Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Maendeleo Ushirikiano na Biashara ya Nje Mhe. Ville Skinnari jijini New York na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Findland.
Akizungumza katika kikao hicho Balozi Mulamula ameelezea nia ya Tanzania kushirikiana na Finland katika maeneo ya uendelezaji wa miundombinu, ICT, Kilimo na utunzaji wa mazao ya kilimo, nishati, gesi na biashara ya hewa ukaa.
Amesema Tanzania inaliona suala la miundombinu kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kama jambo litakaloziunganisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini na hivyo kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika kanda hizo.
Amesema suala la uwepo na upatikanaji wa uhakika wa nishati za umeme na gesi ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali inayatilia mkazo kwani inaamini kuwa yakikamilika yatavutia wawekezaji wengi nchini na hivyo kukukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla na ndio maana serikali inawekeza nguvu kubwa katika maeneo hayo
“Uwepo na upatikanaji wa uhakika wa nishati za umeme na gesi ni moja ya maeneo ambayo, Serikali inayatilia mkazo na yakikamilika yatavutia wawekezaji wengi zaidi nchini na kukukuza uchumi wetu kwa ujumla na ndio maana serikali inaweka mkazo kukuza na kuimarisha maeneo hayo,” amesema Balozi Mulamula
Akiongelea suala la kuimarisha sekta ya kilimo nchini Balozi Mulamula amesema Serikali inalichukulia kwa umakini mkubwa suala hilo na ndio maana imekuwa ikiongeza bajeti yake kila mwaka ili kuifanya sekta hiyo ikue kwa kasi na hivyo nchi kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza nje na hivyo kukuza kipato chake na cha wananchi kwa ujumla
Kuhusu eneo la ICT Balozi Mulamula amesema Serikali inatoa kipaumbele katika eneo hilo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya mafunzo ili kuwa na wahitimu wengi watakaokidhi mahitaji ya viwanda nchini na hivyo kuzalisha kisasa zaidi
Naye Waziri wa Finland Mhe. Skinnari amesema Finland iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya uendelezaji wa miundombinu hasa katika mpango wa upanuzi wa bandari ya Dar es salaam na kuifanya kuwa lango kubwa katika ukanda wa kusini na Afrika Mashariki na kuangalia namna ya kuwa na maeneo ya kilimo bora zaidi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula nchini.
Ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya biashara, uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu ya ICT kwa kushirikiana na wadau wao mbalimbali.
Mawaziri hao wako jijini New York kuhudhuria Mkutno wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaoendelea nchini Marekani
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.