa ya pamoja ikijumuisha changamoto na mafanikio yaliyoainishwa wakati wa Jukwaa hili na kuzifanyia kazi changamoto hizo.

 

Akifunga Jukwaa hilo ambalo limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa hilo wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa kupitia jukwaa hilo na kuahidi kuendeleza jukwaa hilo ili kufikia malengo kusudiwa katika  utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

 

“Nawapongeza waandaji wa Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu  na sitalifunga bali nitaliahirisha ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia” alisema Balozi Mulamula.

 

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini Italia ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.

 

Naye Balozi wa Italia hapa nchini amesisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia majukwaa mbalimbali ya ushirikiano.

 

Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022. Jukwaa hili limewakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.   

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kikaji akifungua kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.

Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombp akizungumza wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi nae akizungumza wakati wa Jukwaa hilo

Sehemu nyingine  ya washiriki wakiwa kwenye mkutano

Sehemu nyingine ya Washiriki wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo
Mhe. Dkt. Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Kombo (kulia), Balozi wa Italia nchini, Mhe. Lombardi (kushoto) na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania jijini Milan, Italia, Bw. Cecil

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania, Italia na Balozi wa Italia nchini pamoja na Mabalozi wastaafu, Balozi Modest Mero (kulia aliyesimama) na Balozi James Msekela (kushoto)

 

TANZANIA, INDIA KUONGEZA USHIRIKIANO SEKTA YA FILAMU

Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya India zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo sekta ya filamu. 

Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), amesema ushirikiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umekuwa imara nyakati zote, na kwa sasa mataifa hayo yamekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika sekta ya filamu.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, maeneno mengine ambayo Tanzania na India zimekusudia kuongeza ushirikiano ni katika sekta ya filamu hasa katika kuwaendeleza wasanii wa Tanzania katika kujifunza zaidi masuala ya uzalishaji wa filamu bora kama wanavyofanya wenzetu wa India.

“Tumekubaliana na Balozi kuwa tufufue ushirikiano katika eneo hili muhimu ili kuwawezesha wasanii wetu hapa nchini kuwa na uwezo wa kutengeneza filamu zenye viwango kama wenzetu wa India,” amesema Balozi Mulamula

Awali Balozi Mulamula amesema ushirikiano wa Tanzania na India umekuwa imara wakati wote kutokana na misingi ya kihistoria iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere wa Tanzania na Baba wa Taifa la India, Mahatma Gandhi. 

Waziri Mulamula ameongeza kuwa misingi hiyo imesaidia kukuza ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta za elimu, afya, maji, ulinzi, utalii, tehama, kilimo, mabadiliko ya tabia nchi, nishati na uchumi wa buluu pamoja na biashara na uwekezaji. Alama ya ushirikiano katika nyanja hizo iliachwa na waasisi wa mataifa haya mawili (Mwl. Nyerere na Mahatma Gandhi) imekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na India nyakati zote kwa maslahi ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan ameongeza kuwa India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania, ambapo uhusiano huo umesaidia kuimarisha maendeleo baina ya mataifa hayo katika nyanja za elimu, afya, biashara na uwekezaji, kilimo na utamaduni.

“Ushirikiano uliopo baina ya India na Tanzania umekuwa chachu ya maendeleo kwa mataifa yetu na tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta za biashara na uwekezaji ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wetu,” amesema Balozi Pradhan 

Mwezi Agosti, 2022, Tanzania na India ziliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano ikiwemo kuhakikisha sekta za afya na nyingine zinaimarika ikiwemo kilimo.

Aidha, India kupitia hospitali ya Apollo zilisaini mkataba wa makubaliano (MoU) na Kampuni ya Eclipse Group Afrika ya Jijini Dar es Salaam wa kujenga kituo cha kisasa cha kutoa huduma za uchunguzi za magonjwa ya saratani kinachotarajiwa kuanza kujengwa nchini kuanzia mwezi Novemba 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan akiwasilisha hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam

Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India ukiendelea katika Ofizi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka ubalozi wa India nchini, ukiongozwa na Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Pradhan

Mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Kijamii na Utamaduni ya India, Bw. Arindam Mukherjee akiwasilisha hotuba yake wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India



Wednesday, September 28, 2022

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AFUNGUA KONGAMANO LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha Wawekezaji wenye tija  kuwekeza katika sekta  mbalimbali  ikiwemo sekta ya Uchumi wa Bluu.



Mhe. Othman ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.



Mhe. Othman ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye kongamano hilo amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali na kwamba inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuzifanyia maboresho sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji.

 

Kadhalika alisema maboresho hayo yanakwenda sambamba na yale ya sekta ya utoaji huduma kama vile za viza, vibali vya kazi na ukaazi pamoja na  kuboresha mawasiliano kupitia mifumo ya kidigitali ambapo Serikali hiyo inatarajia hivi karibuni kuzindua  mfumo wa uombaji viza kwa njia ya mtandao.



"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili  
kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo bora ya uwekezaji duniani. Uwekezaji una manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza pato la taifa pamoja na  kutenegeneza ajira kwa vijana na wanawake " alisema Mhe. Othman.



Mhe. Othman ameeleza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Novemba 2020 hadi wakati wa kongamano hilo Zanzibar imesajili miradi ya uwekezaji 196 yenye thamani ya dola za marekani bilioni 1. 4 ambapo miradi hiyo inatarajiwa  kutengeneza ajira zipatazo 9,000. Hivyo alihimiza washiriki kutumia  Kongamano hilo kama  chachu ya kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kuja nchini.  

 

“Kongamano hili liwe chachu ya kuvutia na kuhamasisha wawekezaji zaidi kuja Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naendelea kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji tulizonazo. Namaliza kwa kusema Wekeza Zanzibar, Wekeza sasa” alisisitiza Mhe. Othman



Awali akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amepongeza jitihada zinazofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Balozi mwenzake wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi za kuandaa kongamano hilo kwa mara ya pili ikiwa ni mchango wao wa  kuhakikisha nchi hizi mbili zinanufaika kupitia ushirikiano mzuri uliopo.

 

Pia aliwataka washiriki wote kutumia kongamano hilo kama fursa ya kubadilishana  mawazo na uzoefu miongoni mwao ili kuendelea kuboresha sekta ya biashara na uwekezaji  nchini. 

 

 Mhe. Soraga  pia alitumia fursa hiyo kuainisha fursa za kipaumbele za uwekezaji Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya Uchumi wa  Bluu, Kilimo, Usindikaji wa mazao ya kilimo, Utalii, ufugaji wa samaki, utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira , miundombinu, nishati na uwekezaji katika mali zisizohamishika kama majengo.


Wakati wa Kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo Maendeleo ya Miundombinu, Uchumi wa Bluu na Kilimobiashara na Kilimo cha Kisasa cha kutumia mashine na mitambo. Kongamano hilo ambalo limewashrikisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji wa hapa nchini na kutoka Italia litahitimishwa rasmi tarehe 30 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam.

 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akifungua rasmi Kongamano la Pili la Uwekezajikati ya Tanzania na Italia lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar tarehe 28 Septemba, 2022. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Othman ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Italia na duniani kote kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali za manufaa
Sehemu ya Washiriki wa Kongamano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga nae akizungumza wakati wa Kongamano hilo

Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mhe Soraga

Mkurugezni Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) akifafanunua fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Zanzibar

Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi (katikati)

Sehemu ya washiriki wa kongamano

Sehemu nyingine ya washiriki

Mhe. Balozi Lombardi akizungumza na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi.  Leluu Abdallah (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Baraka  


 


VACANCY ANNOUNCEMENT


 

Tuesday, September 27, 2022

KONGAMANO LA PILI LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA ITALIA KUFANYIKA ZANZIBAR

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema takribani wawakilishi wa Kampuni 1,000 za nchini Italia wamethibitisha kushiriki kwenye Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji linalotarajiwa kufunguliwa rasmi jijini Zanzibar tarehe 28 Septemba 2022.

 

Akizungumza leo tarehe 27 Septemba 2022 jijini Zanzibar wakati wa mkutano wa maandalizi uliokuwakutanisha Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia na Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Kombo amesema mwitikio huo mkubwa wa washiriki wa kongamano kutoka Italia unatokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi katika kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii nchini humo. 

 

“Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umeendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji, utalii na biashara zilizopo nchini. Ni kutokana na jitihada hizo Kampuni nyingi zimehamasika na kuonesha nia ya kuja kujionea fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zitakazowasilishwa wakati wa Kongamano hili. Nimefarijika sana kuona mwitikio huu wa washiriki kutoka Italia ambao umezidi ule wa kongamano la kwanza” amesema Balozi Kombo.

 

Kadhalika ameongeza kusema kuwa tayari zipo Kampuni kadhaa za Italia zimewekeza nchini ikiwemo ile ya Toscana Macchine Calzature (TMC) iliyopo mkoani Kilimanjaro inayojishughulisha na uuzaji wa mashine za kisasa na vipuri vyake vya utengenezaji wa viatu na bidhaa na ngozi. Amesema Kampuni hiyo ambayo huzalisha viatu zaidi ya jozi 4,000 kwa siku, imeonesha utayari wa kutoa wataalam saba (7) watakao toa mafunzo ya utengenezaji bidhaa za ngozi katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar.

 

Vilevile, Balozi Kombo ameeleza kuwa, kutokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii hapa nchini safari za ndege za watalii kutoka Italia zimeongezeka kutoka safari tatu hadi nane kwa wiki.

 

Balozi Kombo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za soko la bidhaa kama Parachichi ambazo tayari zimeanza kuuzwa nchini Italia. 

 

Kwa upande wake, Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana Tanzania katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.

 

Kongamano hilo ambalo litafunguliwa rasmi tarehe 28 Septemba 2022, linalenga  pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina namna ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia sekta ya biashara na uwekezaji. Pia kutoa nafasi kwa Tanzania kuainisha fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini zinazoweza kuchangamkiwa na washiriki kutoka Italia.

 

Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa Kongamano la Kwanza la aina hii lililofanyika jijini Rome, Italia mwezi Desemba 2021, linatarajiwa kuhitimishwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.


Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiwa na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi wakiongoza kikao cha maandalizi ya Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia kilichowakutanisha Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Italia kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu mahitaji ya wawekezaji hao na fursa zilizopo nchini. Kikao hicho kimefanyika Zanzibar tarehe 27 Septemba 2022. Kongamano hilo litafunguliwa rasmi mjini hapa tarehe 28 Septemba 2022.
Mhe. Balozi Lombardi akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya Kongamano la Pili la Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

Washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia wakati wa kikao baina yao

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bw. Sharif Ali Sharif akifuatilia kikao


Bw, Daniele Ferradini, Meneja Mauzo wa Kampuni ya TMC ya Italia inayojishughulisha na uuzaji mashine za kutengenezea viatu na bidhaa za ngozi iliyopo Kilimanjaro akichangia jambo wakati wa kikao
Kikao kikiendelea

Kikao kikiendelea

Sehemu ya Maafisa Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia kikao

Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Salma Baraka akinukuu mazungumzo wakati wa kikao

Kikao kikiendelea

Mwekezaji kutoka Italia akizungumza wakati wa kikao

Mwekezaji kutoka Italia akichangia jambo wakati wa kikao

Picha ya pamoja